Pande zinazopigana nchini Mali zinahusika na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa na shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW).

Taarifa hiyo imsema: Makundi ya waasi, vikosi vya Jeshi la Mali na mamluki wa kigeni wanaoungwa mkono na Serikali, wote wamefanya unyanyasaji mkubwa dhidi ya raia tangu mapigano yalipoongezeka nchini humo mwezi Aprili.

HRW imesema, tarehe 25 Aprili, waasi wenye uhusiano na al Qaeda waliokuwa na nia ya kupindua utawala wa kijeshi waliungana na wapiganaji wa Tuareg wa harakati ya Azawad Liberation Front, ambapo walimuua Waziri wa Ulinzi wa Mali, Sadio Camara na kuteka mji wa kaskazini wa Kidal.

Jeshi la Serikali ya Mali na wapiganaji wa Urusi wa Kikosi cha Afrika walijibu hujuma hiyo kwa kulipiza kisasi dhidi ya jamii za Fulani na mashambulizi mawili ya anga yaliyopelekea kuwaua raia.

Wapiganaji wa kundi la JNIM waliuzingira mji mkuu wa nchi hiyo, Bamako. Mwezi Mei, waasi hao walichoma moto zaidi ya magari 40 ya raia wakijaribu kuingia mjini humo na kumuua hadharani mwanamume mmoja huko Tonka, karibu na Timbuktu.

Mtafiti mkuu wa HRW katika eneo la Sahel anasema:”Upuuzaji wa muda mrefu wa hali ya Mali unaendelea kuchochea vitendo vya unyanyasaji dhidi ya raia,” na ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kuunga mkono uchunguzi huru kuhusu unyanyasaji huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *