Kiongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen, Abdul-Malik al-Houthi, ameapa kwamba atashambulia uwepo wowote wa Israel katika eneo lililojitenga na Somalia la Somaliland kwa njia zote zinazowezekana, akisisitiza kwamba Yemen “haitakaa kimya mbele ya uwepo wowote wa Israel huko Somaliland, na haitawasubiri waoga.”

Sayyid Abdul-Malik al-Houthi amesema: “Tunafuatilia na kuchunguza kwa karibu hali ya Somaliland, na kile adui anachojaribu kufanya kwa kuigeuza kuwa uwanja wa kudhibiti Ghuba ya Aden, Lango Bahari la Bab al-Mandab na Bahari Nyekundu.”

Al-Houthi ameuhimiza Umma wa Kiislamu na nchi zinazopakana na Bahari Nyekundu “kuchukua msimamo wa pamoja ili kumzuia adui kufikia malengo yake,” akisisitiza kwamba Yemen “itachukua hatua wakati wowote adui atakapoingia katika eneo hilo kwa kutumia nyenzo zote zinazopatikana.”

Kiongozi wa harakati ya Ansarullah pia ametoa wito kwa serikali ya Mogadishu “kurekebisha hali ya Somalia, kuwajali wananchi na kuwaunga mkono katika kukabiliana na adui, Israel.”

Israel ilitangaza kuitambua rasmi Somaliland kama dola huru mnamo Desemba 2025, hatua ambayo Somalia iliipinga na kuilaani vikali, ikiitaja kuwa ni “shambulio la makusudi dhidi ya mamlaka na uhuru wa Somalia.”

Aidha nchi za Afrika, Kiarabu na Kiislamu duniani zimepinga vikali hatua ya utawala wa Israel kuanzisha uhusiano na eneo la Somaliland ambalo ni sehemu ya Somalia.

Mvutano kati mataifa ya Kiislamu na utawala haramu wa Israel uliongezeka baada ya eneo hilo la Somaliland kufungua rasmi ubalozi mjini Al Quds (Jerusalem), kufuatia uamuzi wa Israel kuitambua Somaliland kama dola huru.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *