Misafara ya wanaharakati wanaopinga ubeberu, wasomi, waandishi wa habari na wawakilishi wa vituo vya Kiislamu kutoka kote barani Ulaya inaendelea kuwasili Tehran kushiriki katika mazishi ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei aliyeuawa shahidi katika shambulizi la kushtukiza la Marekani na Israel.

Makundi hayo, ambayo yanajumuisha wanachama wa mhimili wa kupinga ubeberu wa Italia, watafiti, maprofesa wa vyuo vikuu, waandishi wa habari, wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi vinavyopinga vita na waungaji mkono Mapinduzi ya Kiislamu kutoka nchi kadhaa za Ulaya, yameanza kuwasili Iran licha ya serikali za nchi za Ulaya kutopewa mwaliko rasmii wa kushiriki katika shughuli hiyo.

Chanzo kimoja cha kidiplomasia kimesema shughuli ya mazishi ya Imam Khamenei imewavutia wanaharakati na wasomi kutoka kote Ulaya ambao wanataka kuonyesha mshikamano wao na watu wa Iran na kutangaza upinzani wao dhidi ya muungano wa ‘Shetani Mkubwa na Mdogo’ (Marekani an Israel).

Ujumbe huo unajumuisha watu wanaomtambua Kiongozi marehemu wa Iran kama nembo ya kupigania uhuru, kupinga utawala wa kifalme, na uungaji mkono kwa mataifa yanayokandamizwa kwa miongo kadhaa.

Chanzo kingine cha kidiplomasia kimethibitisha kwamba visa zimetolewa kwa wawakilishi kutoka vituo na taasisi za Kiislamu nchini Uholanzi, pamoja na wahamiaji wa Iran na raia wa Iraq na Uturuki wanaoishi nchini humo.

Harakati kama hizo pia zinaripotiwa kutoka nchi nyingi za Ulaya, huku wanaharakati, watu mashuhuri wa masuala ya kitamaduni, na wanajamii wa Kiislamu wakielekea Tehran kwa ajili ya shughuli ya kuaga mwili wa Ayatullah Ali Khamenei.

Vyanzo vinasema harakati za watu wa kawaida, zinazoenea katika miji mbalimbali ya Ulaya, zinaonyesha taathira ya kimataifa ya maono na fikra za Kiongozi huyo wa harakati za kupigania na kutetea uhuru wa kitaifa na mapambano dhidi ya tawala za kibeberu.

Washiriki kutoka Ulaya hawawakilishi jumbe rasmi za serikali bali wanaelekea Iran kama wawakilishi wa mataifa na harakati ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikimtambua Ayatullah Khamenei kama sauti ya upinzani dhidi ya tawala za kimabavu.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei, akifafanua uamuzi wa Iran wa kutotoa mialiko rasmi kwa serikali za nchi za Ulaya, amesema: “Sababu ya uamuzi huu iko wazi kabisa. Wale watakaoshiriki katika shughuli ya mazishi ni wale ambao wamesimama upande sahihi wa historia.”

“Nchi za Ulaya zilisimama upande mbaya wa historia katika vita vilivyopita na vita vya hivi karibuni dhidi ya Iran,” amesema Esmaeil Baqaei.

Mbali na wawakilishi wa asasi za kiraia, waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari vya Ulaya kutoka Uingereza, Denmark, Italia, Uholanzi na Austria pia wamewasili Iran au watawasili katika siku zijazo ili kuripoti matukio ya shughuli ya mazishi ya Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu.

Mahudhurio makubwa ya vyombo vya habari vya kimataifa katika shughuli hiyo ni ishara kwamba marasimu ya kuaga mwili wa hayati Imam Ali Khamenei imepita tukio la kitaifa na kuwa tukio la kimataifa, wakati huu macho ya dunia yakielekezwa Iran inayomuaga shakhsia aliyeongoza Jamhuri ya Kiislamu kuvuka mojawapo ya vipindi vyenye misukosuko zaidi katika historia ya kisasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *