DAR ES SALAAM: Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP-Centre), David Kafulila, amesema mafanikio ya Tanzania kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050 yanahitaji ongezeko kubwa la uzalishaji na mabadiliko ya kasi ya maendeleo.
Amesisitiza kuwa lengo hilo linahitaji kiwango cha uzalishaji kinacholingana na kile kilichopatikana katika kipindi cha miaka 25 iliyopita (2000 hadi 2025).
Akizungumza katika mhadhara wa umma uliofanyika katika Chuo Kikuu Mzumbe ndaki ya Mbeya leo Ijumaa Julai 03, 2026 Kafulila amesema changamoto iliyopo ni kuhakikisha taifa linaelewa ukubwa wa dhamira hiyo, akibainisha kuwa lengo la Dira ya Maendeleo 2050 linahitaji mtazamo mpya wa pamoja katika ngazi ya mtu mmoja mmoja, vijiji na taifa kwa ujumla ili kuhakikisha uzalishaji na tija vinaongezeka kwa kiwango kikubwa zaidi.
Amesema Tanzania inalenga kuingia katika kundi la nchi 21 duniani zenye uchumi wa dola trilioni moja, akieleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan alipozindua Dira ya Maendeleo 2050 alisisitiza kuwa lengo hilo linawezekana endapo kutakuwa na mabadiliko ya msingi katika namna ya kufikiri na kutenda kwa wananchi na taasisi mbalimbali.
Kafulila ameongeza kuwa iwapo taifa litaendelea na mtazamo uleule wa zamani katika ngazi ya mtu binafsi, kijiji na taifa, lengo hilo linaweza lisifikiwe au kufikiwa kwa kiwango cha chini, akisisitiza kuwa mafanikio yatategemea “total turnaround” ya fikra na utekelezaji katika nyanja zote za kiuchumi na kijamii ili kufanikisha mabadiliko ya kweli kuelekea mwaka 2050.
