YANGA inajua msimu huu imekwamishwa na wachezaji wake wapya kushindwa kuonyesha ubora, sasa kuna hesabu kali zinapigwa juu ya kuboresha eneo la kiungo zikimuhusisha kiungo wao wa zamani Stephanie Aziz KI iwapo dili hilo likikwama tu kuna mashine inatua kutoka Uganda.

Mabosi wa Yanga wanapiga hesabu za kumrudisha staa wao wa zamani Aziz KI ambaye kwasasa anaichezea klabu ya Al Ittihad ya Libya, iliyomnunua kutoka Wydad Athletic ya Morocco ambayo awali ndio ilimnunua raia huyo wa Burkina Fasso kutoka Yanga.

Yanga imempa kazi Aziz KI kuhakikisha anamalizana na Walibya hao, kama anataka kuweka hai dili hilo la kurejea nchini na kiungo huyo ameshaanza kupambana na mabosi wa klabu yake kufanikisha jambo hilo akiona kama akirejea kwenye Ligi Kuu Bara atarudisha makali yake.

Aziz KI tayari yupo hapa nchini kwenye mapumziko ya mwisho wa msimu na juzi alionekana akiwa na bosi mmoja wa juu wa Yanga, Antony Mavunde ambaye ni Waziri wa Madini pia ni mjumbe wa bodi ya wadhamini ya klabu hiyo.

Mavunde ana urafiki mkubwa na Aziz KI ambapo Mwanaspoti linafahamu kuwa kigogo huyo ndiye anayezungumza na Aziz KI juu ya shauku yake ya kurejea nchini, kwenye klabu yake hiyo iliyompa mafanikio makubwa.

Hata hivyo Yanga haijaweka akili yake kwa Aziz KI pekee, ambapo mabosi wa klabu hiyo wamezungumza na kiungo mmoja fundi raia wa Uganda, Abdul Karim Watambala ili kama watamkosa Mbukinabe huyo basi wafanye hesabu za haraka kumchukua.

Watambala anaichezea Vipers ya Uganda, alikotoka Allan Okello, amekubali kila kitu kuhusu ofa ya Yanga na anasubiri uamuzi yao tu ili wamalize dili hilo.

Watambala ndiye mchezaji bora wa Ligi ya Uganda msimu uliomalizika (MVP) akiwa amefunga mabao 12 na kutengeneza asisti nne, na kumfanya kuhusika kwenye jumla ya mabao 16.

“Mpaka sasa hakuna uhakika wa moja kama hesabu za Aziz KI zitafanikiwa kukamilika, kila mtu hana mashaka na ubora wake, akirudi litakuwa jambo kubwa, lakini tusubiri kuona atamalizana vipi na klabu yake,”alisema bosi huyo wa juu wa Yanga.

“Hatuwezi kusubiri uamuzi huo tu tunaendelea kutafuta machaguo mengine, kuna yule Watambala kama tukimkosa Aziz tunaona atatufaa  naye ni mzuri sana wa kuchezesha timu, tunataka mtu mwenye ubunifu mkubwa na anayejua kufunga.

Yanga inamtumia Okello kumlainisha kiungo huyo ambapo hesabu hizo zimekubali sasa kinachosubiriwa ni uamuzi ya mwisho ya mabosi hao wa klabu hiyo kinara wa mataji nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *