Dar es Salaam. Kuanzia leo, Jumatano, Julai Mosi, 2026, wanaoanzisha biashara mpya watanufaika na msamaha wa kodi ya mapato kwa mwaka mmoja, hatua inayotarajiwa kuongeza ajira na kupunguza vikwazo kwa wajasiriamali wanaoingia sokoni.

Pamoja na ahueni hiyo, kwa Watanzania wanaopanga kuagiza magari yaliyotumika kutoka nje ya nchi, watalazimika kufunga mkanda kwa kuongeza bajeti zao baada ya Serikali kuongeza ushuru wa asilimia 18.

Vivyo hivyo, kwa wale wanaopenda urembo, hasa wanawake, wasishangae bei utakayokutana nayo au kutozwa ikawa zaidi ya ile uliyotozwa Juni 30 au kabla ya Julai.

Matarajio ya mabadiliko hayo yanatokana na kuanza kwa utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2026/27, iliyopendekeza msamaha wa kodi kwa biashara mpya na nyongeza ya asilimia 10 ya ushuru kwenye mashine za kukaushia kucha.

Bajeti hiyo ya Sh62.3 trilioni, iliyowasilishwa Juni 11, 2026 na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, ilipitishwa Juni 23 na Bunge kwa asilimia 97.7, baada ya wabunge 385 kati ya 393 waliokuwapo bungeni kuunga mkono mapendekezo hayo.

Katika bajeti hiyo, ambayo utekelezaji wake unaanza leo, Julai mosi, Serikali pia imeahidi kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha, kuongeza kasi ya ulipaji wa madeni yake na kubana matumizi.

Pia, utekelezaji wa bajeti hiyo utahusisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, iliyojikita katika kuimarisha kilimo na kuboresha mazingira ya biashara, kukuza pato la Taifa, kuimarisha matumizi ya takwimu katika kupima maendeleo na kuweka mfumo madhubuti wa ufuatiliaji wa utekelezaji wa mipango.

Jana, Ikulu, Dar es Salaam, katika Siku ya Gawio, Rais Samia Suluhu Hassan alisema: “Utekelezaji wa Dira 2050 unahitaji taasisi zenye uwezo wa kuingia kwenye ushindani wa soko. Tunapoanza kesho (leo) utekelezaji wa dira, tunatakiwa kuwa makini kwelikweli, taasisi zetu ziwe imara kwelikweli.”

Rais Samia amesema zinahitajika taasisi zinazotumia teknolojia, zinazopunguza upotevu wa mali, zinazovutia mitaji na kufungua fursa kwa sekta binafsi. Kwa taasisi zinazosuasua, amesisitiza zitafutiwe tiba ili kwenda nazo sambamba katika utekelezaji wa dira hiyo.

Kuanzia leo, Jumatano, Watanzania watashuhudia mabadiliko makubwa, yakiwemo ongezeko la ushuru wa bidhaa (excise duty) kwa magari yaliyotumika yanayoagizwa kutoka nje ya nchi.

Baada ya marekebisho yaliyofanywa na Bunge, magari yenye umri wa kati ya miaka minane na 10 yatatozwa ushuru wa asilimia 18, badala ya asilimia 20 iliyokuwa imependekezwa awali katika Muswada wa Sheria ya Fedha.

Kwa magari yenye umri wa kati ya miaka 10 na 20, ushuru utaendelea kuwa asilimia 35, huku yale yenye zaidi ya miaka 20 yakitozwa asilimia 40.

Aidha, magari yenye ukubwa wa injini usiozidi cc 1,000, ambayo awali hayakuwa yakitozwa ushuru huo, sasa yatatozwa ushuru wa asilimia tano.

Wadau wa sekta ya magari wanaeleza kuwa hatua hiyo huenda ikasababisha kupanda kwa bei za magari yaliyotumika, kwani waagizaji watalazimika kuhamishia sehemu ya gharama hizo kwa wanunuzi.

Wafanyabiashara, wananchi wasema…

Mfanyabiashara wa magari eneo la Kinondoni, Emmanuel Mkonyi, amesema licha ya kuongezeka kwa huduma za ununuzi wa magari kwa mkopo, wanunuzi bado watahitaji fedha nyingi zaidi ili kumiliki magari yanayoagizwa kutoka nje.

“Kodi za uagizaji bila shaka zitaongezeka, lakini mifumo ya ufadhili wa ununuzi wa magari itawasaidia baadhi ya wateja. Kwa baadhi ya utaratibu, mteja hulipa asilimia 50 ya gharama za gari na kampuni ya ufadhili hulipa kiasi kilichobaki, ambacho hulipwa kwa awamu,” amesema.

Mkonyi amesema ongezeko hilo la kodi haliwezi kuepukika ikiwa Serikali inataka kupata fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo.

“Wanunuzi watalazimika kuongeza bajeti zao kwa sababu Serikali inahitaji mapato zaidi ili kutekeleza ajenda yake ya maendeleo,” amesema.

Mkazi wa Mbezi Luis, Shukuru Mabala, amesema ameathiriwa na mabadiliko hayo baada ya kulazimika kuahirisha mpango wake wa kuagiza gari aina ya Toyota Harrier.

“Nilikuwa nimepanga kununua gari hilo Septemba, lakini sasa itanibidi nisubiri hadi Oktoba kwa sababu nahitaji fedha zaidi ya nilizokuwa nimezipanga,” amesema.

Mbali na magari, sekta ya urembo nayo inatarajiwa kuathiriwa na sheria hiyo mpya. Ushuru wa bidhaa kwa bidhaa za urembo zinazoagizwa kutoka nje, zinazotambuliwa chini ya makundi ya forodha 33.03, 33.04, 33.05 na 33.07, umeongezwa kutoka asilimia 10 hadi asilimia 15.

Vilevile, mashine za kukaushia rangi za kucha (nail polish drying machines) zinazoagizwa kutoka nje sasa zitatozwa ushuru wa bidhaa wa asilimia 10.

Akiwasilisha Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2026 bungeni, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, alisema ongezeko hilo la kodi linalenga kuongeza mapato ya Serikali, kuoanisha mfumo wa kodi wa Tanzania na baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), na kupunguza athari za kiafya zinazoweza kusababishwa na baadhi ya bidhaa za vipodozi.

Wataalamu wa urembo

Mtaalamu wa urembo wa kucha, eneo la Mwenge, Davis Katunzi, amesema ongezeko la kodi kwa vifaa vinavyoagizwa kutoka nje linaweza kuwalazimu watoa huduma kuongeza gharama kwa wateja.

“Kodi zikiongezeka, nasi tutalazimika kutafuta namna ya kukabiliana nazo kwa sababu vifaa tunavyotumia vitakuwa ghali zaidi.

“Biashara ya urembo wa kucha imekuwa chanzo muhimu cha ajira kwa vijana wengi. Mimi hupata wastani wa Sh50,000 kwa siku kutokana na kazi hii, fedha zinazoniwezesha kuhudumia familia yangu,” amesema.

Sheria hiyo pia imeanzisha vyanzo vipya vya mapato kupitia bidhaa za tumbaku na sukari inayoagizwa kutoka nje.

Katika sheria hiyo, ushuru wa Sh20 utatozwa kwa kila sigara 1,000 na kwa kila kilo ya sukari inayoingizwa nchini, fedha ambazo zitaelekezwa kugharamia Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote.

Kwa upande wa wafanyabiashara wadogo, sheria hiyo imeleta nafuu kwa kuongeza kiwango cha mauzo ya mwaka kinachostahili mfumo wa kodi ya makadirio kutoka Sh100 milioni hadi Sh200 milioni.

Hatua hiyo inatarajiwa kuwawezesha wafanyabiashara wengi zaidi kunufaika na mfumo huo rahisi wa kodi.

Aidha, kiwango cha kodi kwa biashara zenye mauzo ya kati ya Sh11 milioni na Sh200 milioni kwa mwaka kimepunguzwa kutoka asilimia 4.5 iliyopendekezwa awali hadi asilimia nne, na walipakodi wapya watakaosajiliwa chini ya mfumo huo pia watapata msamaha wa kodi ya mapato kwa mwaka mmoja.

Katika sekta ya madini, Serikali imebana zaidi motisha za kikodi zinazotolewa kupitia mikataba maalumu ya uwekezaji. Kuanzia sasa, misamaha ya kodi itatumika tu katika kipindi cha ujenzi wa miradi ya madini na haitahusisha bidhaa za mafuta.

Aidha, kampuni zitakazobainika kutumia vibaya misamaha hiyo zitapokonywa fursa hizo na kulazimika kulipa kodi zote walizosamehewa.

Mabadiliko mengine ya kiutawala ni jukumu la ukusanyaji wa kodi ya majengo kuhamishiwa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwenda kwa mamlaka za serikali za mitaa.

Hatua hiyo ya Serikali inalenga kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya ndani katika ngazi za halmashauri.

Sheria hiyo pia imepanua matumizi ya fedha zinazokusanywa kupitia Tozo ya Maendeleo ya Reli, ambapo sasa zitatumika pia kufadhili miundombinu inayounga mkono uchakataji wa bidhaa na kuongeza thamani ya mazao, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuharakisha ukuaji wa viwanda.

Pamoja na kupitisha hatua mbalimbali za kuongeza mapato, Bunge liliondoa baadhi ya mapendekezo yaliyokuwa yakipingwa kabla ya kuidhinisha sheria hiyo.

Miongoni mwa mapendekezo yaliyoondolewa ni ushuru wa Sh10 kwa kila kilo ya sukari inayozalishwa nchini.

Sambamba na hilo, Serikali imeendelea na msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa mafuta ya kupikia yanayozalishwa kwa kutumia mbegu za mafuta zinazolimwa nchini, hatua inayolenga kuhamasisha uzalishaji wa ndani na kusaidia kudhibiti bei kwa watumiaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *