Mkuu wa Majeshi ya Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba ametoa amri ya kufungwa televisheni ya NTV na vyombo vingine vya habari.

 

Mkuu huyo wa majeshi ya Uganda amesema kuwa kituo cha televisheni cha NTV Uganda na gazeti la Daily Monitor havitafunguliwa tena bila kibali chake.

Kupitia ujumbe aliouchapisha katika mtandao wa X, Muhoozi alisema kuwa vyombo hivyo viwili vya habari vitafungwa kuanzia leo.

Katika ujumbe mwingine, alisema haamini katika uhuru wa vyombo vya habari nchini Uganda na kwamba vyombo vya habari vinapaswa kuongozwa kwa kuzingatia misingi ya mapinduzi.

”Kuanzia sasa vyombo vyote vya habari vya Uganda vitafuata sheria”, ameandika Muhoozi.

Kufikia alfajiri ya Jumapili, watazamaji wa NTV Uganda na Spark TV walikumbana na skrini tupu zenye ujumbe ulioonyesha kuwa matangazo ya vituo hivyo hayapatikani.

Shughuli za gazeti la Daily Monitor pamoja na vituo vya redio vya KFM na Dembe FM ziliathiriwa na operesheni hiyo.

Hadi wakati wa kuchapishwa kwa taarifa hii, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda, Jeshi la Polisi la Uganda na Tume ya Mawasiliano ya Uganda havikuwa vimetoa taarifa rasmi kueleza sababu za operesheni hiyo au msingi wa kisheria wa kufungwa vyombo hivyo vya habari.

‘Bado hatujaelezwa kufungwa kwa vyombo vya habari Uganda kutaendelea hadi lini’, Daily Monitor ilichapisha kauli hiyo katika mtandao wa X.

Tukio hilo limezua upya hofu kuhusu uhuru wa vyombo vya habari nchini Uganda, ambako taasisi huru za habari zimewahi kukumbwa na shinikizo na vikwazo vya serikali katika utekelezaji wa majukumu yao.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *