Ezekiel Kyama ni miongoni mwa sura zilizobeba simulizi ya maandamano ya Juni 25.

Chanzo cha picha, Ezekiel Kiama/BBC

”Tulikuwa na hasira kwa sababu hakuna aliyekuwa anatusikiliza”, Kijana ambaye alikatiza masomo yake ya chuo kikuu baada ya maandamano ya kupinga mswada wa fedha wa 2024 anasimulia maisha yalivyobadilika siku hiyo.

Leo, Juni 25, ni miaka miwili tangu Kenya ishuhudie moja ya siku zilizoacha alama kubwa katika historia yake ya kisiasa.

Maelfu ya vijana wa Gen Z walijitokeza mitaani kupinga Mswada wa Fedha wa mwaka 2024, wakidai kuondolewa kwa ushuru waliodai ungeongeza ugumu wa maisha na wakitaka uwajibikaji zaidi serikalini.

Lakini kumbukumbu ya siku hiyo bado inawaandama wengi.

Kwa baadhi ya familia, Juni 25 ni siku waliyoagana na wapendwa wao bila kujua kwamba wangewaona kwa mara ya mwisho. Kwa wengine, ni siku iliyoacha machozi, majeraha na maswali ambayo hadi leo hayajajibiwa.

Na huku taifa likiendelea kutafakari kilichotokea, mmoja wa vijana waliokuwa katikati ya matukio hayo ameamua kuvunja ukimya wake.

“Tulikuwa na hasira kwa sababu hakuna aliyekuwa anatusikiliza”

Ezekiel Kyama ni miongoni mwa sura zilizobeba simulizi ya Juni 25.

Picha zake zilienea kwa kasi mitandaoni baada ya kuingia ndani ya Bunge la Taifa wakati waandamanaji walipovunja vizuizi vya usalama na kuingia katika moja ya majengo yenye ulinzi mkali zaidi nchini.

Akiwa ameketi kwenye kiti cha Spika, alisikika akisema:

“Mr Speaker, Sir, Ruto must go.”

Takriban miaka miwili baadaye, bado anakumbuka kila dakika ya siku hiyo.

“Asubuhi nilienda maandamano nikakutana na marafiki. Tukaingia bungeni kwa sababu tulikuwa na hasira kuwa serikali haikutaka kutusikiliza,” anasema.

Anasema hali ilibadilika zaidi baada ya Bunge kupitisha Mswada wa Fedha.

“Ilipofika saa sita au saa saba, vijana walipata motisha mpya. Watu walikuwa wakiangushwa, wanabebwa juu huku wengine wakisonga mbele. Polisi walikuwa na kila kitu cha kuzuia maandamano, mabomu ya kutoa machozi, marungu na kila aina ya vifaa vya usalama, lakini vijana walikuwa wengi.”

Licha ya hali ya taharuki, Kyama anasisitiza kuwa wao hawakuingia bungeni kwa lengo la kuharibu mali.

“Tulikuwa tunaingia katika nyumba inayojengwa na kodi yetu. Watu waliomo ndani wanalipwa kwa kodi yetu. Chakula wanachokula kinanunuliwa kwa kodi yetu. Tulikuwa tunasema tumekuja kwa amani.”

Lakini maandamano hayo yaligeuka kuwa ya umwagaji damu.

“Vijana wengi waliumia, wengine walipigwa risasi. Lakini tulijua tukirudi nyuma, Kenya inaweza kukosa kubadilika.”

Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu nchini Kenya (KNCHR) imesema kuwa maandamano ya mwaka 2024 yalisababisha angalau vifo 63, watu 610 kujeruhiwa na visa 74 vya watu kutoweka kwa lazima. Tume hiyo imeongeza kuwa watu 26 kati ya walioripotiwa kutoweka bado hawajapatikana.

Maisha ya ukimya

Lakini punde tu baada ya siku iliyotikisa taifa, Ezekiel Kyama alitoweka.

Aliizima ghafla sura yake ya umma, akakata mawasiliano na kuanza maisha ya kujificha.

Anasema hofu ilimtawala.

“Nilitupa simu yangu na laini yangu. Sikupenda mtu yeyote anifuatilie. Maisha yangu yalibadilika kabisa.”

Kwa miezi 23, yule kijana aliyekuwa ameketi kwenye kiti cha Spika wa Bunge katika picha zilizosambaa duniani kote, alitoweka bila kufahamika alikokuwa.

Lakini sasa, karibu miaka miwili baadaye, amerejea. Ameiambia BBC kuwa anaamini kuwa harakati za vijana zilizoanzia mitaani Juni 25 bado zinaishi.

“Muda ni sasa wa kubadilisha Kenya yetu. Historia itaandika kwamba vijana walisimama na walikuwa tayari kuongoza.”

Na anaporejea kwenye kumbukumbu ya dakika zile ndani ya Bunge, anasema hakuuona ukumbi ule kama jengo la mamlaka pekee.Aliuona kama ishara ya kile kinachowezekana.

“Sikuwa nimewahi kukanyaga bungeni. Lakini nilijiona siku moja kuna kijana anaweza kuwa Spika wa Bunge. Siku moja vijana wanaweza kuongoza taasisi hizi.”

Kwa Kyama, kuvamiwa kwa Bunge hakukuwa mwisho wa simulizi.

Kulikuwa mwanzo wa ndoto mpya, kwamba kizazi kilichojitokeza barabarani kudai kusikilizwa, siku moja kinaweza pia kupewa nafasi ya kuongoza taifa.

Nyumba iliyojaa kumbukumbu

g

Lakini kwa familia nyingi, Juni 25 si simulizi ya ushujaa.

Ni simulizi ya majonzi.

Katika eneo la Eastleigh jijini Nairobi Nchini Kenya, Edith Wanjiku bado anaishi na pengo kubwa lililoachwa na kifo cha mwanawe, Ibrahim Wanjiku, aliyekuwa na umri wa miaka 19.

Ibrahim ambaye alikuwa amemaliza kidato cha nne na kuamua kutafuta riziki kupitia uendeshaji bodaboda alivuta pumzi zake za mwisho karibu na majengo ya Bunge wakati wa maandamano hayo.

Tulimkuta Edith nyumbani kwake akiwa ameshika picha za mwanawe.

Kila picha aliyotuonyesha ilionekana kufufua kumbukumbu za kijana aliyemlea kwa miaka 19 na ambaye sasa amebaki katika picha na simulizi.

”Ibrahim alitoka nyumbani lakini hakuniambia anaenda kwa maandamano, nilimsubiri aje kupata chakula cha mchana sikumuona. Nilimtafuta kwa simu iliyopokelewa na mmoja wa rafiki yake”, ananieleza.

”Baada ya kumtafuta hospitali zote, nilimpta makafani ya City yaliyoko Nairobi akiwa mmoja ya miili iliyokuwa imerundikwa, ….anasita kidogo kwa huzuni kisha anaikumbatia picha yake.

”Nakumbuka vizuri, nilimuona akiwa amelala akiwa amevalia fulana ya rangi ya waridi lakini shingoni kulikuwa na alama ya risasi ambayo ndiyo iliyomuua kulingana na upasuaji wa maiti”, Edith anaendelea kunisumilia.

Mama wa muathiriwa wa maandamano ya Juni 2024 akiwa ameshikilia picha ya mtoto wake aliyeuawa

Machozi ya kimlengalenga, Edith anasema alimtegemea mwanawe kwa riziki kwa sasa hali ya maisha imekuwa ngumu zaidi asijue pa kugeukia.

”Mariam – ananiita jina Langu’- wajua nikikosa kibarua ya kufua nguo nalala njaa na mtoto wangu, msongo wa mawazo umenifanya nishinde nyumbani sifikirii kabisa na sina nguvu ya kuhangaikia tumbo langu, inauma sana”, Edith ananyamaza ghafla anavuta kamasi jepesi la uchungu.

Anasema karibu miaka miwili baadaye, safari ya kutafuta ukweli na haki bado haijafika mwisho.

”Tangu upasuaji wa maiti ya mwanangu na kugundua risasi ndio ilimuua Mamlaka ya IPOA haijanitafuta na hakuna kesi yoyote imeanza mahakamani, naskia uchungu kwasababu waliomuua mwanangu bado wako huru na wanaendelea kuua kila maandamano”, anaeleza.

Ni madai ambayo BBC Swahili hayajathibitisha kuhusu waliomuua Ibrahim Wanjiku.

Licha ya serikali kutangaza mpango wa kufidia waathiriwa wa ukiukaji wa haki za binadamu, Edith anasema bado hajawahi kuwasiliana na mamlaka kuhusu fidia.

”Nikimuona Rais Ruto nashangaa anasema nini kwasababu haki ya mwanangu bado haijasimama hata hiyo fidia sijapigiwa simu yoyote kuarifiwa nitapatiwa.”, anaendelea kunieleza huku akifunika mikono yake na leso ya njjano aliyokuwa amejitanda.

Serikali ya Kenya imeanza rasmi kutoa fidia kwa waathiriwa wa ukiukaji wa haki za binadamu, ikiwemo wale walioathiriwa katika maandamano ya umma yaliyofanyika kati ya mwaka 2013 na 2025. Jumla ya waathiriwa 348 ambao kesi zao zimethibitishwa watanufaika katika awamu ya kwanza ya mpango huo, ambapo serikali imetenga shilingi milioni 448.7 za Kenya kwa ajili ya fidia hiyo.

”Fidia si haki”

"Tafadhali polisi sisi ni wazazi. Hatuna nia mbaya. Sisi hatuna wahuni, ni wazazi peke yetu. Tunaomba muturuhusu tuweke maua tu alafu twende zetu," alisema mama wa mwathirika.

Chanzo cha picha, NMG

Mtetezi wa haki za binadamu Hussein Khalid anasema suala la fidia pekee halitoshi.

“Maandamano ya Juni 25 ni ya kuwakumbuka vijana waliokuwa wakipigania mabadiliko ya uongozi. Serikali iwajengee sanamu kama kumbukumbu yao na siku hii iwe siku ya mapumziko ya kitaifa. Fidia sio haki. Tunataka maafisa walioua waandamanaji wawajibishwe.”

Kwa upande wake, Marsden Kibet, mwakilishi wa vijana katika chama tawala cha UDA, anasema serikali haihusiki na madai ya watu kutoweka.

“Sijasikia kesi yoyote ya mtu kutoweka inayohusishwa na serikali hii.”

Lakini maswali kuhusu uwajibikaji bado yanaendelea.

Mamlaka Huru ya Kusimamia Utendaji wa Polisi, IPOA, imesema ni kesi tatu tu kati ya vifo 62 vilivyoripotiwa wakati wa maandamano ya Gen Z mwaka 2024 ambazo zimefikishwa mahakamani, huku nyingi zikiwa bado katika hatua za uchunguzi.

Maswali ambayo bado hayajajibiwa

Mama wa Mwathirika

Chanzo cha picha, NMG

Miaka miwili baadaye, majeraha bado yapo. Machozi ya baadhi ya familia bado hayajakauka.

Na maswali yaliyoulizwa na vijana wa Gen Z bado yanaendelea kutafuta majibu.

Je, haki ilitendeka?

Je, taifa lilijifunza chochote kutokana na vifo vya vijana hao?

Na je, sauti za wale waliotaka mabadiliko zitabaki kuwa kumbukumbu tu, au zitakuwa mwanzo wa sura mpya katika historia ya Kenya?

Uanaharakati wa vijana Afrika Mashariki

Maadhimisho ya Juni 25 yanakuja miaka miwili tangu maelfu ya Wakenya wengi wao vijana kulivunja Bunge wakati wa maandamano ya kupinga mapendekezo ya nyongeza ya ushuru, katika mojawapo ya changamoto kubwa kwa mamlaka ya serikali katika historia ya hivi majuzi nchini.

Chanzo cha picha, EPA

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, wakati wa mkutano wa hadhara, Mei 4 alitoa wito wa kuwepo kwa hatua za pamoja na Rais wa Kenya, William Ruto, ili kukabiliana na kile alichokieleza kuwa ni shughuli za vijana zinazovuruga utulivu katika ukanda huu.

“Piga mikwaju, wakija kwangu napiga mikwaju,” alisema, akisisitiza haja ya kuchukuliwa kwa hatua kali dhidi ya vijana wanaovuka mipaka ya nchi kushiriki katika maandamano na shughuli za uhamasishaji wa kiraia.

Katika hotuba yake, Rais Samia alisema serikali za ukanda huu hazipaswi kuwa na msimamo wa kulegeza kamba kwa watu aliowataja kuwa wasio na nidhamu, akiongeza kuwa hatua za pamoja na zenye uratibu ni muhimu ili kudumisha utulivu na utaratibu.

Akionekana kujibu matamshi haya, Ezekiel Kiama, mmoja wa vijana wa Gen Z Kenya amesema kuwa ”Vijana Afrika Mashariki hatutakubali kunyamazishwa na viongozi ambao hawana nia ya kuheshimu katiba na demokrasia, viongozi wa Afrika Mashariki wajue hilo”.

”Nitawaambia vijana kuwa tuna nguvu ya kubadilisha nchi zetu na kufufua ustawi usio na kikomo”, Ezekiel anaiambia BBC Swahili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *