
Dar es Salaam. Katika ulimwengu wa uhusiano, busu hutazamwa kama kilele cha mahaba, ishara ya ukaribu, na kiunganishi cha mioyo miwili.
Hata hivyo, nyuma ya hisia hizo za kusisimua, kuna ulimwengu mwingine usioonekana kwa macho—ulimwengu wa viumbe hai wadogo.
Kazi za kitafiti za hivi karibuni za kisayansi zimeibua mjadala mzito baada ya kubainika kuwa busu moja la dhati la sekunde 10 pekee linaweza kuhamisha hadi bakteria milioni 80 kati ya wapenzi wawili.
Licha ya takwimu hizo zinazoweza kushtua wengi, wataalamu wa afya na saikolojia wanasisitiza kuwa busu si jambo la kuogopwa wala kuachwa. Badala yake, ni tabia yenye faida nyingi mwilini, mradi tu kuwe na uelewa wa tahadhari zinazostahili.
Tahadhari kiafya
Utafiti ulioongozwa na Profesa Remco Kort kutoka Shirika la Utafiti wa Kisayansi la Uholanzi (TNO), ulibaini kuwa kinywa cha binadamu ni makazi ya aina zaidi ya 700 za bakteria.
”Busu la dhati linalohusisha mabadilishano ya mate ni moja ya mifano mikubwa ya mwingiliano wa viumbe hai kati ya binadamu,” anasema. Utafiti wake ulibaini kuwa wapenzi wanaobusiana angalau mara tisa kwa siku wana uwezekano mkubwa wa kuwa na mfumo wa bakteria unaofanana kwenye ndimi zao, jambo linalosaidia miili yao kukabiliana na maambukizi yanayofanana.
Aidha, pamoja na utamu na faida zake, busu linaweza kuwa daraja la magonjwa ikiwa wahusika hawatazingatia afya ya kinywa.
Kuna aina fulani za bakteria na virusi ambavyo ni hatari na vinaweza kuambukizwa kwa urahisi kama vile ‘streptococcus mutans’
Huyu ndiye adui mkuu wa meno. Ikiwa mwenza mmoja ana matatizo makubwa ya meno na kutoosha kinywa, anaweza kumshirikisha mwenzake bakteria hawa wanaosababisha matundu kwenye meno. Pia yuko ‘porphyromonas gingivalis’ anayehusishwa na magonjwa ya fizi.
Madhara mengine ni homa ya tezi inayosababishwa na kirusi cha ‘epstein-barr. Huambukizwa kwa urahisi kupitia mate na kusababisha uchovu uliopitiliza na homa.
Herpes Simplex (HSV-1): Huyu husababisha vidonda vya baridi mdomoni. Ni rahisi sana kuambukizwa wakati vidonda vikiwa vimechipua.
Upande wa pili wa busu
Wataalamu wanashauri kuwa busu ni “chanjo ya asili.” Unapobusu, unashirikiana bakteria na mwenza wako, jambo ambalo huimarisha mfumo wa kinga kwa kuufanya mwili uanze kutengeneza kingamwili dhidi ya vimelea vipya.
Dk Gail Shust, mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza anabainisha: “Ingawa namba milioni 80 inaonekana kubwa, wengi wa bakteria hawa ni rafiki na ni muhimu kwa afya ya kinywa na mfumo wa chakula.”
Mbali na kinga, busu huchochea utolewaji wa homoni za “furaha” kama vile ‘oxytocin’ inayojulikana kama homoni ya upendo, inayoongeza ukaribu na uaminifu.
Homoni nyingine ni ‘ dopamine inayochochea hisia za hamu na zawadi mwilini na ‘ serotonin’ inayosaidia kurekebisha hisia na kuzuia msongo wa mawazo.
Nini cha Kufanya?
Ili kuendelea kufurahia faida za busu bila kuingia kwenye mtego wa maradhi, wataalamu wanatoa mwongozo ufuatao:
Moja, zingatia usafi wa kinywa: Kupiga mswaki na kutumia uzi wa kusafishia meno, hupunguza idadi ya bakteria wabaya.
Pili,epuka kubusu ukiwa na vidonda: Ikiwa una kidonda mdomoni au homa ya mafua, ni busara kusubiri mpaka upone ili kumlinda mwenza wako.
Tatu, uaminifu: Kuwa na mwenza mmoja hupunguza hatari ya kukutana na vimelea vigeni na hatari ambavyo mwili wako haujazoea.
Muhimu kukumbuka kuwa busu ni lugha ya asili inayovuka mipaka ya maneno. Ingawa sayansi inatuambia kuwa tunabadilishana mamilioni ya viumbe, ukweli unabaki kuwa mbadilishano huo mara nyingi huleta afya na ukaribu zaidi kuliko madhara.
Kama alivyowahi kusema mwanasayansi mmoja, “Sisi ni viumbe wa bakteria; busu ni namna tu ya kusema ‘karibu katika ulimwengu wangu wa vimelea’.”
Makala hii imetafsiriwa kutoka mtandao wa The Conversation.