Dar es Salaam. Mabadiliko ya uongozi katika taasisi ya kimataifa ya Hanns R. Neumann Stiftung (HRNS) yametajwa kuleta matumaini ya mwendelezo wa programu za maendeleo zinazolenga kuongeza tija, kipato na ustawi wa wakulima wadogo wa kahawa nchini.

HRNS, taasisi inayojihusisha na maendeleo endelevu ya jamii za wakulima wa kahawa duniani, imemtangaza Dk Karen Hadem kujiunga na Jens Sorgenfrei katika uongozi wa juu wa taasisi hiyo, akichukua nafasi ya Michael Opitz anayestaafu baada ya utumishi wa zaidi ya miaka 20.

Akizungumzia hilo leo Jumapili, Julai 5, 2026, Meneja wa HRNS Tanzania, Morgan Mkonyi, amesema mabadiliko hayo yanaashiria mwendelezo wa dhamira ya taasisi hiyo ya kuendelea kuleta matokeo chanya kwa jamii za wakulima.

“Tunakaribisha mwanzo wa sura mpya katika uongozi wa HRNS. Chini ya Michael Opitz, taasisi imeheshimika duniani katika kuboresha maisha ya wakulima wadogo. Tunatarajia kuendeleza mafanikio hayo chini ya uongozi mpya,” amesema.

Amesema wataendelea kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali ili kuhakikisha programu zake zinaendelea kuwafikia wakulima na kuchangia maendeleo ya jamii za vijijini.

Kwa upande wake, Michael Opitz, anayestaafu, amesema mafanikio ya taasisi hiyo yametokana na ushirikiano wa karibu kati ya wafanyakazi, washirika na jamii zinazonufaika na programu zake.

“Imekuwa heshima kubwa kushiriki katika kujenga taasisi hii. Mafanikio yaliyopatikana ni matokeo ya juhudi za pamoja za watu wengi waliokuwa na dhamira ya kuboresha maisha ya wakulima wadogo,” amesema.

Akizungumza baada ya kuteuliwa, Dk Hadem amesema ataendeleza msingi imara uliojengwa na mtangulizi wake kwa kuimarisha programu zinazowanufaisha wakulima na vijana.

“HRNS imejijengea historia ya kuleta matokeo yenye maana katika jamii. Natarajia kufanya kazi na timu yetu na washirika mbalimbali ili kuendeleza mchango huo kwa njia endelevu,” amesema.

Amesema ataendelea kutekeleza shughuli za taasisi hiyo katika nchi saba za Kusini mwa Dunia, ikiwemo Tanzania, huku ikiungwa mkono na mtaji wa kudumu unaokadiriwa kufikia euro milioni 150.

Amesema hatua hiyo itaifanya taasisi hiyo kuwa katika nafasi ya kuendelea kufadhili kwa muda mrefu programu zinazolenga kuboresha maisha ya wakulima wadogo, kulinda mazingira na kuwapatia vijana fursa za kujenga maisha bora katika jamii zinazolima kahawa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *