Dar es Salaam. Ongezeko la joto kali barani Ulaya limehusishwa na vifo zaidi ya 13,000 katika kipindi cha wiki moja tangu Juni 21, huku mamilioni wakikabiliwa na viwango vya juu vya joto vinavyovunja rekodi na kusababisha msongamano mkubwa kwenye huduma za afya.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) joto kali limeendelea barani Ulaya, likihusishwa na vifo zaidi ya 1,300 vilivyothibitishwa katika nchi kadhaa, huku wataalamu wakionya kuwa idadi halisi inaweza kuwa kubwa zaidi kutokana na vifo visivyoorodheshwa moja kwa moja kuwa vinavyotokana na joto.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema wimbi hili la joto linaonyesha udhaifu mkubwa wa mifumo ya miji ya Ulaya, akibainisha kuwa nyumba, shule na maeneo ya kazi hayakujengwa kuhimili hali hiyo.

“Mamilioni ya watu sasa wanaishi chini ya hali hatarishi, huku wazee na wagonjwa wa muda mrefu wakiwa kwenye hatari kubwa zaidi,” amesema.

Wakati huohuo, Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) limeeleza kuwa Ulaya ndilo bara linaloongezeka joto kwa kasi zaidi duniani ikiwa ni mara mbili ya wastani wa dunia.

WMO imesisitiza kuwa mawimbi ya joto sasa yamekuwa ya mara kwa mara, marefu na yenye nguvu zaidi kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kushuhudiwa duniani.

Taarifa za mamlaka za afya nchini Ufaransa zinaonyesha takriban vifo 1,000 vilivyoripotiwa ndani ya siku chache za kilele cha joto hilo, huku nchi nyingine kama Ujerumani, Poland, Jamhuri ya Czech, Uingereza, Ubelgiji na Uswisi zimekumbwa na joto la kati ya nyuzi joto 35 hadi 41.7, viwango vilivyovunja rekodi katika historia ya mataifa hayo.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Ujerumani (DWD) imetahadharisha juu ya kuendelea kupanda kwa joto, huku vituo vya uokoaji vikieleza kushindwa kumudu ongezeko la wagonjwa wanaofikishwa hospitalini kutokana na matatizo ya moyo, upungufu wa maji mwilini na kuzimia.

Katika taarifa zake, Tume ya Ulaya (European Commission) imesema nchi wanachama lazima ziharakishe mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo kubadili miundombinu ya miji ikiwamo kuongeza miti, vivuli, vyanzo vya maji na maeneo ya hifadhi ya joto.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron ameitaja hali hiyo kama mgogoro wa afya ya umma unaohitaji hatua za haraka, akiiagiza serikali yake kupanua vituo vya baridi (cooling centers), kuongeza maji ya bure kwa wananchi na kulinda makundi hatarishi hasa wazee.

Nchini Uingereza, Wakala wa Usalama wa Afya wa Uingereza (UKHSA) umetoa tahadhari ya viwango vya juu vya hatari, ikieleza joto linaweza kusababisha vifo vinavyoweza kuzuilika ikiwa tahadhari hazitazingatiwa.

Mamlaka hiyo imehimiza wananchi kunywa maji mara kwa mara, kuepuka jua kali na kuwasaidia wazee.

Nchini Italia, serikali ya Waziri Mkuu, Giorgia Meloni imeweka hatua za dharura za afya ya umma, ikiwemo kusimamisha kazi za nje wakati wa mchana na kuimarisha huduma za uangalizi wa wazee majumbani.

Wataalamu wa afya wameeleza kuwa chanzo kikuu cha hali hiyo ni mchanganyiko wa joto la kawaida la msimu wa kiangazi Ulaya na ongezeko la gesi chafuzi, ambalo limeongeza kasi na ukubwa wa mawimbi ya joto.

Pia wamesema mifumo ya umeme, hospitali na miundombinu ya miji inazidiwa kutokana na ongezeko la matumizi ya vifaa vya kupooza kama viyoyozi na feni.

Kwa mujibu wa ripoti za pamoja za wataalamu wa hali ya hewa barani humo, watu karibu milioni 200 wamekumbwa na joto kati ya nyuzi joto 35 hadi 40, huku baadhi ya maeneo yakifikia zaidi ya nyuzi joto 41, jambo lililosababisha kufungwa kwa shule, kusimama kwa baadhi ya shughuli za uchumi na ongezeko la ajali na vifo vya ghafla.

Wataalamu wa WHO wamesisitiza kuwa bila mabadiliko makubwa ya sera za miji na mazingira, Ulaya itaendelea kukumbwa na mawimbi ya joto yanayozidi kuwa hatari zaidi kila mwaka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *