
Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu ameagiza jeshi la nchi hiyo kuongeza mashambulizi na kuharibu miundombinu yote ya kundi la Hezbollah kusini mwa Lebanon, hatua inayozidisha tena mvutano wa muda mrefu kati ya pande hizo mbili.
Akizungumza katika ziara ya kuwatembelea wanajeshi wa Israel, Juni 30, 2026, Netanyahu amesema agizo hilo linahusu miundombinu yote ya kijeshi ya Hezbollah, iwe ya juu ya ardhi au chini ya ardhi, ikiwemo mtandao wa mahandaki unaodaiwa kutumika kurusha mashambulizi dhidi ya Israel.
Amesisitiza kuwa jeshi la Israel halitaondoka katika maeneo ya mpakani hadi Hezbollah itakapokubali kuweka chini silaha.
“Israel itaendelea kuchukua hatua zote kuhakikisha usalama wake unalindwa dhidi ya tishio la Hezbollah,” Netanyahu amenukuliwa akisema katika mkutano wake na wanajeshi.
Israel inalitaja kundi la Hezbollah kama sehemu muhimu ya mtandao wa washirika wa Iran katika kanda hiyo, na inadai imepunguza uwezo wake wa kijeshi katika miezi ya hivi karibuni kupitia mashambulizi ya mara kwa mara.
Hata hivyo, Lebanon pamoja na Hezbollah wamepinga vikali hatua hizo, wakisema ni uvamizi unaokiuka sheria za kimataifa na kuongeza hatari ya vita vipya katika mpaka wa kusini.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Lebanon, maeneo kadhaa ya mpakani yameendelea kushuhudia taharuki na ulinzi mkali, huku raia wakihofia kuongezeka kwa mapigano makali zaidi.
Serikali ya Lebanon imetaka jamii ya kimataifa kuingilia kati kuzuia hali hiyo kuzidi kuwa mbaya.
Wakati huohuo, mvutano kati ya Iran na Marekani umeendelea kuonyesha dalili za kusuasua baada ya pande hizo kushindwa kufikia makubaliano ya moja kwa moja katika mazungumzo yanayoendelea Doha, Qatar.
Mazungumzo ya Iran na Marekani yasuasua Doha
Maofisa wa Iran wamesema hawako tayari kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na Marekani hadi masharti kadhaa ya awali kuhusu makubaliano ya kusitisha mapigano na mpango wa nyuklia yatakaporekebishwa.
Wameeleza kuwa mazungumzo lazima yaanze kwa kurekebisha makubaliano ya muda yaliyosainiwa hivi karibuni.
Kwa upande wake, Marekani kupitia wajumbe wake wa ngazi ya juu, Jared Kushner na Steve Witkoff, imeendelea kushiriki mazungumzo ya upatanishi nchini Qatar, ingawa Tehran inasisitiza kuwa mazungumzo ya moja kwa moja bado hayajawezekana.
Mpatanishi mkuu upande wa Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, amenukuliwa akisema kuwa Iran inaendelea kuamini njia ya kidiplomasia lakini pia ipo tayari kujilinda iwapo mazungumzo yatashindwa kufikia makubaliano ya kudumu.
“Tunaendelea na njia ya mazungumzo, lakini kama haitazaa matunda, tutakuwa tayari kwa vita na tutajibu ipasavyo,” amenukuliwa akisema.
Mvutano huo umeongezeka kufuatia mapigano ya
Juni kati ya Iran na Israel yaliyohusisha pia mashambulizi ya Marekani dhidi ya maeneo ya nyuklia ya Iran, kabla ya kusitishwa kwa muda kwa mapigano hayo ili kutoa nafasi ya diplomasia.
Hata hivyo, licha ya kusitishwa kwa mapigano, bado hakuna makubaliano ya kudumu yaliyofikiwa, na hali ya sintofahamu inaendelea kuifanya Mashariki ya Kati kubaki katika taharuki kubwa ya kisiasa na kijeshi.