Ethiopia itakuwa mwenyeji mkutano wa kimkakati kwa ajili ya kujadili mwelekeo mpya wa diplomasia ya umma Afrika

 

Taarifa zinasema, watu zaidi ya 600, wakiwemo viongozi wa kimataifa, wanadiplomasia, watunga sera, wabunifu, wafanyabiashara, wasomi na wawakilishi wa mashirika ya kiraia kutoka Afrika na sehemu nyingine za dunia, wanatarajiwa kukutana jijini Addis Ababa, Ethiopia, tarehe 29 na 30 Julai kwa ajili ya mkutano wa World Public Summit Africa.

Mkutano huo wa kimataifa unalenga kuimarisha diplomasia ya umma na kuongeza mchango wa Afrika katika kuunda mustakabali wa dunia.

Rais wa Ethiopia, Taye Atske Selassie anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano huo wenye kauli mbiu “Dunia mpya: Afrika itavyobadili mwelekeo wa siku zijazo” ambao unakuja wakati ambapo mataifa ya Afrika yanazidi kutafuta nafasi kubwa zaidi katika maamuzi ya kimataifa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jukwaa la World Peoples Assembly, mfumo wa awali wa kidiplomasia unaozingatia serikali kwa serikali pekee haukidhi tena mahitaji ya dunia ya sasa badala yake, wanasisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wananchi, asasi za kiraia, taasisi za elimu, sekta binafsi na wadau wa utamaduni katika kujenga mahusiano ya kimataifa.

“Mkutano huu unaakisi mtazamo mpya wa ushirikiano wa kimataifa unaoweka mbele ushirikiano kati ya watu, kuheshimiana na malengo ya pamoja ya maendeleo,” inaeleza taarifa ya waandalizi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *