Iran imekemea mashambulizi ya hivi karibuni ya anga ya Marekani dhidi ya maeneo kadhaa kando ya pwani za kusini mwa nchi, ikiyataja kuwa “ukiukaji wa wazi” wa hati ya makubaliano ya maelewano (MoU) iliyopatanishwa na Pakistan.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema katika taarifa iliyotolewa Jumamosi kwamba: “Mashambulizi ya anga ya jeshi la kigaidi la Marekani dhidi ya vituo vya ufuatiliaji wa pwani vya Iran ni ukiukaji wa wazi wa Kifungu cha 2(4) cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa na pia ni uvunjaji wa wazi wa Kifungu cha 1 cha MoU ya kusitisha mapigano,”

Wizara hiyo pia imesema kuwa “utawala wa ghasibu wa Kizayuni ambao pia ni utawala wa kibaguzi, kwa uratibu na Marekani, kwa wakati mmoja uliishambulia Lebanon,” jambo ambalo pia ni ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa: “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran italinda mamlaka yake ya kitaifa, usalama wake na maslahi yake ya kitaifa kwa nguvu zake zote kwa mujibu wa Kifungu cha 51 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa.”

Wizara hiyo imeongeza kuwa Jeshi la Iran limetekeleza mashambulizi ya kujihami dhidi ya malengo yanayohusishwa na majeshi vamizi ya Marekani kujibu mashambulizi hayo.

Taarifa hiyo pia imezitaka nchi zote zilizoko katika mwambao wa kusini wa Ghuba ya Uajemi kuheshimu kanuni ya ujirani mwema na kuepuka kuruhusu ardhi au miundombinu yao kutumiwa na pande vamizi kufanya mashambulizi dhidi ya Iran.

Aidha, Wizara ya Mambo ya Nje iliutaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Baraza la Usalama, na taasisi nyingine za kimataifa “kutobaki kimya mbele ya ukiukaji wa wazi wa Marekani dhidi ya misingi ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa,” na kutekeleza wajibu wao wa kisheria na kimaadili katika kulinda amani na usalama wa kikanda na wa kimataifa.

Katika taarifa iliyotolewa Ijumaa usiku, Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) ilisema kuwa ilifanya mashambulizi dhidi ya kile ilichodai kuwa maghala ya makombora na ndege zisizo na rubani pamoja na vituo vya rada vya pwani vya Iran, ikidai kuwa hatua hiyo ilikuwa jibu kwa shambulio la Jeshi la Iran dhidi ya chombo cha majini kilichokuwa kinapita katika Mlango wa Hormuz.

Masaa machache baadaye, Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) lilifanya mashambulizi ya kulipiza kisasi, likilenga malengo ya kijeshi ya Marekani katika ukanda huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *