
Kamandi Kuu ya Majeshi ya Iran, maarufu kama Kamandi ya Khatam al-Anbiya, imetoa onyo kali kuwa, uingiliaji wowote wa kijeshi wa Marekani katika Lango Bahari la Hormuz utajibiwa kwa kasi na maamuzi madhubuti na vikosi vya ulinzi vya Iran, huku ikisisitiza kuwa njia hiyo muhimu ya bahari iko chini ya mamlaka kamili ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Katika taarifa iliyotolewa jana Alhamisi, makao makuu hayo ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yamethibitisha tena mamlaka ya Tehran juu ya Lango Bahari la Hormuz, yakiitahadharisha Marekani dhidi ya jaribio lolote la kuhujumu usalama wa eneo hilo la kimkakati.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa: “Lango Bahari la Hormuz si uwanja wa michezo kwa ajili ya Marekani yenye nia ya uchokozi; bali ni himaya isiyoweza kupingwa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Usalama na utulivu wa njia hiyo muhimu ya nishati ni mstari mwekundu kwa Vikosi vya Jeshi lenye nguvu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.”
Onyo hilo limetolewa wiki kadhaa baada ya vita vya uchokozi vya Marekani na Israel dhidi ya Iran, ambapo majeshi ya Iran yalifanya mashambulizi makali ya kulipiza kisasi na kuzuia safari za meli katika njia hiyo ya kimkakati, kabla ya kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano na mkataba wa maelewano (MoU) tete kati ya Tehran na Washington uliotuliza hali ya mambo.
Makubaliano hayo ambayo yana vipengele 14, miongoni mwa mambo mengine, yanataka kuondolewa vizuizi vya wakati wa vita katika Lango Bahari la Hormuz, njia muhimu ya nishati duniani, kwa sharti kwamba Marekani na washirika wake wasitishe kikamilifu uchokozi wao wa kijeshi dhidi ya Iran na washirika wake wa kikanda, wakiwemo wale wa Lebanon.
Kamandi ya Khatam al-Anbiya imesisitiza kuwa: “Meli zote za mafuta na za kibiashara zinatakiwa kutumia njia zilizoainishwa na Iran kwa ajili ya safari yoyote salama kupitia kwenye Lango Bahari la Hormuz,”
Aidha kamani hiyo ya majeshi ya Iran imeonya kuwa: “Ukiukaji wowote wa maelekezo haya, kupotoka kutoka kwa njia zilizopangwa, au kupuuza itifaki za urambazaji za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Lango la Hormuz, utajibiwa mara moja kwa nguvu na Vikosi vya Silaha, na jambo hilo litahatarisha usalama wa vyombo husika vinavyokiuka kanuni hizo.”