KUNA wakati pesa inakupa kile unachotaka, na ni mara chache inaweza kukunyima kile unachotamani. Azam FC imepata kile inachotaka baada ya kufanikiwa kumbakisha kocha wao Florent Ibenge, ambaye alishachukua dili jipya la miaka miwili na matajiri hao wa Chamazi.

MALI PESA HAITOSHI

Azam ilifanikiwa kumtoa Ibenge kwenye tamaa ya kufundisha timu yenye hadhi kubwa ya Mali, ambayo ilikaribia kabisa kumchukua kocha huyo Mkongomani, likabaki suala moja tu kuhusu uhakika wa malipo yake.

Chama cha Soka nchini Mali baada ya kusikia mahitaji ya Ibenge, kikaomba siku chache kukutana na serikali ya nchi hiyo kuidhinisha bajeti ambayo kocha huyo aliihitaji kabla ya kukubali mkataba wao. Kosa lao kubwa likawa hapo.

Azam iliposikia hayo ikaangalia namna ilivyoanza kuona njia ya mafanikio kwa muda ambao Ibenge amekaa nao kwa msimu huu tu. Likawa jambo rahisi, likatanua bajeti yao na kumpa mkataba mnono zaidi kocha huyo, na mambo yakamalizikia hapo Mali ikiachwa mezani.

Hata hivyo, mkataba mpya wa Ibenge, ambao utaanza kutumika msimu ujao, una vitanzi vitano vizito ambavyo kocha huyo wa zamani wa AS Vita (DR Congo), RS Berkane (Morocco) na Al Hilal Omdurman (Sudan), atatakiwa kuvipigania kuipa mafanikio Azam.

UBINGWA LIGI KUU

Azam iliwahi kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara mwaka 2014 ikiwa chini ya kocha Mcameroon Joseph Omog, msimu ambao ilizifanyia vibaya klabu nyingine kwa kuchukua taji hilo bila kupoteza mchezo wowote.

Baada ya kuchukua ubingwa huo, haikuwahi tena kukaribia kuchukua ubingwa huo, ikipita miaka 12 bila kurudia mafanikio hayo. Mfupa huo sasa unahitaji meno ya Ibenge ili kuuvunja na kwenda kutafuta taji hilo la pili kwa Azam FC, akiwa na kipengele hicho kwenye mkataba wake kuanzia msimu ujao.

Msimu huu ni mgumu kwa Ibenge kupata ubingwa huo kutokana na hesabu zinazoonyesha inawezekana, lakini uhalisia unaiondoa Azam kwenye mbio za taji hilo, ikihitaji zaidi maombi ya timu zilizo juu yake Yanga na Simba kuanguka, huku yenyewe ikitakiwa kushinda mechi zote.

KUPASUA KATI YA SIMBA NA YANGA

Msimu huu ambao Ibenge ameanza na Azam, bado timu hiyo imeendelea kubaki nyuma ya vigogo Yanga na Simba katika msimamo wa ligi, lakini hata kwenye mataji mengine yaliyomalizika tayari, yakiwemo Kombe la Muungano ambalo Simba ililibeba, Ngao ya Jamii iliyoenda kwa Yanga, na Kombe la Mapinduzi lililochukuliwa na Yanga.

Azam wanatamani sana kuona timu yao ipo juu ya vigogo au, ikishindikana, basi ikae kati ya timu hizo kubwa mbili. Ibenge ameachiwa jukumu hilo na mabosi wake wamemhakikishia mahitaji yake wakitaka kuona linatimia kuanzia msimu ujao ndani ya miaka miwili atakayokuwa kwenye benchi la klabu hiyo.

UBINGWA FA

Ukiacha ubingwa wa ligi, Ibenge aliyezaliwa miaka 64 iliyopita, Azam inalitaka Kombe la Shirikisho la CRDB ambalo mara ya mwisho ililichukua mwaka 2019 kutoka kwa Mtibwa Sugar, waliolichukua mwaka 2018.

Yanga ndio vinara wa taji hilo kwa kulitwaa mara nne (2016, 2022, 2023, 2024), ikifuatiwa na Simba waliolichukua mara tatu (2017, 2020, 2021).

Ibenge anaweza kuanza kurahisisha mkataba wake mpya msimu huu baada ya kuiwezesha Azam kutinga fainali kwa kuing’oa Yanga kwenye nusu fainali iliyopigwa CCM Kirumba jijini Mwanza kwa ushindi wa mabao 3-2 baada ya dakika 120.

Azam itakutana na Simba kwenye fainali itakayochezwa Julai 4. Kama Ibenge atabeba taji hilo, litakuwa la kwanza kwake tangu atue nchini, na pia atakuwa ametimiza mtego wa kwanza wa mkataba wake mpya mapema kabla ya kuanza kuutumikia.

ROBO FAINALI AFRIKA

Ibenge msimu huu wa kwanza ndani ya Azam alifanikiwa kimataifa baada ya kuipeleka timu hiyo kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, ikiwa ni mara ya kwanza kwa kikosi hicho kufika hatua hiyo.

Azam muda mrefu ilikuwa ikisota kwenye hatua za awali za mashindano ya Afrika, lakini Mkongomani huyo akaibadilisha. Mkataba wake mpya unamtaka kuipeleka timu hiyo mbali zaidi, akiwekewa angalau hatua ya robo fainali.

Ikumbukwe Ibenge amewahi kuchukua taji la Kombe la Shirikisho akiwa na RS Berkane msimu wa 2021-22, walipoing’oa Orlando Pirates ya Afrika Kusini kwa mikwaju ya penalti 5-4 baada ya sare ya 1-1 ndani ya dakika 90.

Msimu wa kwanza wa Ibenge ndani ya Azam hakufanikiwa sana kwenye usajili, ambapo wachezaji wengi aliowasajili walishindwa kufanya makubwa, wengi wakionekana kuwa na viwango vya kawaida.

Hata hivyo, jambo kubwa ambalo matajiri hao wa Chamazi linawapa ahueni ni namna kocha huyo alivyowapa nafasi na thamani wachezaji vijana kutoka timu za vijana za klabu hiyo.

Azam tayari imeanza maandalizi ya usajili wa msimu ujao, ambapo viongozi wanaohusika na usajili wanamshirikisha kocha huyo kwa kiasi kikubwa katika kuanza kutengeneza kikosi chake cha msimu ujao.

Iwapo Ibenge atashindwa tena kuleta wachezaji bora na Azam ikaendelea kuyumba uwanjani, hilo linaweza kumtia matatani mbele ya mabosi wake, ambao wanataka kikosi tishio kitakachoweza kufikia malengo yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *