
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amefanya mfululizo wa mazungumzo kwa njia ya simu na mawaziri wa kutoka Pakistan, Misri, Falme za Kiarabu (UAE), Uingereza, na Romania, ambapo walijadili makubaliano ya Islamabad pamoja na maendeleo ya karibuni katika ukanda.
Katika mazungumzo yake ya Ijumaa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Mohammad Ishaq Dar, Araqchi alitoa shukrani kwa ukarimu wa Pakistan wakati wa ziara ya hivi karibuni ya Rais Masoud Pezeshkian mjini Islamabad, na akaeleza matumaini kuwa makubaliano yaliyofikiwa katika ziara hiyo yatafuatiliwa kwa uzito na kutekelezwa katika ngazi mbalimbali.
Araqchi pia alizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdelatty, kuhusu matukio ya kikanda pamoja na hali ya karibuni ya michakato ya kidiplomasia inayoendelea kati ya Iran na Marekani, kwa lengo la kudumisha amani na uthabiti katika Asia Magharibi.
Katika mazungumzo tofauti na Waziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Sheikh Abdullah bin Zayed Al Nahyan, pande hizo mbili zilibadilishana maoni kuhusu maendeleo ya kikanda kwa kuzingatia uelewano uliopatikana kati ya Iran na Marekani.
Waziri huyo wa UAE amesisitiza umuhimu wa kuendelea kwa mazungumzo na njia za kidiplomasia, akieleza matumaini kuwa mchakato wa sasa wa kidiplomasia utazaa matokeo yenye kujenga kwa ajili ya amani, usalama na uthabiti wa kikanda.
Araqchi pia alifanya mazungumzo ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Yvette Cooper, na kumweleza kuhusu duru za karibuni za mazungumzo, yanayojiri katika utekelezaji wa makubaliano, pamoja na mashauriano yanayoendelea.
Aidha wamejadili matukio ya kikanda, na kusisitiza kuendelea kwa mashauriano ya kidiplomasia ili kuimarisha uthabiti wa kikanda, kusukuma mbele mchakato wa mazungumzo, na kufikia matokeo chanya na ya kudumu.
Katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Romania, Ana Tuyo, Araqchi amefafanua kuhusu utekelezaji wa hati ya makubaliano ya maelewano (MoU) pamoja na mtazamo wa Iran kuhusu suala hilo.
Waziri wa Romania amekaribisha juhudi zinazoendelea za kidiplomasia za kupunguza mvutano katika Asia Magharibi, na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza mchakato huo pamoja na kutekeleza ahadi za pande husika.
Pande zote mbili pia zimesisitiza haja ya kuendelea na mashauriano na kukuza ushirikiano wa pande mbili katika kipindi kijacho.
Rais wa Iran Masoud Pezeshkian na Rais wa Marekani Donald Trump walitia saini rasmi hati ya makubaliano ya maelewano ya Islamabad yenye vipengele 14 tarehe 18 Juni, baada ya maandishi yake kukamilishwa na makubaliano hayo kuanza kutumika rasmi, kufuatia miezi kadhaa ya mazungumzo mazito yaliyopatanishwa na Pakistan kwa uungwaji mkono wa nchi nyingine za ukanda.
Kwa mujibu wa MoU hiyo, pande hizo mbili zimeingia katika kipindi cha mazungumzo cha siku 60, kwa lengo la kufikia makubaliano ya mwisho yaliyo kamili.
MoU hiyo inataka kusitishwa kabisa kwa uhasama katika medani zote, ikiwemo Lebanon, kuondolewa kwa hatua kwa hatua kwa vikwazo vya Marekani, kuondolewa kwa mzingiro wa majini dhidi ya Iran, na kurejeshwa kwa usafiri wa kibiashara kupitia Mlango wa Hormuz ndani ya siku 30.