ILIPOISHIA

James akamuuliza yule mkuu wa kituo cha yatima.

Mkuu wa kituo hicho alimtazama na kumuuliza:

“Kwani wewe ni nani?”

“Mimi ndiye niliyechukuliwa na Mchungaji Antony James Hiza kutoka katika kituo hiki.”

“Unasema kweli?”

“Kweli kabisa.”

Mkuu wa kituo hicho cha yatima alishangaa.

“Umekuwa mkubwa sasa. Ulikuwa wapi?” alimuuliza James.

“Niko hapa hapa Tanga. Nimeajiriwa na mzee Wakwetu.”

Aliposema hivyo, James alielekeza mkono wake kwa Wakwetu.

“Kumbe kijana ni mfanyakazi wako?” mkuu wa kituo cha yatima akamuuliza Wakwetu.

“Ni mfanyakazi wangu, lakini wakati namuajiri sikujua kama alitoka katika kituo hiki. Alinieleza leo.”

“Vizuri sana. Sasa yule mchungaji aliyekuchukua kwa sasa yuko wapi?” mkuu wa kituo cha yatima akamuuliza James.

SASA ENDELEA…

“YILE alikufa tangu mwaka juzi, hivi sasa najitegemea mwenyewe”

“Vizuri sana. Leo tuna bahati kubwa. Pacha mwenzako pia alifika hapa kuitafuta familia yake. Ameonana na mzee”

Masumbuko akashituka.

“Yuko wapi. Nataka nimuone?”

“Alikuwa na mzee”

“Utamuona. Tukitoka hapa nitakupeleka mahali alipo” Wakwetu akamwambia.

“Kwa kweli nitafurahi sana”

“Mwenzako alikuwa Zambia” Wakwetu aliendelea kumwambia.

“Mmeachana mkiwa watoto, mnakutana mkiwa wakubwa. Ni jambo zuri sana” Mkuu wa kituo cha yatima alimwambia James.

Wakwetu hakutaka kusema lililokuwa moyoni mwake. Alikuwa akisubiri uchunguzi wake ukamilike.

Baada ya mazungumzo ya muda mfupi Wakwetu na James walimuaga mkuu wa kituo hicho cha yatima na kuondoka. Wakwetu alikuwa bado yuko kwenye lindi la mawazo. Alikuwa akimdodosa dodosa tu James.

“Huyo mchungaji aliyekuwa amekuchukua alikuwa akiishi wapi?”

“Tulikuwa tunakaa Usagara lilipo kanisa lake” James alimjibu.

“Umesema yeye ndiye aliyekupa jina hilo la James, kabla ya hapo ulikuwa unaitwa nani?”

“Sikumbuki, aliponichukua nilikuwa mdogo. Alinianzisha yeye darasa la kwanza. Ninachokumbuka ni kuwa nilipokuwa na fahamu zangu alinibatiza na kunipa jina hilo la James. Jina hilo ni la baba yake. Yeye anaitwa Anthony James Hiza”

“Na ulisoma hadi kiwango gani?”

“Niliishia darasa la kumi na mbili.  Yule mzee alipokufa nikaamua kutafuta kazi”

Walipofika katika ile hoteli ambayo Masumbuko alipangishiwa chumba, walibisha katika chumba alichokuwamo Masumbuko. Masumbuko aliyekuwa amejilaza kitandani akitafakari aliinuka na kwenda kufungua mlango.

“Karibuni ndani” aliwambia.

Wakwetu na James waliingia ndani.

“Nimekuletea pacha mwenzako” Wakwetu alimwambia Masumbuko mara tu walipoketi.

Masumbuko akamtumbulia macho James, uso wake ukiwa na mshangao na alama ya kuuliza.

Wakwetu akamgeukia James.

“James kutana na pacha mwenzako mliopotena tangu utoto”. Akamwambia James.

Nyuso za James na Masumbuko zilikunjuka kwa furaha. Katika kutazamana miili iliwasisimka. Kila mmoja aliwania kumfuata mwenzake wakakumbatiana kwa furaha ya ajabu.

Wakwetu aliona macho ya wote wawili yakitoka machozi. Yalikuwa machozi ya furaha ya kukutana tena baada ya kupotezana kwa miaka mingi.

Walipoachiana, kila mmoja alijifuta machozi wakapeana mikono. Kila mmoja alikuwa akimuita mwenzake kaka.

“Kaka habari za siku nyingi?” alianza Masumbuko.

“Nzuri kaka. Ulikuwa wapi?”

“Niko hapa hapa Tanga, wewe je”

“Mimi nilikuwa Zambia”

“Ulifikaje huko?” James akamuuliza Masumbuko.

“Kuna mzungu aliyekuja kunichukua kwa nia ya kunilea. Alikuwa akiishi hapa Tanga halafu alihamia Zambia. Niliishi naye kule tangu nikiwa mtoto hadi mwaka jana alipokufa. Mwaka huu nikaamua kuja Tanzania kuitafuta familia yangu” Masumbuko alimjibu.

“Na mimi nilichukuliwa na Mchungaji Anthony James Hiza. Alinifanya kama mwanawe. Na yeye alikufa kama miaka mitatu iliyopita, nikaja kupata kazi ya udereva kwa mzee”

“Namshukuru sana mzee kwa kutukutanisha tena tukiwa wakubwa, vinginevyo ningehangaika sana. Nilipigwa risasi juzi juzi nikiwa gesti. Nimeponea tundu ya sindano kufa”

“Oh! Kumbe wewe ndiye uliyekuwa umelazwa kule hospitali?”

“Uliwahi kuja kuniuona?’

“Niliwahi kufika na mzee”

“Sikukumbuki tena kaka. Lakini hukuwa ukinitambua?’

“Hapana, sikukutambua. Isingekuwa rahisi kukutambua bila kutambulishwa”

“Ni kweli. Mimi nimeshakusahau”

“Ulikuwa taabani sana. Huwezi kuwa na kumbukumbu. Sasa kwanini ulipigwa risasi”

“Kwa kweli sijajua sababu. Kuna kijana mmoja alikuja na bastola chumbani akaniuliza wewe ndiye Masumbuko nilipomjibu ndiye mimi akanipiga risasi kisha akakimbia”

James akamtazama Wakwetu.

“Ndiyo ile kesi niliyosingiziwa mimi” akamwambia.

“Ulisingiziwa wewe?” Masumbuko akamuuliza.

“Ndiyo, polisi walinkamata mimi wakadai ndiye niliyekupiga risasi”

“Hapana, hukuwa wewe”

“Kama unakumbuka kuna mpelelezi mmoja wa kesi yako tulikutana naye pale hospitali, alikuuliza kama mimi ndiye huyo kijana aliyekupiga risasi. Ukaniangalia kisha ukasema siye mimi”

“Nakumbuka…nakumbuka…kumbe ulikuwa wewe?”

“Ndiyo, nilikuwa ni mimi. Niliwekwa ndani kwa karibu siku tatu bila kujua kuwa nawekwa ndani kwa ajili ya ndugu yangu”

Wakwetu hakutaka waendelee na mazungumzo yale, akawakatisha.

“Kwa vile mmeshakutana na kujuana, Masumbuko tutakuacha kwanza. Tutarudi saa mbili usiku tule chakula pamoja hapa hoteli au siyo?” akawauliza.

“Sawa tu” Masumbuko alisema.

“Sasa James twende kwanza”

James aliagana na Masumbuko kwa furaha kabla ya kuondoka na Wakwetu.

“Twende wapi?” James alimuuliza Wakwetu wakiwa kwenye gari.

“Twende unakoishi wewe, nikuache halafu nitakupitia tena mnamo saa moja na nusu usiku”

“Sawa mzee wangu”

Wakaenda anakoishi James. James akashuka kwenye gari. Alionekana wazi kuwa alikuwa na furaha. Wakwetu alisogea kwenye sukani akaondoka na gari.

Alirudi nyumbani kwake. Wakati James na Masumbuko walikuwa na furaha ya kukutana, Wakwetu alikuwa amepatwa na fadhaa. Uso wake ulikuwa umejikunja na alijiona yuko njia panda bila kujua elekee upande upi. Maswali mengi yasiyokuwa na majibu ya kuridhisha yalikuwa yamekitawala kichwa chake.

Alipofika nyumbani kwake alimkuta mke wake akiwa na Majaliwa. Walikuwa wameketi sebuleni wakizungumza. Dakika chache kabla ya Wakwetu kufika nyumbani Sharifa alikuwa amemueleza Majaliwa kuwa amemuona mume wake ana uso wa fadhaa.

“Sijui amepata habari gani?” akamwambia.

“Kwani hofu yako ni nini mama?” Majaliwa alimuuliza.

“Isije kuwa amesikia habari yoyote”

“Sidhani lakini jaribu kumdadisidadisi, anaweza kukueleza alilonalo”

“Mh…namuogopa!”

Ndipo waliposikia gari linasimama nje.

“Huyo anakuja” Sharifa akamwambia Majaliwa.

Wakabadili mazungumzo.

Wakwetu alipoingia aliwasalimia.

“Hamjambo?”

“Hatujambo” walimjibu kwa pamoja na Majaliwa akamwamkia.

“Shikamoo baba”

“Marahaba”

Wakati akimuitikia alikuwa akielekea chumbani kwake. Alifungua mlango akaingia ndani. Sharifa na Majaliwa waliwasha televisheni wakawa wanaangalia.

Saa moja na nusu usiku, Wakwetu alisimamisha gari mbele ya nyumba aliyokuwa akiishi James. James alikuwa amesimama barazani mwa nyumba hiyo akimsubiri tajiri yake.

Gari liliposimama James alikwenda kwenye mlango aliokuwa Wakwetu akijijua yeye ni dereva. Siti yake alikuwa ameikalia Wakwetu.

“Zunguka mlango wa pili ujipakie” Wakwetu alimwambia.

James akazunguka mlango wa upande wa pili wa gari hilo akaufungua na kujipakia. Wakwetu akaliondoa gari.

Hawakuzungumza chochote hadi walipofika kwenye ile hoteli aliyokuwepo Masumbuko. Waliingia kwenye sehemu ya mkahawa wa hoteli, Wakwetu akamwambia James aende akamuite Masumbuko.

Wakwetu alipanda ghorofani kilikokuwa chumba cha Masumbuko. Akabisha mlango. Masumbuko akafungua mlango.

“Tumeshafika” James alimwambia Masumbuko.

“Mzee yuko wapi?”

“Yuko mkahawani, amenituma nikufuate”

“Haya twende” Masumbuko akafunga mlango wakashuka ngazi na kuingia mgahawani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *