
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesisitiza kuwa umati mkubwa wa wananchi utakaojitokeza katika shughuli ya mazishi ya Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, utakuwa “jibu madhubuti” dhidi ya vitendo vya kigaidi, ukatili na mbinu za kibeberu. Amesema kuwa tukio hilo litakuwa dhihirisho la wazi la umoja wa taifa la Iran na dhamira yake isiyotetereka katika kulinda uhuru na heshima ya nchi.
Rais Pezeshkian aliyasema hayo katika ujumbe wake jana Alhamisi kwa taifa la Iran, wakati wa maandalizi ya shughuli ya kuaga na mazishi ya Imam Khamenei, ambaye aliuawa shahidi mnamo Februari 28, siku ya kwanza ya vita vya kichokozi Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Rais Pezeshkian ameeleza imani yake kuu juu ya nafasi ya wananchi katika kipindi hiki cha mabadiliko, akibainisha kuwa katika shughuli hiyo adhimu ya mazishi, taifa la Iran litathibitisha tena utiifu wake kwa njia na malengo makuu ya Kiongozi huyo aliyeawa shahidi.
Pezeshkian amesisitiza kuwa ushiriki mkubwa wa wananchi katika tukio hili la kihistoria utathibitisha, bila shaka yoyote, uaminifu wao kwa njia iliyowekwa na marehemu Kiongozi.
Ameongeza kuwa kuuawa shahidi Ayatullah Khamenei kumeacha simanzi nzito si tu miongoni mwa Wairani, bali pia katika Ulimwengu wa Kiislamu na mataifa yote yanayopigania uhuru. Hata hivyo, amesisitiza kuwa pigo hilo limefichua ukweli usiopingika kwamba misingi imara ya utawala wa Kiislamu imejengeka juu ya “nguzo madhubuti za imani, malengo matukufu, na utashi wa taifa kubwa.”
Rais Pezeshkian ameusifu upeo wa mawazo na utendaji wa Shahidi Imam Khamenei katika kulinda uhuru wa Iran, na kuimarisha demokrasia ya kidini na utamaduni wa Muqawama (mapambano) katika baadhi ya vipindi vyenye changamoto kubwa zaidi katika historia ya kisasa ya taifa la Iran.
Amesema kuwa jina, mawazo na mafanikio ya Shahidi Ayatullah Khamenei bila shaka yatasalia milele katika kumbukumbu ya kihistoria ya taifa la Iran na dhamiri ya watu wote wanaopigania haki duniani kote.
Rais wa Iran ametoa wito kwa Wairani wote, bila kujali kabila, dini au mielekeo yao ya kisiasa, kujitokeza kwa wingi katika shughuli ya mazishi ili kuonesha taswira ya umoja wa kitaifa na uaminifu kwa malengo matukufu ya mfumo wa Kiislamu.