Ashura; Shule ambayo iliunganika na damu tukufu na kupelekea watu waaminifu 72 kuuawa shahidi, na hivyo kuwa taa ya wongofu wa historia huku wakiwa wamechagua utukufu wa milele kwa ufahamu na mwamko kamili.

Mapambano ya Ashura ilikuwa hatua muhimu ya kihistoria katika kurejea Umma wa Kiislamu kwenye njia ya mafundisho aali ya Mtume Mtukufu wa Uislamu (saw). Katika zama ambazo bida’ na uzushi ulikuwa umechukua nafasi ya Sunna za Mtume, Nainawa ikawa kituo cha kusafisha na kutenganisha ukweli na batili. Katika uwanja huu, nafasi ya wafuasi wa Imam Hussein (as) ilikuwa zaidi ya wafuasi tu. Walikuwa “mashahidi wenye utambuzi” wa shule iliyodhihirisha uaminifu, maarifa na uvumilivu katika kiwango cha juu zaidi.

Uaminifu huko Karbala ulikuwa na maana ya kina zaidi kuliko kujitolea kimaadili. Uaminifu huu ulikuwa dhihirisho kuu la “ufuasi na kujitenga” ambalo lilitokana na utambuzi halisi na wa yakini wa wafuasi hao waaminifu kuhusu suala zima la nafasi ya kiongozi aliyeteuliwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuongoza umma wa Kiislamu. Walikichukulia kifo pembeni ya Imam wao kuwa sio mwisho, bali mwanzo wa maisha mema ya kudumu milele. Ufahamu huu ndio ulipelekea katika usiku ule wa kuamkia Ashura, pale Imam alipowaondolea kiapo cha utiifu kwake, hakuna hata mmoja kati yao alirejea nyuma na kukimbia uwanja wa vita, bali walisimama imara na kushikamana na agano lao. Utofauti wa umri wa wafuasi hao, kuanzia wazee kama Habib ibn Madhahir hadi vijana kama Ali Akbar na Qassim bin Hassan (as), ulithibitisha wazi kwamba njia ya kufikia kilele hiki cha uaminifu iko wazi kwa kila umri na matabaka ya kijamii, na kwamba sharti pekee la kufikia kilele hiki ni ukweli na ikhlasi.

Kipengele cha “ufahamu” pia kilikuwa na nafasi muhimu sana katika mapambano haya. Wafuasi hawa waaminifu hawakupoteza mwelekeo wa ukweli hata katika mazingira magumu zaidi ya kuenezwa shaka, hofu, vitisho na propaganda za Yazidi, bali walijua fika kwamba kusimama pembeni ya Imam Hussein (as) ni kusimama katika safu ya ukweli mutlaki, hata kama jambo hilo lingegharimu maisha yao. Ufahamu huu ulijikita katika malezi ya kidini na mafungamano ya dhati na Qur’ani Tukufu pamoja na kizazi kitoharifu cha Mtume Mtukufu (saw).

Uwanja wa Karbala ulikuwa dhihirisho la utekelezaji wa ahadi ambayo Mwenyezi Mungu aliichukua kutoka kwa wanadamu. Wafausi hawa 72 ni wawakilishi wa wanadamu wote walio huru ambao huitikia vyema wito wa “je, kuna yeyote miongoni mwenu atakeyenisaidia.” Katika mahesabu ya kimungu, idadi sio kigezo, bali ubora wa imani na kina cha uaminifu ndio huamua kila jambo. Kuuawa kwao shahidi, huku wakiwa wanatabasamu na kuonyesha shauku kubwa, kulithibitisha wazi ushindi wa utambuzi dhidi ya masuala ya kimaada. Kwao wao, Karbala hayakuwa mauaji ya umwagaji damu, bali safari ya kupaa kelekea kwa Mwenyezi Mungu. Kupewa wafuasi hao na Imam (as), nishani ya heshima ya “Wafuasi Safi na Waaminifu zaidi” ni ushahidi unaothibitisha ukweli huu.

Katika mtazamo wa kijamii, uaminifu wao ni somo kubwa kwa vizazi vya zama zote: Kwamba katika njia ya kupigania matukufu ya Mwenyezi Mungu, manufaa ya mtu binafsi hayana nafasi. Uaminifu huu ulipanda mbegu katika historia ambayo matunda yake yalionekana wazi katika mapambano ya baadaye ya umwagaji damu yaliyofanywa na harakati za mwamko na utambuzi. Ashura ni mgongano kati ya “mantiki ya Maisha” na “mantiki ya ufufuo,” ambapo kwa kuvuka mantiki ya maisha ya muda ya humu duniani, masahaba na wafuasi hawa walifanikiwa kuingia kwenye uwanja wa maisha ya mbinguni ya kudumu milele. Uaminifu huko Karbala ulifungamana na “subira,” na kuvumilia kiu na huzuni ya kuwapoteza wapendwa wao, jambo ambalo bila shaka lilihitajia uvumilivu na subira ya kiwango cha Imam Hussein (as). Uhusiano baina ya wafuasi na Imam ulikuwa wa upendo uliokita mizizi katika kumtambua Khalifa wa Mwenyezi Mungu, na mshikamano huu ukawafanya washindane katika kuuawa shahidi. Chaguo hili la ufahamu katika kilele cha mgogoro lilithibitisha kuwa uaminifu ni njia ya maisha.

Damu iliyomwagika huko Karbala ilidhamini kuendelea kuwepo kwa dini ya Uislamu, na lau isingekuwa kujitolea kwa wafuasi hawa waaminifu 72, ujumbe wa harakati na dini hii tukufu ungezikwa katika kaburi la historia. Maisha ya wafuasi hawa, kuanzia kwa Waislamu wapya hadi watumwa, yanaonyesha kwamba Karbala kilikuwa kiwanda cha kutengeneza watu, ambapo rangi na yaliyopita hayakuwa na muhimu tena, ambapo uaminifu uligeuza shaba ya uwepo wao kuwa dhahabu. Ashura, likiwa ni “tukio kubwa kupita kiasi”, huhamasisha kila mtu aliye huru kusimama imara mbele ya dhulma, na mtindo huu wa uaminifu unachukuliwa kuwa dawa ya kutibu changamoto za utambulisho wa mwanadamu wa sasa. Kwa kuvuka  sifa ya “Mimi” walimfikia “Yeye” na hivyo kudiri vyema maana ya kuzama kwenye upendo wa Mwenyezi Mungu na wakaiona Karbala kama lango la kuingia mbinguni, lango ambalo lilifanya hofu kutokuwa na maana.

Swala chini ya mvua ya mishale ni kielelezo halisi cha ucha-Mungu kinachoonyesha kuwa lengo kuu ni kumwabudu Mwenyezi Mungu. Uaminifu wao ulikuwa chaguo kubwa kati ya heshima ya milele na kujidhalilisha, na kupitia chaguo hilo, wakawa wameainisha nafasi yao ya heshima katika jamii ya mwanadamu.

Leo, kuhuishwa tena uaminifu huu ni muhimu ili kuandaa mazingira ya kudhihiri Imam wa Zama (AF), na Karbala inatufundisha kwamba uaminifu una gharama yake ambayo ni lazima ilipwe. Watu hawa 72 walikuwa kiini cha fadhila za mwanadamu, na historia hukaa kwenye meza ya maarifa yao kila mwaka inapowadia Muharram. Karbala ni mkondo katika kila wakati na mahali, ambapo sisi pia hukabiliwa na mtihani kama huo maishani. Uaminifu wao ni kielelezo chenye nguvu cha kupaa kutoka kwenye kupenda mali ya dunia hadi kilele cha hali ya kiroho na kujitayarisha kwa ajili ya medani kuu za mbinguni. Hii ndiyo maana halisi ya kudumu milele damu ya watukufu hawa ulimwenguni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *