
Leo ni Ijumaa tarehe 11 Muharram 1448 Hijria sawa na Juni 26, 2026.
Miaka 1387 iliyopita katika siku hii ya leo, tarehe 11 Muharram, 61 Hijria ilianza harakati ya mateka na familia ya Imam Hussein (AS) kuelekea Syria baada ya tukio la Ashura.
Mwishoni mwa siku ya 10 ya Muharram mwaka wa 61 Hijria na baada ya kuuawa shahidi Imam Hussein (AS) na masahaba wake waaminifu, askari wa Yazidi walianza kupora mali na vifaa vya watu wa msafara wa Imam Husseini.
Walichoma mahema ya Imam na hawakusita kupora mali ndogo zaidi. Hatimaye, msafara wa Imam Hussein (AS), wakati huu ukiongozwa na Imam Sajjad (AS) na Hazrat Zainab al Kubra (SA), ulianza kuelekea Kufa jioni ya tarehe 11 Muharram. ****
Miaka 190 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo, aliaga dunia Rouget de Lisle, malenga na mtunzi wa nyimbo za kimapinduzi wa Ufaransa. Rouget alihudumu pia jeshini na alikuwa akitunga mashairi ya kuwahamasisha wanamapinduzi wa Ufaransa na nyimbo za hamasa na za kusisimua. Rouget de Lisle alitunga wimbo wa kimapinduzi kwa jina “La Marseillaise” ambao baadaye ulikuwa wimbo rasmi wa taifa. **
Miaka 81 iliyopita sawa na tarehe 26 Juni 1945, mkutano wa kimataifa wa San Fransisco ulimaliza shughuli zake katika mji unaojulikana kwa jina hilo huko Marekani kwa kupasishwa hati ya Umoja wa Mataifa.
Mkutano huo ambao ulikuwa wa kwanza wa kimataifa kuwahi kufanyika baada ya Vita vya Pili vya Dunia, ulihudhuriwa na wawakilishi wa nchi 50 waitifaki katika vita hivyo. **
Siku kama ya leo miaka 66 iliyopita kisiwa cha Madagascar kilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Uingereza na Ufaransa zilianzisha ushindani wa kuidhibiti nchi hiyo ya Kiafrika katika karne ya 18. Mwishoni mwa karne ya 19 Ufaransa ilikidhibiti kikamilifu kisiwa cha Madagascar. Hata hivyo wananchi wa Madagascar waliendesha mapambano mengi ya ukombozi dhidi ya wakoloni wa Kifaransa, miongoni mwake ni yale ya mwaka 1947 ambapo karibu watu elfu 80 waliuawa. **
Tarehe 26 Juni kila mwaka huadhimishwa kama siku ya kimataifa ya kupinga matumizi ya dawa za kulevya na usafirishaji haramu wa dawa hizo.
Siku hii ilianishwa katika kikao kilichofanyika tarehe 26 Juni mwaka 1987 huko Vienna, Austria. Kikao hicho pia kilijadili hatua za kuchukuliwa kukabiliana na mihadarati ambayo sasa ni tatizo kubwa la dunia nzima.
***
Na tarehe 26 Juni miaka 29 iliyopita Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliitangaza kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kuwatetea Wahanga wa Mateso kwa lengo la kufuta kabisa vitendo hivyo viovu duniani.
Vitendo vya mateso vina historia ndefu duniani lakini ilitazamiwa kuwa maovu hayo yangehitimishwa kikamilifu katika zama hizi hususan baada ya kupasishwa nyaraka kadhaa zinazohusiana na haki za binadamu.
Hata hivyo bado kuna nchi zinazotumia mateso kuwakandamiza wapinzani. Marekani ambayo inajinadi kuwa mtetezi mkubwa wa haki za binadamu ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kutesa wapinzani kote duniani. Vilevile utawala wa Kizayuni wa Israel unaosaidiwa na kuungwa mkono na nchi za Magharibi hususan Marekani umekuwa ukiwatesa na kuwanyanyasa raia wa Palestina katika korokoro na jela zake za kutisha.