Dar es Salaam. Muziki umeendelea kuwa sehemu muhimu ya maisha ya kila siku. Utafiti mpya uliofanya na QS Supplies mwaka 2025 unaonesha kuwa hata shughuli za faragha kama kuoga na kutumia choo zimegeuka kuwa sehemu maalum za kusikiliza nyimbo mbalimbali.
Utafiti huo wa QS Supplies kwa kushirikisha washiriki 1,000 kutoka Uingereza na Marekani pamoja na uchambuzi wa zaidi ya nyimbo 300,000 kutoka orodha za Spotify, zinazohusiana na kuoga, kuogelea bafuni na matumizi mengine ya bafuni. Umebaini kuwa asilimia 27 ya watu husikiliza muziki wanapooga au wanapokuwa bafuni.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, sababu kuu zinazowafanya watu kusikiliza muziki wakiwa bafuni ni kujiburudisha na kujiondoa kwenye mawazo ya kawaida ya kila siku. Asilimia 56 ya washiriki walieleza kuwa hutumia muziki kama njia ya burudani na kujisahaulisha.
Huku asilimia 53 wakisema huwasaidia kupumzika na kuondoa msongo wa mawazo. Aidha, asilimia 44 walibainisha kuwa muziki huwapa nguvu na kuboresha hali yao ya hisia.
Utafiti huo pia unaonyesha kuwa tabia ya kusikiliza muziki haipo tu wakati wa kuoga, bali pia wakati wa kutumia choo. Ingawa haukutaja asilimia mahsusi ya watu wanaosikiliza muziki chooni pekee. Matokeo yake yanaonyesha sehemu ya watu hutumia muda huo wa faragha kusikiliza nyimbo wanazopenda ili kupunguza kuchoka, kuongeza utulivu au kufanya muda uonekane mfupi zaidi.
Utafiti huo pia umeonyesha kuwa muziki wa Pop ndio unaopendwa zaidi wakati wa kuoga na kutumia muda bafuni. Takribani asilimia 40 ya wasikilizaji walichagua aina hiyo ya muziki kama chaguo lao kuu.
Huku wasikilizaji wa Uingereza wakionyesha mapenzi makubwa zaidi kwa Pop kuliko wenzao wa Marekani. Kwa upande mwingine, Wamarekani walionekana kuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kusikiliza muziki wa EDM wakati wa kuoga.
Katika orodha ya wasanii wanaotawala playlist za bafuni, mwimbaji Taylor Swift aliongoza kwa kuwa msanii anayesikilizwa zaidi katika mazingira hayo. DJ na mtayarishaji wa muziki Avicii alitajwa kuwa msanii wa EDM anayependwa zaidi katika playlist za kuoga.
Kwa upande wa nyimbo, ‘Sweater Weather’ ya The Neighbourhood iliongoza kama wimbo unaosikilizwa zaidi wakati wa kuoga na hata katika muda wa bafuni kwa ujumla. Ikiwemo wakati wa kutumia choo.
Nyimbo nyingine zilizojitokeza zaidi ni ‘The Night We Met’ ya Lord Huron, ‘505’ ya Arctic Monkeys, ‘Do I Wanna Know?’ ya Arctic Monkeys, ‘Mr. Brightside’ ya The Killers, ‘Riptide’ ya Vance Joy, ‘I Wanna Be Yours’ ya Arctic Monkeys, ‘Somebody Else ya The 1975, ‘Take Me To Church’ ya Hozier na ‘Yellow’ ya Coldplay.
Kwa upande wa mabafu ya kujiloweka (bathtub), ‘Flowers’ ya Miley Cyrus iliongoza kama wimbo unaopendwa zaidi kusikilizwa wakati wa kuoga kwa mtindo huo.
Watafiti wanaamini kuwa matokeo hayo yanaonyesha jinsi muziki ulivyozidi kuwa sehemu ya utaratibu wa kila siku wa binadamu. Kutoka kuanza siku kwa kutumia nguvu nyingi, kupunguza msongo wa mawazo hadi kuongeza furaha. Muziki unaendelea kuwa rafiki wa karibu hata katika nyakati za faragha zaidi.