
Askari usalama wa mji wa Tehran wamewatia baroni watu sita waliokuwa wakifanya kazi katika mitandao ya maadui na dhidi ya mapinduzi. Mamluki hao walitiwa mbaroni katika eneo la Pardis, mashariki mwa mkoa wa Tehran.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Uhusiano wa Umma ya Kituo cha Hazrat Seyyed al-Shohada (AS) cha IRGC katika mkoa wa Tehran, washukiwa hao walikuwa wakituma maudhui na kubadilishana taarifa kikamilifu na mitandao ya maadui na ile inayopinga mapinduzi.
Taarifa ya IRG imebainisha kuwa, mamluki hao 6 walihusika pia katika ghasia za mwezi Disemba mwaka jana na kuchochea machafuko nyakati za usiku kwa lengo la kuibua mazingira ya ukosefu wa usalama wakiongozwa na kusimamiwa na maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Watu hao 6 wametiwa nguvuni baada ya kufuatiliwa na kuchunguzwa kwa muda harakati na shughuli zao kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii kama vile Instagram na Telegram.
Operesheni ya kuwanasa mamluki hao imefanywa kwa nyakati tofauti kufuatia kutolewa waranti na vyombo vya mahakama.
Mamlaka husika za Iran zinasisitiza kuwa ingawa raia wana haki ya kutumia majukwaa ya mitandao ya kijamii kwa mujibu wa sheria; kitendo cha kuwa uhusiano wowote na mitandao ya adui kitapelekea kuchukuliwa taratibu za kimahakama na hatua za kisheria.