
Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamejulishwa kuwa kuongezeka kwa mapigano, kuzorota kwa hali ya kibinadamu na mlipuko mpya wa Ebola kunazidi kuongeza mateso kwa wananchi wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC) licha ya juhudi za kikanda za kuleta amani kuendelea kupata mafanikio.
Taarifa hizo zimetolewa na James Swan, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, aliyoitoa mbele ya Baraza hilo lililokutana Ijumaa mchana kwenye mjadala wa wazi kujadili hali inayoendelea kwenye taifa hilo la Maziwa Makuu barani Afrika.
Swan ambaye pia ni Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani DRC, amesema “Wananchi wa mashariki mwa nchi wanaendelea kukabiliwa na moja ya migogoro mikubwa zaidi ya kibinadamu barani Afrika, huku mapigano kati ya makundi yenye silaha yakiongezeka, maelfu wakilazimika kuyahama makazi yao, na mlipuko mpya wa ugonjwa wa Ebola ukitishia matumaini ya kufikiwa kwa amani ya kudumu.”
Ikiwa ni hotuba yake ya kwanza tangu achajuliwe na Katibu Mkuu kushika wadhifa huo, Swan ameweka bayana kuwa hali ya usalama Mashariki mwa nchi hiyo bado ni “ngumu, tete na yenye madhara makubwa kwa wananchi,” licha ya hatua muhimu zilizopigwa katika juhudi za kidiplomasia ndani ya mwaka mmoja uliopita. Aidhaamezitaka pande zote zinazohusika kuheshimu kikamilifu makubaliano ya amani na kuendelea na juhudi za kumaliza mzozo kwa njia ya mazungumzo.
Wakati juhudi za kidiplomasia zikiendelea, mapigano bado ni makali katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, ambako waasi wa AFC/M23, wanaodaiwa kuungwa mkono na Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF), wanaendelea kupambana na Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (FARDC) pamoja na makundi washirika wake.
Mapigano ya hivi karibuni yamejikita katika eneo la Rubaya, ambalo ni kitovu muhimu cha uchimbaji madini pamoja na Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini, pamoja na nyanda za juu za Minembwe huko Kivu Kusini.
Matumizi ya ndege zisizo na rubani za kivita, mizinga na silaha nzito yameongeza kwa kiasi kikubwa hatari kwa raia na kusababisha uharibifu wa miundombinu muhimu.