Dar es Salaam. Agizo la Serikali la kuwataka wamiliki wa hoteli na nyumba za kulala wageni kusajili wageni wote kwa kutumia kitambulisho cha Taifa, limewaibua wataalamu wa sheria na wale wa sekta ya malazi, wakisema ni ngumu kutekeleza.

Ugumu wake unatokana na kile wanachoeleza, si Watanzania wote wanamiliki vitambulisho vya Taifa, wengi wana namba za utambulisho pekee, wengine wamejisajili na hawajapata na baadhi hawakujisajili kabisa.

Katika takriban watu milioni 68 wanaokadiriwa kuwepo nchini, chini ya nusu wameshasajiliwa na kutambuliwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida). Watu hao ni milioni 27.18 kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani.

Ukiacha ugumu, utekelezwaji wa agizo hilo unatajwa kuwa na upande wa faida na hatari. Faida, itarahisisha kupata taarifa za mgeni iwapo atapatwa au kufanya tukio lolote litakalohitaji kujulikana kwake.

Kwa upande wa hatari, wataalamu wa sheria, wanaona kuwasilisha kitambulisho hicho ni kuweka wazi taarifa binafsi, ambazo wakati mwingine zinaweza kutumika vibaya dhidi ya aliyeziwasilisha.

Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2022 (Sura ya 44), kifungu cha 14(1), inaeleza mtu haruhusiwi kukusanya au kuchakata taarifa binafsi bila kusajiliwa kama mkusanyaji au mchakataji wa taarifa chini ya sheria hiyo.

Agizo lenyewe

Akijibu swali bungeni jijini Dodoma Juni 26, 2026 kuhusu hali ya usalama nchini, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi alisema wamiliki wa hoteli na nyumba za kulala wageni wanapaswa kuhakikisha wageni wote wanaowapokea wanasajiliwa kwa kutumia Kitambulisho cha Taifa.

“Wamiliki wa hoteli zote, airbnb, guest house na lodge nchini, waanze kusajili kila anayeingia ndani kwa kutumia vitambulisho vya Nida. Wageni wote wanaoingia kwenye majiji wajisajili. Tutakapoenda kwenye hoteli yako, tukakuta kuna watu wasioeleweka, tutachukua hatua dhidi ya mmiliki pamoja na mhudumu,” alisema.

Alifafanua hatua hiyo inalenga kusaidia vyombo vya ulinzi na usalama kuwabaini watu wanaotumia maeneo ya malazi kujificha au kufanya shughuli zinazohatarisha usalama wa nchi.

Hatari kwa taarifa binafsi

Wakili Edson Kilatu amesema hakuna sheria inayowapa wamiliki wa hoteli mamlaka ya kudai na kuhifadhi taarifa za Kitambulisho cha Taifa cha kila mteja bila utaratibu maalumu wa kisheria.

“Unapomchukua mtu taarifa zake binafsi lazima kuwe na uhakika wa namna zitakavyolindwa. Bila mfumo huo, kuna hatari ya taarifa hizo kutumika vibaya au kuingia mikononi mwa wasiostahili,” amesema.

Sio wote wana Nida

Kwa mujibu wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mwaka wa fedha 2026/27 iliyowasilishwa bungeni Juni mwaka huu, watu 27,186,421 walikuwa wamesajiliwa na kutambuliwa na Nida.

Pia, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ilitangaza wananchi 37,647,235 walijiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa Uchaguzi Mkuu wa 2025, huku Ofisi ya Taifa ya Takwimu ikikadiria idadi ya Watanzania mwaka 2026 itafikia milioni 70.04.

Mwanaharakati wa Haki za Binadamu, Anitha Kamizi amesema agizo hilo pia linaweza kuwanyima huduma baadhi ya Watanzania ambao bado hawajapata vitambulisho vya Taifa.

“Sasa sio wote wana vitambulisho vya Taifa. Pia, kuna dharura unapatwa na jambo linalohitaji ukalale nyumba ya wageni wakati huo hauna kitambulisho. Hii sio sawa,” amesema.

Mtaalamu wa sheria, Ibrahim Bendera amesema tamko hilo haliendani na uhalisia wa mazingira ya sasa kwa kuwa bado kuna idadi kubwa ya wananchi wasio na vitambulisho vya Nida.

“Iwapo Serikali ilitaka kutumia utaratibu huo, ilipaswa kwanza kuhakikisha kila Mtanzania anapata utambulisho wake. Huwezi kumzuia mtu kupata huduma ya malazi kwa sababu hana kitambulisho ambacho bado hakijamfikia,” amesema.

Wamiliki wa hoteli, gesti

Msimamizi wa nyumba ya kulala wageni mkoani Iringa, Mussa Yassin amesema kutegemea Nida pekee kutaleta changamoto kwa kuwa si kila mteja anakimiliki.

Amesema badala yake Serikali iruhusu matumizi ya vitambulisho vingine rasmi vyenye picha za mhusika ili kurahisisha utambuzi.

Christina Gabriel, mmiliki wa nyumba ya kulala wageni mkoani Arusha, amesema hata yeye bado hajapata kitambulisho licha ya kuwa na namba ya Nida.

“Kama mimi mwenyewe sina kitambulisho, je, ni wangapi wako katika hali kama yangu? Tukiwataka wateja wote walete Nida tutawapoteza wengi,” amesema.

Mmiliki mwingine wa nyumba ya kulala wageni aliyeomba kutotajwa jina, amesema agizo hilo linaweza kuathiri biashara, hasa maeneo ya vijijini ambako wananchi wengi bado hawana vitambulisho vya Taifa.

Wakati hao wakisema hayo, kifungu cha 18 cha Sheria ya Hoteli, Sura ya 105, kinasema, “kila mmiliki au msimamizi wa hoteli anatakiwa kuweka daftari katika hoteli yake ambalo litakuwa na jina na anuani ya kila mgeni anayelala hotelini na taarifa nyingine zitakazokuwa zimeelekezwa kisheria.”

Maoni tofauti

Katika mitandao ya kijamii, Lucas Mwashambwa ameandika utekelezaji wa agizo hilo unaongeza usumbufu kwa wananchi wanaosafiri kwa shughuli za biashara au dharura.

Amedai baadhi ya watu watakwama kufika maeneo wanayokwenda kwa kukosa sehemu ya kulala na hivyo kujikuta kwenye mazingira yanayoweza kuhatarisha usalama wao.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Hifadhi, Hoteli, Majumbani, Huduma za Jamii na Ushauri (Chodawu), Said Wamba ameunga mkono hatua ya Serikali akisema usalama wa Taifa unapaswa kupewa kipaumbele.

“Kama vyombo vya dola vinaona kuna changamoto za kiusalama, ni muhimu kila mdau kushiriki kuzidhibiti. Usalama ukivurugika, athari zake zitafika hata kwenye biashara za hoteli,”amesema.

Si jambo geni

Kwa upande wake mmiliki wa hoteli, Kennedy Edward amesema ukusanyaji wa taarifa za wageni si jambo jipya kwani ni utaratibu ulioanza kufanyika muda mrefu na husaidia Serikali kupata takwimu za wageni wa ndani na wa nje.

“Hili sio jambo jipya, mteja kutoa vitambulisho vyake au pasi ya kusafiria ni kawaida hasa kwenye hoteli. Ni muhimu na nzuri na imekuwa ikifanyika ni vile baadhi wameacha ndio maana kumeibuka mazoea tofauti,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *