
Caracas, Venezuela. Idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na matetemeko mawili makubwa ya ardhi yaliyoikumba Venezuela imeongezeka na kufikia 1,430 huku juhudi za kuwaokoa manusura zikiendelea wakati muda muhimu wa saa 72 wa kuwapata wakiwa hai ukikaribia kuisha.
Kwa mujibu wa kiongozi mwandamizi wa Bunge la Venezuela, Jorge Rodríguez, watu wengine 3,238 wamejeruhiwa na zaidi ya familia 3,100 zimehamishwa kutoka makazi yao na kuwekwa kwenye vituo vya muda.
Ameiambia BBC janga hilo ni kubwa kuwahi kulikumba taifa hilo katika kipindi cha zaidi ya miaka 120.
Eneo la Guaira ndilo lililoathirika zaidi baada ya matetemeko hayo yenye ukubwa wa kipimo cha 7.2 na 7.5 kutokea ndani ya muda usiozidi dakika moja, huku majengo mengi yakiporomoka na maelfu ya watu kufukiwa chini ya vifusi.
Vikosi vya uokoaji kutoka Venezuela na mataifa mbalimbali vinaendelea kuchimba vifusi kutafuta manusura. Hata hivyo, wataalamu wa uokoaji wanasema uwezekano wa kuwapata watu wakiwa hai hupungua kadiri muda unavyosonga.
Mtoto mchanga aokolewa akiwa hai
Licha ya hali hiyo, bado matumaini hayajazimika baada ya mtoto mchanga kuokolewa akiwa hai kutoka chini ya kifusi, tukio lililowapa faraja waokoaji na familia zilizopoteza ndugu zao.
Wakazi wengi wa maeneo yaliyoathirika wameendelea kushiriki katika uokoaji kwa kutumia mikono yao kutokana na uhaba wa vifaa vya kisasa, huku baadhi yao wakiilaumu serikali kwa kuchelewa na kutoratibu vizuri operesheni za dharura.
Katika Hospitali ya Vargas mjini Caracas, mamia ya majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu huku familia zikiweka picha za ndugu zao waliopotea kwenye kuta za hospitali wakitumaini kutambuliwa miongoni mwa manusura.
Serikali imeeleza zaidi ya watu 30,000 wakiwemo wanajeshi, polisi, wahudumu wa afya, wanasaikolojia na waokoaji wanashiriki katika operesheni hiyo, huku zaidi ya timu 20 za kimataifa zikitumwa kusaidia juhudi za uokoaji.
Hata hivyo, Wataalamu wa Shirika la Jiolojia la Marekani (USGS) wameonya kuwa idadi halisi ya vifo inaweza kuongezeka kadiri operesheni za utafutaji zinavyoendelea, kutokana na ukubwa wa tetemeko hilo na kiwango kikubwa cha uharibifu wa majengo.
Huku matumaini yakizidi kufifia, familia nyingi bado zinaendelea kusubiri taarifa za wapendwa wao, zikiviomba vikosi vya uokoaji visiache kutafuta manusura hadi pale watakapopatikana wote.