
Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameviagiza vyombo vinavyohusika na mapambano ya dawa za kulevya kubuni mbinu mpya kuendana na mabadiliko ya zile wanazotumia wahalifu wa vitendo hivyo.
Amesema, pamoja na mafanikio yaliyopatikana ya kupambana na dawa hizo, bado kuna changamoto za mabadiliko ya mara kwa mara ya mbinu zinazotumiwa na wahalifu ikiwemo utengenezaji wa dawa mpya za kulevya zenye muundo sawa dawa za asili.
Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Juni 27, 2026 kupitia hotuba yake iliyosomwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah katika kilele cha kupiga vita matumizi ya biashara haramu ya dawa za kulevya Zanzibar.
“Naviagiza vyombo vinavyohusika na mapambano haya kuimarisha ushirikiano, uwajibikaji, weledi kujua mbinu za wahalifu hao na kuhakikisha sheria zinatekelezwa ipasavyo,” amesema.
Amesema wahalifu wa dawa za kulevya wamekuwa wakitumia matumizi ya teknolojia katika biashara hiyo haramu pamoja na kuongezeka ushawishi kwa vijana kupitia mitandao ya kijamii.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, mapambano dhidi ya dawa za kulevya hayawezi kufanikiwa kwa kutumia nguvu za kisheria pekee bila kuwekeza kikamalifu katika elimu, malezi na uhamasishaji kwa vijana kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
“Nazikumbusha familia ambazo ndio msingi wa kwanza wa kinga dhidi ya dawa za kulevya, kuongeza juhudi za kuwekeza kwenye maadili, elimu na mawasilino mazuri ndani ya familia zetu kwani tusipofanya hayo tutakuwa tumeacha pengo linaloweza kutumiwa vibaya na wahalifu wanaosambaza dawa za kulevya,” alisema.
Aidha alisema, serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukabiliana na uhalifu wa dawa za kulevya imekua ikichukua hatua mbalimbali ikiwemo kuanzishwa kwa mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya.
Ametaja miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo ni pamoja na kusambaratisha mitandao ya wahalifu wakubwa wa dawa hizo.
Kwa mwaka 2025/26 kwa mujibu wa Dk Mwinyi jumla ya mitandao minne inayojihusisha na usafirishaji wa heroini, mirungi pamoja na kuchanganya dawa hizo katika vyakula mbalimbali Zanzibar na mataifa mengine duniani imegundulika na kusambaratishwa.
Vile vile, serikali imeimarisha huduma za tiba na marekebisho ya tabia kwa kujenga kituo cha kutoa huduma hizo kwa waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya huko Kidimni Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja ambapo jumla ya waathirika 769 wamesajiliwa kupatiwa huduma.
Kaimu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais, Hamza Hassan Juma amesema biashara ya dawa za kulevya inamilikiwa na watu matajiri na inafanyika kwa njia ya mifumo hivyo ameiomba serikali kuwapatia vifaa ili kupambana na wahalifu kupitia njia ya mifumo.
Amesema upo umuhimu kwa wananchi wote kupitia masheha na viongozi wa ngazi mbalimbali kuunganisha nguvu za pamoja katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya Zanzibar.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya Zanzibar, Kanali Burhani Zubeiri Nassoro amesema wamefanikiwa kusambaratisha mitandao mikubwa minne inayojihusha na usafirshaji na usambazaji wa dawa za kulevya.
Amesema, ushirikiano uliopo baina ya Mamlaka ya kupambana na dawa za kuevya ya Zanzibar na Tanzania bara umefanikisha kupungua kwa wahalifu wa dawa za kulevya.
“Tunaendelea na ushirikiano huo ili kuhakikisha kunakuwa na taifa lenye vijana imara kwani taifa lisilokuwa na vijana imara taifa hilo litakuwa limekufa,” amesema.
Ujumbe wa mwaka huu katika maadhimisho ya siku kilele cha kupiga vita matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya inasema ushahidi uko wazi, wekeza katika kinga.