
Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa ameitaka jamii ya kimataifa kuacha kauli za kulaani pekee na badala yake kuchukua hatua za kivitendo ili kusitisha mpango wa Israel wa kupora ardhi za Palestina.
Riyad Mansour ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Jumatatu kuwa Israel imeongeza kasi ya juhudi zake za kuunganisha ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, huku ikiimarisha pia uvamizi wake wa kijeshi katika Ukanda wa Gaza uliowekwa chini ya mzingiro na vilevile katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
Alionya kuwa utawala huo ghasibu “umeamua kuimarisha na kukita mizizi kwa uvamizi wake badala ya kuumaliza,” akisisitiza kuwa umechukua udhibiti kinyume cha sheria wa takribani asilimia 70 ya Ukanda wa Gaza na kwa vitendo umepora zaidi ya asilimia 60 ya Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, ikiwemo al-Quds (Jerusalem) Mashariki.
Kwa mujibu wa Mansour, hatua hizi si tu kwamba ni kinyume cha sheria za kimataifa, bali pia zinakiuka “mpango” pamoja na Azimio nambari 2803 la Rais wa Marekani Donald Trump, ambavyo vyote vinakataa uvamizi na kuunganisha ardhi kwa nguvu.
Aidha alionya kuwa sera za utawala wa Tel Aviv zinalenga kuzuia haki ya watu wa Palestina ya kujitawala na kuanzisha dola lao huru.
Akizungumzia upanuzi wa makazi haramu ya walowezi wa Kizayuni, Mansour alionya kuwa mpango wa kupanua makazi katika eneo nyeti la kimkakati la E1 utakuwa sawa na “hukumu ya kifo kwa dola ya Palestina na kwa matumaini ya amani katika kanda yetu.”
Mradi wa E1 karibu na al-Quds unachukua takribani kilomita za mraba 12, ukiwa na mipango ya kujenga karibu vitongoji 3,400 vya makazi ya walowezi haramu katika Ukingo wa Magharibi.
Mansour amesisitiza kuwa licha ya upinzani mpana wa kimataifa, mchakato wa kuunganisha ardhi unaofanywa na Israel unaendelea “kwa kasi zaidi kuliko wakati wowote uliopita na kwa uwazi zaidi kuliko hapo awali,” huku Israel ikiendelea kupuuza matamko na maazimio ya kimataifa.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, upanuzi wa makazi ya walowezi wa Israel katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu umefikia kiwango cha juu zaidi tangu angalau mwaka 2017.
Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, makazi yote ya walowezi wa Israel katika ardhi za Palestina zilizo chini ya uvamizi ni haramu bila shaka yoyote. Mkataba wa Nne wa Geneva unakataza wazi mamlaka ya uvamizi kuhamisha raia wake na kuwapeleka kuishi katika ardhi iliyo chini ya uvamizi, kanuni ambayo Israel imeendelea kuipuuza bila kuwajibishwa.
Umoja wa Mataifa umesisitiza mara kwa mara kuwa upanuzi wa makazi ya walowezi wa utawala wa Israel ni kikwazo kikubwa kwa amani.