Spika wa Bunge la Lebanon, Nabih Berri, amekosoa vikali makubaliano yaliyosainiwa Washington kati ya Lebanon na utawala wa Israel, akiyataja kuwa ni seti ya maagizo ya kutwishwa badala ya kuwa makubaliano yanayolinda haki za nchi hiyo ya Kiarabu.

Katika maelezo yake kwa gazeti la Al Akhbar, Berri amesema makubaliano hayo “ni ya kutishwa, si makubaliano yanayolinda haki za Lebanon,” akionya kwamba matokeo yake yatakuwa mabaya sana.

Nabih Berri amesema kuwa makubaliano hayo ni “mabaya mara kumi zaidi” kuliko Mkataba wa Mei 17 wa 1983, ambao ulipingwa sana nchini Lebanon na baadaye kufutwa.

Ameonya kwamba kipengele chake hatari zaidi ni uwezo wake wa kuchochea migawanyiko ya ndani na mizozo ya kidini, jambo ambalo hatimaye linahudumia maslahi ya utawala vamizi wa Israel.

“Mkataba huu ni uchochezi wa uasi unaotishia umoja wa Lebanon na watu wa Lebanon,” amesema Nabih Berri akiongeza kwamba kuuelezea kama “uchochezi wa uasi” kunawakilisha “kiwango cha juu zaidi cha onyo la kisiasa.”

Matamshi hayo ya Spika wa Bunge la Lebanon yametolewa baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, kutangaza Ijumaa iliyopita kwamba makubaliano ya mfumo yamefikiwa kati ya Lebanon na Israel.

Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imepinga vikali makubaliano hayo, ikisema mpango huo unahalalisha uvamizi wa Israel kusini mwa Lebanon.

“Makubaliano haya ni batili na hayana maana, na badala yake vifungu vya Mkataba wa Maelewamo wa Iran na Marekani lazima vitekelezwe,” amesema Katibu Mkuu wa Hizbullah Sheikh Naeim Qassem katika taarifa iliyotolewa Jumamosi.

Hassan Fadlallah, mbunge mwandamizi wa Hizbullah pia amepinga vikali mfumo huo wa makubaliano unaosimamiwa na Marekani, akiutaja kama “aibu,” “fedheha,” na kusualimu amri mamlaka ya Lebanon.

Harakati ya Amal ya Lebanon pia imepinga kile kinachoitwa makubaliano baina ya serikali ya Beirut na utawala wa Kizayuni, ikisema kwamba vifungu vingi vya makubaliano hayo vina madhara kwa maslahi ya kitaifa ya Lebanon na vinahudumia maslahi ya utawala wa Israel.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *