DAR ES SALAAM: Rais wa Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Mbeya, Profesa Henry Mollel amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP-Centre), David Kafulila, ameleta mabadiliko makubwa ya fikra nchini kuhusu utekelezaji wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), hatua inayochochea matumizi ya mfumo huo kama nyenzo ya maendeleo ya taifa.

Akizungumza katika mhadhara wa umma uliofanyika leo Ijumaa, Julai 3, 2026, chuoni hapo, Profesa Mollel amesema jukwaa hilo ni fursa muhimu kwa wanafunzi na vijana kupata uelewa mpana kuhusu dhana ya PPP, ili waweze kutambua nafasi yake katika kuibua fursa za maendeleo na kushiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa taifa unaolengwa na Dira ya Maendeleo 2050.

Amesema hapo awali dhana ya PPP ilikuwa ikizungumzwa zaidi kinadharia bila kuleta athari kubwa katika utekelezaji, lakini kupitia uongozi wa Kafulila, uelewa kuhusu umuhimu wa mfumo huo umeongezeka na kuanza kubadili mtazamo wa wadau wengi kuhusu mchango wake katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Profesa Mollel ameongeza kuwa Chuo Kikuu Mzumbe kinajivunia ushirikiano wake na Kafulila pamoja na PPP-Centre, kikisisitiza kuwa kitaendelea kuunga mkono juhudi za kuendeleza elimu na tafiti kuhusu PPP ili kuhakikisha maarifa hayo yanazalisha matokeo chanya kwa jamii na kuchangia kufikiwa kwa malengo ya uchumi wa Tanzania ifikapo mwaka 2050.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *