Tanga. Changamoto ya wazazi wengi kushindwa kugharamia mahitaji muhimu ya watoto njiti wanaolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo imeendelea kuwa kikwazo katika jitihada za kuhakikisha watoto hao wanapata huduma stahiki za kuwasaidia kuishi na kukua salama.

Hali hiyo imebainika Juni 23, 2026 wakati Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Tanga ilipofika hospitalini hapo na kukabidhi msaada wa mahitaji mbalimbali kwa watoto njiti, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 ya utoaji wa huduma wa mamlaka hiyo.

Watoto njiti ni miongoni mwa makundi yanayohitaji uangalizi maalumu tangu wanapozaliwa kutokana na uzito mdogo na changamoto mbalimbali za kiafya zinazoweza kujitokeza katika hatua za awali za maisha yao.

Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo, Muuguzi Kiongozi Idara ya Watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo, Mtawa Rukia Mbega, amesema msaada huo umefika wakati mwafaka kutokana na wazazi wengi wa watoto njiti kushindwa kumudu baadhi ya mahitaji muhimu ya watoto wao wanapokuwa katika uangalizi maalumu.

Amesema wodi hiyo hupokea watoto wengi wanaohitaji huduma za karibu kila siku huku baadhi ya wazazi wakitoka katika familia zenye uwezo mdogo wa kiuchumi.

Wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, TRA Mkoa wa Tanga wakiwa katika harakati za kubeba mahitaji kwa ajili ya kuwakabidhi wazazi wa watoto njiti katika hospitali ya Mkoa wa Tanga Bombo ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 30 ya TRA. Picha na Mbonea Herman.

“Msaada huu ni muhimu sana kwa watoto wetu. Wazazi wengi wanaowaleta watoto hawa hawana uwezo wa kukidhi mahitaji yote yanayohitajika wakati wa matibabu na uangalizi wa watoto njiti,” anasema Mbega.

Ameongeza kuwa wadau mbalimbali wa maendeleo pamoja na wananchi wanapaswa kuendelea kuikumbuka wodi hiyo kwa misaada ya kijamii ili kuwasaidia watoto hao pamoja na wazazi wao wanaopitia kipindi kigumu baada ya kujifungua.

Ofisa Muuguzi katika hospitali hiyo, Nuru Omari amesema hospitali hiyo hupokea watoto njiti kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Tanga kwa ajili ya kupata huduma maalumu zinazowasaidia kuendelea kuishi.

Amesema watoto hao hupatiwa huduma mbalimbali ikiwemo kuongeza kiwango cha sukari mwilini pamoja na kusaidiwa kupumua kwa kutumia mashine maalumu hadi wanapofikia uzito unaoruhusiwa kuruhusiwa kurejea nyumbani.

Amefafanua kuwa baada ya kuruhusiwa, watoto hao huendelea kufuatiliwa katika kliniki maalumu ya ukuaji hadi wanapofikia uzito wa kilo tatu kabla ya kuhamishiwa katika huduma za kawaida za kliniki.

Zaidana Mparu mama mwenye watoto njiti ambao ni mapacha amesema alikuwa ana wasiwasi mkubwa baada ya kuambiwa atajifungua watoto mapacha wakiwa na muda wa miezi saba, lakini kwa sasa wanaendelea vizuri  kutokana na huduma wanazopatiwa za malezi katika hosipitali hiyo

”Nilipewa rufaa kutoka katika wilaya ya Handeni kuja hapa Bombo baada ya madaktari kunipa rufaa kutokana na hali yangu waliniambia kutokana na dalili nilizokuwa nazo huenda nikajifungua chini ya muda wenyewe kufika kweli imekuwa hivyo na sasa ninaendelea vizuri na watoto wangu mapacha,” anasema Zaidana.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Naibu Kamishna wa Huduma za Kiufundi kutoka Makao Makuu ya TRA, Ted Silkiluwasha amesema katika jamii ya Watanzania bado kuna makundi yenye mahitaji maalumu yanayohitaji kusaidiwa ili yaweze kuishi katika mazingira bora.

Kamishna wa Huduma za Kiufundi kutoka Makao Makuu ya TRA, Ted Silkiluwasha katikati akikabidhi mahitaji kwenye hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo kwa ajili ya watoto njiti ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 30 ya mamlaka hiyo. Picha na Mbonea Herman.

“Sambamba na kuimarisha taifa, hatupendi kumuacha mtu yeyote nyuma. Miaka 30 ya TRA imewezekana kutokana na walipa kodi, na mamlaka inatambua kuwa uhai wa walipa kodi ndio uhai wa TRA. Ndiyo maana tumeamua kutoa msaada huu kwa watoto njiti kama sehemu ya kurudisha kwa jamii inayochangia maendeleo ya taifa kupitia kodi,” amesema Silkiluwasha.

Amesema Julai Mosi mwaka huu TRA itatimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake ikiwa na kauli mbiu ya “Tanzania kwa Pamoja Tunajenga Taifa Letu”, huku mamlaka hiyo ikiendelea kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii zinazogusa maisha ya wananchi.

Naye Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Castro John, amesema mamlaka hiyo inaamini kuwa kila Mtanzania ni mlipa kodi wa sasa au wa baadaye, hivyo hata watoto waliotembelewa ni sehemu ya kizazi kitakacholijenga taifa hapo baadaye.

Amesema mtazamo huo ndio unaoifanya TRA kushiriki katika shughuli za kijamii zinazolenga kuwafariji na kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu.

Katika msaada huo, TRA imekabidhi sabuni, nepi, maziwa ya unga na vifaa vingine muhimu vinavyotumika katika kuwahudumia watoto njiti wanaopatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *