Dar es Salaam. Jitihada za Benki ya ICBC Standard (ICBC Standard Bank PLC) ya nchini Uingereza na Serikali ya Tanzania kuzima kesi ya Kikatiba inayozikabili inayotokana na madai ya ufisadi wa Dola 8.4 milioni za Marekani (zaidi ya Sh22 bilioni) mali ya Serikali ya Tanzania zimegonga ukuta.

Hatua hiyo inatokana na uamuzi wa Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma kutupilia mbali pingamizi lililowekwa na benki hiyo na Serikali ya Tanzania, zikipinga kesi hiyo na kuiomba mahakama iifute kwa madai kuwa aliyeifungua hana haki ya kisheria kufungua kesi hiyo.

Badala yake, mahakama hiyo imesema kuwa mlalamikaji aliyefungua kesi hiyo ana haki ya kuchukua hatua hiyo kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 kama ambavyo imekuwa ikirekebishwa, na hivyo itaendelea kuisikiliza kesi hiyo.

Kesi hiyo ya Kikatiba namba 29 ya mwaka 2021 imefunguliwa na Mtanzania, Sioi Graham Solomon dhidi ya benki ICBC Standard Bank PLC (awali ikijulikana kama Standard Bank PLC), Stanbic Bank Tanzania Limited ambayo ni benki dada na ICBC, Waziri wa Fedha na Mipango na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania (AG).

Katika kesi hiyo Sioi anapinga malipo ya Dola 8.4 milioni za Marekani ambazo Standard Bank/ICBC Standard Bank iliilipa Serikali ya Uingereza.

Fedha hizo ni sehemu ya Dola 14.4 milioni (zaidi ya Sh37.87 bilioni) zilizolipwa na Serikali ya Tanzania kwa benki hiyo mwaka 2013 kama ada ya kuiwezesha kupata mkopo wa Dola 600 milioni (zaidi ya Sh1.57 trilioni kwa sasa).

Sioi anadai kuwa amefungua kesi hiyo kama wajibu wake wa kikatiba chini ya  Ibara za 26 na 27 zinazompa haki na wajibu kama raia wa Tanzania kulinda mali za umma kwa kuwa Standard Bank ilikiri yenyewe kuwa mkataba wake na Serikali iliupata kwa njia za udanganyifu.

Walalamikiwa walimwekea pingamizi wakitaka mahakama isiikilize kesi hiyo badala yake iitupilie mbali, pamoja na hoja nyingine wakidai kuwa hana haki ya kisheria kufungua kesi hiyo kwa kuwa hana maslahi katika fedha hizo anazozilalamikia, ambazo ni mali ya Serikali.

Hata hivyo, Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na jopo la majaji watatu wanaoisikiliza kesi hiyo, Amir Mruma (kiongozi wa jopo) Dk  Fatma Khalfan na Dk Everisto Longopa, imetupilia mbali hoja zote za walalamikiwa.

Katika uamuzi huo ulioandikwa na Jaji Mruma kwa niaba ya jopo, Mahakama hiyo imeelezea kwa undani namna wananchi walivyo na haki na wajibu kikatiba  kulinda mali ya umma na kupambana na ubadhirifu na matumizi mabaya ya rasilimali za umma.

Chimbuko la kesi

Chimbuko la kesi hiyo ni mchakato wa mkopo wa Dola 600 milioni kwa Serikali ya Tanzania uliowezeshwa  na Standard Bank PLC (wakati huo), ya Uingereza kwa kushirikiana na benki dada, Stanbic Tanzania mwaka 2013.

Serikali ya Tanzania ililazimika kutafuta mkopo huo ili kufidia upungufu wa fedha katika Bajeti ya mwaka 2011/2012,  kwa ajili ya utekelezaji miradi mbalimbali baada ya kukabiliwa na upungufu wa Dola 800 milioni katika bajeti hiyo.

Hivyo Novemba 15, 2012 Serikali iliziteua  Stanbic Bank Tanzania na Standard Bank PLC  ambazo  zilishirikiana zikiwa ni miongoni mwa taasisi za kifedha zilizowasilisha mapendekezo yake kwa Waziri wa Fedha na Uchumi, wakati huo, Mustafa Mkulo.

Katika pendekezo lake, benki hizo pamoja na mambo mengine, zilieleza kuwa zitaiwezesha Serikali kupata mkopo wa Dola 550 milioni, kabla ya baadaye kuongezwa kiasi cha mkopo huo na kufikia Dola 600 milioni.

Pia zilipendekeza kuwa zingeiwezesha Serikali kupata mkopo huo kwa ada ya uwezeshaji wa upatikanaji mkopo huo ya asilimia 1.4 ya mkopo huo na kwa riba ya asilimia 6.5 na muda wa kuanza kulipa ulikuwa miaka saba.

Serikali ilikubaliana na mapendekezo ya benki hizo na kuzipa jukumu hilo, ambapo ziliiwezesha kupatikana kwa mkopo huo wa Dola 600 milioni uliotolewa Machi 2013 (wakati bajeti husika ikiwa imepita) kwa ada ya asilimia 2.4 ya mkopo, badala ya asilimia 1.4 ambayo ziliiweka katika mapendekezo yake iliyoyawasilisha kwa waziri.

Wakati huo, Sioi alikuwa ofisa wa benki hiyo ya Stanbic, akiwa mwanasheria wa benki hiyo.

Baadaye Februari 2015 Standard Bank PLC iliuza asilimia 60 ya hisa zake kwa Industrial Commercial Bank of China Limited (ICBC) na kuanzia hapo Standard Bank PLC ikaitwa ICBC Standard Bank PLC.

Desemba 2015 ICBC Standard Bank ilijishtaki yenyewe kwa Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa Makubwa ya Udanganyifu ya Uingereza (Serious Fraud Office -SFO) kuwa ilishindwa kuizuia Stanbic na au Shose Sinare na Bashir Awale kujihusisha na rushwa katika mchakato wa upatikanaji mkopo huo.

Shose alikuwa ni Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wakubwa na Uwekezaji wa Stanbic Tanzania kabla ya kujiuzulu utumishi mwaka 2013 na Awale alikuwa mkurugenzi wa benki hiyo.

Katika taarifa yake kwa SFO, ICBC Standard ilieleza kuwa katika kufanikisha rushwa hiyo walimhusisha kampuni ya Ushauri wa Uwekezaji, Huduma za uwezeshaji na Upatikanaji wa Fedha, Enterprise Growth Market Advisors Limited (Egma).

Benki hiyo ilifafanua kuwa katika mpango huo ada ya uwezeshaji upatikanaji mkopo huo iliongezwa kwa asilimia moja ya kiasi cha mkopo husika, kutoka asilimia 1.4 hadi 2.4.

Hivyo asilimia hiyo moja iliyoongezwa katika ada ya mkopo uliowezeshwa (Dola 600 milioni), ambayo ni Dola 6 milioni sawa na zaidi ya Sh15.78 bilioni kwa sasa ililipwa kwa kampuni hiyo ya Egma kwa madai kuwa ilihusika katika kutoa ushauri upatikanaji mkopo huo.

Kutokana na kukiri huko, ICBC Standard ilikwepa kufunguliwa mashtaka kwa kulipa adhabu ya kifedha na kukubali masharti mengine chini ya Makubaliano ya Kuahirisha Mashtaka (Deferred Prosecution Agreement – DPA) yaliyoidhinishwa na Mahakama ya Crown Court, Southwark, Uingereza, mwaka huo huo wa 2015.

Usikose kufuatilia sehemu inayofuata kujua nini kilitokea baada ya benki hiyo kujishtaki yenyewe na kuibua tuhuma hizo dhidi ya benki dada na maofisa wake.

Itaendelea kesho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *