BAADA ya kushiriki katika mchakato wa kujenga upya mfumo wa maendeleo ya soka la vijana Yanga, Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu hiyo, Paul Mathews amerejea nchini kwao Afrika Kusini, ambako ameteuliwa kuwa mkurugenzi wa michezo wa Marumo Gallants.
Mathews alitambulishwa kuwa mkurugenzi wa ufundi wa Yanga Julai 29, 2025 na akiwa katika nafasi hiyo alisimamia pia maendeleo ya soka la vijana pamoja na kuanzishwa kwa mradi wa Yanga Soccer School Novemba 2025.
Katika kipindi chake cha utumishi, Mathews alijikita zaidi katika maendeleo ya soka la vijana kwa kuweka mfumo wa kutambua vipaji, kuwaendeleza na kuwajenga wachezaji wa baadaye wa Yanga.
Moja ya maeneo yaliyoonekana kupata msukumo mpya chini ya uongozi wake ni mradi wa soka la vijana, ambao kwa muda mrefu ulikuwa ukihitaji maboresho na mwelekeo wa kimkakati ili kuimarisha maendeleo ya vipaji ndani ya klabu.
Taarifa za ndani ya Yanga zinaeleza mchango wake haukuishia katika majukumu ya kawaida ya kiufundi pekee, bali ulijikita pia katika kuweka msingi wa muda mrefu wa maendeleo ya wachezaji wa klabu hiyo.
“Mathews alikuwa sehemu muhimu ya kuamsha tena mfumo wa vijana. Aliamini klabu kubwa haiwezi kuendelea kutegemea usajili pekee, bali lazima ijenge kizazi chake cha wachezaji,” zilidai taarifa hizo.
Kupitia ushirikiano wake na viongozi wa Yanga, klabu ilianza kuweka mkazo zaidi katika utambuzi wa vipaji, ufuatiliaji wa maendeleo ya vijana na ujenzi wa mfumo wa kuwapa nafasi ya kupanda hatua kwa hatua kuelekea timu ya wakubwa.
Chanzo hicho kilieleza mradi huo umeendelea kutokana na msingi wa muda mrefu uliowekwa, badala ya kulenga matokeo ya haraka.
“Alifanya kazi kwa karibu na viongozi kuhakikisha mradi wa vijana unarejea na kuendelea kukua. Hata kama ameondoka, kuna mambo muhimu ambayo tayari yamewekwa na yanaendelea kufanya kazi.”
Kuondoka kwa Mathews kunafungua ukurasa mpya katika maisha yake ya soka, ambapo sasa atakuwa na jukumu la kusimamia masuala ya michezo ndani ya Marumo Gallants, huku Yanga ikitarajiwa kuendeleza dira iliyoanza kujengwa katika maendeleo ya soka la vijana.