
Bwana Yesu asifiwe, karibu tena siku nyingine ya baraka kwetu sote, ninaitwa Mwalimu Erasto Maliganya. Karibu kwenye tafakari ya Neno la Mungu lililohai kwenye maisha yetu.
Maisha ya mwanadamu yamejawa na vipindi vya misimu tofauti tofauti, na kuna wakati unaweza kukaa chini na kuanza kulinganisha misimu ya maisha yako, hasa vipindi ambavyo pengine ulivifurahia zaidi. Pia kuna misimu inakuja katika maisha ambayo, kama ungeulizwa mapema, usingekubali kukutana na kipindi kama hicho maishani mwako.
Nyakati kama hizi ni kama wakati ambapo pengine kile ambacho ulikuwa ukikingoja kinachelewa au kinaonekana kutotimia kwa wakati uliotarajia.
Mstari wa msingi: 1 Wafalme 19:4
“Lakini yeye mwenyewe akaendelea katika jangwa mwendo wa siku moja, akaenda akaketi chini ya mretemu. Akajiombea roho yake afe, akasema, ‘Yatosha; sasa, Ee Bwana, uiondoe roho yangu; kwa kuwa mimi si mwema kuliko baba zangu.’”
Ni kweli, katika maisha kuna nyakati unachoka. Unafika mahali ambapo hata yale maono yaliyokuwa yanakupa hamasa yanaanza kuonekana kama mzigo. Unajikuta hutaki tena kusikia chochote kuhusu kile ulichokuwa ukikifuatilia kwa moyo wako wote. Kama umefika katika hatua hiyo, fahamu kwamba hauko peke yako.
Hata Eliya, nabii mkuu wa Mungu, aliwahi kufika mahali pa kuchoka na kukata tamaa. Baada ya ushindi mkubwa alioupata, alijikuta amevunjika moyo na akaona hana nguvu za kuendelea. Lakini Mungu hakumwacha; alimtia nguvu, akamfariji, na akamwinua tena.
Unapofika katika nyakati kama hizo, usikate tamaa wala usiache safari. Mweleze Mungu kwa unyenyekevu:
“Baba, hapa nilipofika nimechoka. Nitie nguvu, kwa sababu bila Wewe siwezi kuendelea.”
Mara nyingi katika hatua hiyo huhitaji mpango mpya wala nguvu zako binafsi; unachohitaji ni mguso wa Mungu na neno moja kutoka Kwake litakalohuisha moyo wako.
Kumbuka, uchovu wa leo siyo ishara kwamba maono yako yamekufa. Inaweza kuwa ni ishara kwamba unahitaji kurudi mbele za Mungu ili upokee nguvu mpya za kuvuka ulipo na kwenda hatua inayofuata. Mungu bado yupo pamoja nawe, na atakutia nguvu mpaka ufike mahali alipokupangia kufika.
Mungu hakuahidi maisha yasiyo na mito wala moto. Hakuahidi kwamba safari yetu itakuwa bila majaribu, machozi au nyakati za maumivu. Lakini alitoa ahadi iliyo kubwa kuliko kuondolewa kwa changamoto zote, na ahadi hiyo ni uwepo Wake.
Mito inaweza kuwakilisha matatizo yanayotishia kutuzamisha, na moto unaweza kuwakilisha majaribu yanayojaribu kuteketeza imani yetu kwa Mungu. Hata hivyo, nguvu ya ahadi ya Mungu haipo katika kutokuwepo kwa dhoruba, bali katika uwepo Wake katikati ya dhoruba hizo.
Unapopita katika maji mengi, Yeye yuko pamoja nawe. Unapokabiliana na moto mkubwa unaoletwa na majaribu, Yeye hasimami mbali akikuchungulia; anatembea nawe ndani yake.
Unakumbuka habari ya Meshaki, Shadraki na Abednego? Mungu aliungana nao kwenye moto. Kile wengine wanachoona kuwa mwisho wako, Mungu anaweza kukigeuza kuwa ushuhuda wako.
Kwa hiyo, usipime uwepo wa Mungu kwa ukubwa wa changamoto unazokutana nazo. Badala yake, kumbuka kwamba hakuna kina cha maji kinachoweza kuzidi mkono Wake kukuokoa, wala hakuna moto mkali unaoweza kuzima kusudi Lake juu ya maisha yako.
“Mungu hakuahidi maisha yasiyo na mito wala moto; aliahidi kwamba katika yote hayo Atakuwa pamoja nawe.”
Isaya 43:2
“Upitapo katika maji mengi, nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea, wala mwali wa moto hautakuunguza.”
Mungu hakusema kwamba mahali pagumu tunakaa; alisema tunapita.
Unaweza kuchoka kwenye kituo cha daladala kwa kusubiri daladala. Lakini ukikumbuka kwamba hukai hapo, bali una mahali unapoenda, inakupa moyo kwamba hapo si mwisho wa safari yako; unapita tu.
Usiyaache maono yako kwa sababu ya uchovu wa leo. Hapo ni mahali unapopita tu. Unahitaji kushinda uchovu huo na kusema, “Hali hii ni ya muda tu, si ya kudumu.”
Amani ya kweli siyo kutokuwa na dhoruba, bali kuwa na Kristo katikati ya dhoruba.
Watu wengi hudhani amani ni maisha yasiyo na matatizo, machozi au changamoto. Lakini ukweli ni kwamba hakuna maisha yasiyo na dhoruba. Kila mtu hukutana na nyakati za maumivu, hasara, kukatishwa tamaa na majaribu yanayoonekana kuzidi uwezo wake.
Amani ya kweli haiji kwa sababu hali zimekuwa nzuri; huja kwa sababu tunajua ni nani yuko pamoja nasi katikati ya hali hizo. Dhoruba inaweza kuendelea kuvuma, mawimbi yanaweza kuendelea kupanda, lakini uwepo wa Kristo huleta utulivu ambao mazingira hayawezi kuutoa wala kuuchukua.
Wakati wanafunzi walipokuwa ndani ya mashua na dhoruba kali ikainuka, hofu yao haikutokana na ukubwa wa mawimbi pekee, bali walikuwa wamesahau kwamba Yesu alikuwa pamoja nao. Uwepo Wake ndani ya mashua ulikuwa mkubwa kuliko nguvu ya dhoruba iliyokuwa nje ya mashua.
Ndivyo ilivyo katika maisha yetu. Kuna nyakati ambazo hatuelewi kile tunachopitia, lakini tunaweza kuwa na amani kwa sababu Kristo yuko pamoja nasi.
Fuatisha sala hii
“Bwana Yesu, ninasema asante, kwa maana hata hapa ninapopita Wewe, Bwana, unafahamu. Naomba, Bwana, unipe nguvu zako niweze kushinda kila aina ya uchovu ndani yangu. Naomba unitie nguvu niweze kusonga mbele na kuyakabili yale ambayo niliona sina nguvu ya kuyakabili. Naomba unipe Roho wako anitie nguvu niweze kushinda yale ambayo nisingeweza kushinda peke yangu. Nisaidie kuyafikia maono yangu. Amina.”
Mungu akubariki sana na akutie nguvu uweze kushinda kila aina ya uchovu ndani yako.
Mwalimu Erasto Maliganya anapatikana Kanisa la KKKT Forest, Mbeya. Kwa maombi, ushauri wasiliana name 0755371354.