Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeanza maandalizi ya kufanya mapitio ya sheria mbalimbali za nchi ili ziendane na mahitaji ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Hilo linafanyika baada ya kuonekana kuwa mfumo wa sheria wa sasa uliopo unapaswa kwenda sambamba na mabadiliko ya kiuchumi, kiteknolojia na kijamii yanayolengwa katika miaka ijayo.

Hatua hiyo inakuja wakati Serikali imeanza rasmi utekelezaji wa Dira 2050 sambamba na mwaka mpya wa bajeti wa 2026/27 leo Jumatano, Julai 1, 2026 huku ikisisitiza kuwa mafanikio ya dira hiyo hayatategemea tu sera na mipango, bali pia uwepo wa sheria zinazowezesha utekelezaji wake.

Akizungumza baada ya kutembelea maonyesho ya 50 ya biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DiTF), Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainab Katimba amesema kazi hiyo itasimamiwa na Tume ya Marekebisho ya Sheria ili kuhakikisha mfumo wa sheria unaendana na mwelekeo mpya wa maendeleo ya Taifa.

“Kuna mabadiliko makubwa tunayotarajia kuyatekeleza kupitia Dira 2050 na mafanikio yake yanategemea uwepo wa sheria zinazowezesha utekelezaji wake,” amesema.

Amesema marekebisho hayo yatagusa maeneo mbalimbali muhimu yatakayochochea ukuaji wa uchumi, uwekezaji, biashara na matumizi ya teknolojia huku akisisitiza sheria zinapaswa kuendana na kasi ya mabadiliko yanayotokea duniani.

Hilo linasemwa wakati Tanzania inaelekea katika uchumi unaotegemea zaidi mifumo ya kidijitali na matumizi madogo ya fedha taslimu hali inayohitaji sheria zinazoweka mazingira rafiki kwa ubunifu, biashara za kidijitali na huduma za kifedha za kisasa.

“Tunapaswa kuhakikisha sheria zetu zinaendana na maendeleo ya teknolojia. Tunaelekea katika uchumi wa kidijitali na matumizi ya mifumo ya kisasa ya kifedha, hivyo sheria lazima ziwezeshe mabadiliko hayo,” amesema.

Amesema kupitia Tume ya Marekebisho ya Sheria, Serikali itaendelea kufanya tathmini ya sheria zilizopo ili kubaini maeneo yanayohitaji kuboreshwa au kufutwa na kuweka mfumo wa kisheria unaoendana na mazingira ya sasa na ya baadaye.

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeanza kutekelezwa Julai 1, 2026 ambayo inalenga kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kisasa, shindani na jumuishi unaochochewa na viwanda, teknolojia, ubunifu, matumizi ya maarifa na rasilimali watu wenye ujuzi.

Miongoni mwa vipaumbele vikuu vya Dira 2050 ni kuharakisha mageuzi ya uchumi wa kidijitali, kuongeza thamani ya mazao na rasilimali za madini, kukuza sekta ya viwanda na biashara, kuimarisha kilimo cha kisasa chenye tija, kuendeleza uchumi wa buluu, kuwekeza katika nishati ya uhakika, pamoja na kuboresha miundombinu ya reli, bandari, viwanja vya ndege na barabara ili kuongeza ushindani wa uchumi.

Aidha, dira hiyo inalenga kujenga rasilimali watu yenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira, kuboresha mifumo ya afya na elimu, kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na matumizi ya Tehama katika utoaji wa huduma za umma.

Alitumia nafasi hiyo kuwataka wananchi kutumia fursa ya Maonesho Sabasaba kupata huduma za msaada wa kisheria zinazotolewa bure na Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na taasisi zilizo chini yake.

Katimba amesema Serikali imeendelea kutumia Sabasaba kama jukwaa la kuwafikia wananchi kwa kuwapa elimu ya sheria na ushauri wa kisheria kuhusu changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo.

“Nitumie fursa hii kuwakaribisha Watanzania wote wenye changamoto za kisheria kufika katika banda la Wizara ya Katiba na Sheria ili waweze kupata huduma za msaada wa kisheria,” amesema.

Amesema huduma zinazotolewa zinasaidia wananchi kupata ufafanuzi wa masuala ya kisheria, kuelekezwa namna ya kushughulikia migogoro yao na kufahamu haki pamoja na wajibu wao kwa mujibu wa sheria.

Mmoja wa washiriki katika maonyesho hayo, Rehema Mussa amesema uwepo wa msaada kisheria unasaidia kukamilisha taratibu mbalimbali zinazohitajika katika biashara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *