Watu 11 wamefariki dunia baada ya ndege ndogo waliyokuwa wakisafiria kuanguka muda mfupi baada ya kuruka katika mji wa Tomblaine, kaskazini mashariki mwa Ufaransa.

Kwa mujibu wa Reuters, mamlaka za eneo hilo zimeeleza tukio hilo limetokea leo Jumapili, Juni 28, 2026 na kusababisha kifo cha rubani pamoja na wengine 10 waliokuwa katika ndege hiyo iliyokuwa ikitumika kwa ajili ya mafunzo.

Taarifa zinaeleza ndege hiyo ilikuwa imewabeba wanafunzi watano waliokuwa wakijifunza kuruka kwa parachuti pamoja na wakufunzi watano.

Mkuu wa jimbo hilo, Yves Seguy amesema ndege hiyo ilianguka moja kwa moja kuelekea ardhini karibu na kituo cha biashara pamoja na makazi huku mabaki yake yakitapakaa kwenye njia maalumu ya waendesha baiskeli.

“Ajali hii ingeweza kusababisha vifo vya watu wengine kama ndege ingeanguka umbali wa mita chache kutoka ilipoangukia,” amesema Seguy.

Sababu ya ajali bado haijafahamika, japokuwa siku moja kabla ya ajali, jiji la Nancy lililo karibu na Tomblaine lilirekodi kiwango cha juu zaidi cha joto kuwahi kushuhudiwa.

Hata hivyo, mamlaka ya jimbo hilo zinaendelea na uchunguzi wa kubaini chanzo cha ajali hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *