
Dar es Salaam. Walalamikaji katika kesi ya madai ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali usio sawa ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kati ya Tanzania Bara na Zanzibar wameibua tena maombi ya zuio dhidi ya chama hicho kufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali za chama.
Maombi hayo yanatokana na kesi ya msingi iliyofunguliwa tena Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, ikiwa ni mwendelezo wa kesi ya awali iliyofutwa kutokana na kasoro za kisheria.
Kesi hiyo ya madai namba 13832 ya mwaka 2026 imefunguliwa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema Zanzibar, Said Issa Mohamed, na mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis.
Wadaiwa katika kesi hiyo ni Bodi ya Wadhamini Waliosajiliwa wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.
Kutokana na kesi hiyo pia walalamikaji hao wamefungua shauri dogo la maombi ya zuio la muda dhidi ya walalamikiwa wao, wakiiomba mahakama itoe amri ya kuwazuia kujishughulisha na shughuli za kisiasa na kutumia mali za chama mpaka kesi hiyo itakapoamuliwa.
Shauri hilo limetajwa leo Jumanne, Juni 23, 2026 mbele ya Jaji Awamu Mbagwa anayesikiliza kesi hiyo, na maombi hayo. Ameelekeza wajibu maombi wawasilishe mahakamani majibu yao ya maandishi na kiapo kinzani kabla au kufikia Julai 2, 2026, na akapanga kusikiliza shauri hilo pande zote Julai 6, 2026.
Katika kesi ya msingi, walalamikaji wanadai kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara, kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya chama hicho.
Madai mengine ni ubaguzi wa kidini na kijinsia, pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga Muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hivyo, pamoja na mambo mengine, wanaomba mahakama isitishe kwa muda shughuli zote za kisiasa mpaka maagizo ya mahakama yatakapotekelezwa, na kutoa zuio la kudumu la matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi walalamikiwa watakapotekeleza matakwa ya sheria husika.
Kesi hiyo ilitajwa Juni 15, 2026 kwa mara ya kwanza kwa ajili ya kuangalia kama ubadilishanaji wa nyaraka umeshakamilika na mahakama kutoa maelekezo muhimu.
Wakili Nshala alikiri kuwa wajibu maombi hawajawasilisha majibu yao dhidi ya madai ya wadai na kwamba bado walikuwa ndani ya muda wa siku 21 za kisheria zinazoishia Julai Mosi, 2026, tarehe ambayo alisema ndiyo waliyopanga kuwasilisha majibu yao.
Jaji Mbagwa alikubaliana na hoja hiyo na akaelekeza wadaiwa wawasilishe majibu yao kabla au kufikia Julai Mosi, 2026 na akapanga kesi hiyo itajwe kwa mara nyingine Julai 8, 2026.
Kesi ya awali, kesi ya madai namba 8323 ya mwaka 2025, ilifunguliwa mahakamani hapo na Mohamed, Khamis na Maulida Anna Komu (marehemu kwa sasa), ambaye pia alikuwa mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar.
Pia walifungua shauri la maombi madogo ya zuio la muda dhidi ya walalamikiwa, wakiomba mahakama iwazuie kufanya shughuli za siasa na kutumia mali za chama kusubiri kuamuliwa kwa kesi hiyo.
Juni 10, 2025, mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Hamidu Mwanga aliyekuwa akiisikiliza kesi hiyo, alikubaliana na maombi hayo baada ya kuyasikiliza upande mmoja kutokana na wakili wa wajibu maombi hao (walalamikiwa) kujiondoa siku hiyo kwenye kesi hiyo.
Hivyo alitoa amri ya zuio dhidi ya chama hicho kupitia kwa walalamikiwa hao, kutokujihusisha na shughuli za kisiasa wala kutumia mali za chama kusubiri uamuzi wa kesi hiyo.
Hata hivyo, amri hiyo ilibatilishwa na Mahakama ya Rufani Aprili 15, 2026 baada ya kutumia mamlaka yake kufanya mapitio ya kesi hiyo pamoja na mashauri madogo yaliyotokana na kesi hiyo, kufuatia barua iliyoandikwa na Chadema wakilalamikia mwenendo wa kesi na mashauri hayo.
Katika uamuzi huo, Mahakama ya Rufani ilisema kuwa baada ya wakili wa wajibu maombi kujiondoa, mahakama haikuwa sahihi kuendelea na usikilizwaji wa maombi hayo upande mmoja na kwamba wajibu maombi, kutokana na kutokuwa na wakili wa kuwawakilisha, walinyimwa haki ya kusikilizwa.
Hivyo ilibatilisha mwenendo wa shauri hilo kuanzia pale wakili wa wajibu maombi alipojitoa mpaka uamuzi wa zuio hilo.
Kisha Mahakama ya Rufani iliamuru kesi isikilizwe na jaji mwingine na ikaelekeza jaji huyo aanze kusikiliza na kuamua kwanza pingamizi la walalamikiwa.
Katika pingamizi hilo, walalamikiwa walikuwa wakidai kuwa kesi hiyo haipaswi kusikilizwa wakidai kuwa imefunguliwa nje ya muda kinyume na Sheria ya Ukomo wa Muda, kutokana na hati ya madai kutokubainisha muda ambao mambo waliyokuwa wakiyalalamikia yalitokea.
Pingamizi hilo lilisikilizwa na Jaji David Ngunyale Mei 2026 na Mei 28, 2026. Katika uamuzi wake, alikubaliana na hoja ya Chadema kuwa hati ya madai haibainishi kuwa mambo wanayolalamikia yalianza lini, jambo ambalo alisema linaifanya mahakama ishindwe kuona kama ina mamlaka ya kuisikiliza au la.
Hivyo, kutokana na kasoro hiyo, Jaji Ngunyale aliitupilia mbali kesi kabla ya kuisikiliza madai ya msingi.
Hata hivyo, siku chache tu baada ya kesi hiyo kufutwa, wadai hawa wawili walirudi mahakamani hapo ambapo walifungua upya kesi hiyo baada ya kurekebisha kasoro za kisheria zilizobainishwa na mahakama, na wakafungua tena maombi hayo ya zuio.
Wakati kesi hii ya sasa ikisubiriwa kusikilizwa, tayari Chadema Zanzibar kimeshatangaza kumvua uanachama Mohamed.