Mnamo Jumatatu, Julai 6, magazeti ya humu nchini yaliangazia mabadiliko ya haraka katika ulingo wa kisiasa nchini Kenya, huku majarida hayo yakijikita katika vurugu zilizosambaratisha mkutano wa Linda Mwananchi uliofanyika Kisii.

Uhakiki wa Magazeti ya Kenya
Habari kuu katika magazeti ya Kenya mnamo Jumatatu, Julai 6. Picha: Daily Nation, The Standard, The Star na Taifa Leo.
Source: UGC

1. The Standard

Kwa mujibu wa gazeti hilo, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Justin Muturi amewataka viongozi wa upinzani kuacha kuchelewesha uteuzi wa mgombea mmoja wa urais, akionya kuwa kusuasua huko kunaweza kuimarisha nafasi za Rais William Ruto kushinda Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.

Akizungumza wakati wa ibada ya kanisani Kamulu, Nairobi, Muturi alikosoa muungano huo kwa kuendelea kuweka siri kuhusu mgombea wake, akisema Wakenya wanastahili kujua ni nani atakayepeperusha bendera ya urais kwa niaba ya upinzani.

Muturi alipuuza madai kwamba kutangaza mapema mgombea wa muungano kutamweka kwenye mashambulizi ya kisiasa kutoka kwa serikali ya Kenya Kwanza.

Badala yake, alisema upinzani unapoteza muda muhimu huku ukiwaachia washirika wa Ruto nafasi ya kuwazidi ujanja kisiasa.

Aliwataka wenzake kuachana na kile alichokiita “siasa za usiri,” akisisitiza kuwa hakuna sababu ya kuendelea kuogopa.

Pia soma

Moses Kuria atabiri Ruto kuwa kiongozi wa upinzani mwenye mkono wa chuma akishindwa urais 2027

Ingawa alisisitiza kuwa bado ana nia ya kuwania tiketi ya urais ya muungano huo, Muturi alisema wazi kuwa atamuunga mkono kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ikiwa atachaguliwa kuwa mgombea wa maridhiano.

Alisisitiza kuwa umoja, badala ya maslahi binafsi, ndio unapaswa kuongoza mkakati wa upinzani kuelekea uchaguzi.

Kauli zake zinajiri miezi kadhaa baada ya viongozi wa upinzani kuahidi kumtangaza mgombea wao wa pamoja kufikia mwisho wa robo ya kwanza ya mwaka 2026, muda ambao tayari umepita.

Kuchelewa huko kumechochea uvumi kuhusu ushindani wa ndani unaowahusisha Kalonzo, Rigathi Gachagua, Martha Karua, Fred Matiang’i, Eugene Wamalwa na Muturi mwenyewe.

2. The Star

Gazeti hilo linaripoti kuwa Rais William Ruto amempinga moja kwa moja aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kuhusu madai yake ya mara kwa mara kwamba ndiye aliyemhakikishia kura za Mlima Kenya katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2022, akisisitiza kuwa alijipatia mwenyewe uungwaji mkono wa eneo hilo kupitia kampeni za kina na mawasiliano ya moja kwa moja na wapiga kura.

Akizungumza katika ibada ya kanisani Kaunti ya Embu, Ruto alipuuza madai ya Gachagua, akisema alitegemea uzoefu wake wa kisiasa, maombi na rekodi yake ya utendaji badala ya mtu yeyote ili kushinda uchaguzi.

Pia soma

Ndindi Nyoro adokeza kuhusu mipango yake ya kisiasa baada ya kula hu kwa William Ruto

Rais alisema alitembelea Embu na maeneo mengine ya Mlima Kenya wakati wa kampeni, ambapo aliwaomba wakazi kura zao na kufanya makubaliano nao moja kwa moja.

“Sasa wewe, mbunge wa muhula mmoja, utanifundisha siasa? Nimekaa kwenye siasa kwa muda mrefu, rafiki yangu. Mimi si mtu anayewategemea wengine. Ninamtegemea Mungu, maombi na kazi ambayo nimeifanya. Wengine wanasema sikuja Embu kuomba kura na kwamba watu wengine walikuja kwa niaba yangu. Mlinipigia kura kwa sababu nilikuja hapa mwenyewe na kuwaomba kura zenu. Tulikubaliana jinsi tutakavyofanya kazi pamoja,” alisema Ruto.

Aliwashutumu wakosoaji kwa kujaribu kuandika upya historia na kuwataka viongozi kuachana na mashambulizi ya kibinafsi na badala yake kujikita katika siasa za maendeleo.

Ruto pia alitetea rekodi ya serikali yake, akisema utawala wa Kenya Kwanza umetimiza ahadi kadhaa za kampeni.

Alitaja kushuka kwa bei ya mbolea, kuajiri walimu 100,000, kuongezwa kwa ufadhili wa vyuo vikuu, ujenzi wa mabweni ya wanafunzi na utekelezaji wa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) kama baadhi ya mafanikio.

Aidha, alidai kuwa hospitali za umma sasa zina dawa za kutosha na kuahidi kutoa hesabu ya utendaji wa serikali kabla ya uchaguzi ujao.

Pia soma

Magazeti ya Kenya: Upinzani wazama katika wasiwasi kuhusu madai Gachagua amesema Kalonzo tosha

Akizungumzia mazingira ya kisiasa kuelekea mwaka 2027, Ruto alikosoa kile alichokitaja kuwa siasa za ukabila, akiwatuhumu Gachagua na viongozi wa upinzani kwa kujaribu kugawa jamii mbalimbali.

Alionya kuwa ukabila, vitisho vya kisiasa na matusi haviwezi kuamua mustakabali wa Kenya na akawahimiza Wakenya kuwahukumu viongozi kwa misingi ya ajenda zao za maendeleo badala ya kauli za kisiasa.

Rais pia aliwahakikishia wananchi kuwa nchi itaendelea kuwa na amani licha ya ushindani mkali wa kisiasa, akisema serikali yake ina mpango thabiti wa kubadili uchumi na kuendeleza taifa.

3. Daily Nation

Kwa mujibu wa gazeti hilo, Mahakama Kuu imewaamuru Inspekta Jenerali wa Polisi pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) kumlipa aliyekuwa mwanafunzi wa chuo kikuu fidia ya shilingi milioni 8 baada ya kubaini kuwa haki zake za kikatiba zilikiukwa kupitia ukatili wa polisi na kucheleweshwa kwa haki kwa muda mrefu.

Uamuzi huo unatokana na tukio la mwaka 2019 ambapo Allan Omondi alipigwa na kuzuiliwa kinyume cha sheria na maafisa wa polisi karibu na Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) alipokuwa akielekea hosteli.

Pia soma

Babu Owino apuuzilia mbali msururu wa vijembe vya Caleb Amisi kwa Linda Mwananchi: “Huna lolote”

Jaji Patricia Nyaundi alibaini kuwa maafisa hao walimfanyia Omondi ukatili, mateso na udhalilishaji uliokiuka haki zake za utu na uhuru wa kibinafsi chini ya Ibara ya 28 na 29 za Katiba.

Mahakama pia iliilaumu ODPP kwa kushindwa kuhakikisha haki inatendeka baada ya kuamua kutatua suala hilo kupitia mpango wa diversion badala ya kuwafungulia mashtaka maafisa wanne waliotuhumiwa kwa shambulio hilo.

Mahakama ilielezwa kuwa ingawa ODPP ilibaini kuwa kulikuwa na ushahidi wa kutosha kuwafungulia mashtaka maafisa hao kwa kosa la kushambulia na kusababisha majeraha, mpango huo wa diversion haukutekelezwa kamwe.

Kutokana na hali hiyo, Omondi aliachwa bila fidia, bila kuombwa msamaha wala kupata aina yoyote ya haki, jambo lililomnyima haki ya kupata haki.

Jaji Nyaundi aliamua kuwa mpango wa diversion ambao hautekelezwi hauwezi kukidhi viwango vya Katiba, akisisitiza kuwa waathiriwa wanapaswa kupata suluhisho la kweli mara maamuzi kama hayo yanapofanywa.

Alitangaza kuwa ODPP ilikiuka Ibara ya 48 ya Katiba kwa kuruhusu mchakato huo kusimama bila kikomo.

4. Taifa Leo

Kwa mujibu wa gazeti hilo la Kiswahili, Waziri Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi ameendelea kuwa kimya katika mjadala unaozidi kushika kasi kuhusu nani atakuwa mgombea mwenza wa Rais William Ruto kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027, huku makundi mbalimbali ya kisiasa yakiendelea kuwapigia debe wagombea wao.

Pia soma

Ndindi Nyoro ajuta sana kumuunga mkono William Ruto katika kura ya 2022

Wakati viongozi kutoka Mlima Kenya wanamuunga mkono Naibu Rais Kithure Kindiki kubaki katika nafasi hiyo, na wengine kutoka Magharibi mwa Kenya wakimsukuma Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula, jina la Mudavadi halijatajwa sana, jambo lililozua maswali kuhusu mkakati wake wa kisiasa na malengo yake ya muda mrefu.

Ukimya huo unajiri licha ya ushindani unaoongezeka ndani ya serikali ya broad-based pamoja na ODM, ambapo makundi mbalimbali yanawapigia debe Waziri wa Madini Hassan Joho na Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya kwa nafasi ya naibu rais.

Viongozi wa upinzani pia wamemtaja Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kama anayefaa kuwania urais au nafasi ya naibu rais, jambo linaloonyesha mabadiliko yanayoendelea katika siasa za Kenya.

Badala ya kujihusisha na siasa za urithi wa madaraka, Mudavadi ameendelea kuzingatia majukumu yake serikalini, mara nyingi akiandamana na Ruto katika ziara za kimataifa huku akiendelea kuwa mtulivu katika kampeni za kisiasa za ndani.

Kauli yake kubwa ya hivi karibuni kuhusu siasa ilitolewa mwezi Juni, alipowataka wakazi wa Magharibi mwa Kenya kumuunga mkono Ruto katika azma yake ya kuchaguliwa tena na kupuuza viongozi wa upinzani wanaotafuta uungwaji mkono katika eneo hilo.

“Kuna watu wanaojifanya kutoa mwelekeo kwa jamii yetu ilhali waliondolewa madarakani kwa njia ya impeachment na hawajui mustakabali wao. Sisi kama viongozi tumeamua kumuunga mkono Rais Ruto achaguliwe tena. Niliwaambia mwaka 2022 kuwa yeye ndiye njia, na leo nawaambia tena kuwa bado ndiye njia. Tunapaswa kubaki imara na tusikubali watu wetu wapotoshwe,” alisema Mudavadi.

Pia soma

Mbadi asema hana mpango wa kuwania kiti chochote, atuma ombi la dhati kwa Ruto

Mudavadi, pamoja na Wetang’ula na Oparanya, wanaendelea kuwa miongoni mwa viongozi wakongwe wa Magharibi mwa Kenya na wanatazamwa kama wahusika muhimu katika siasa za urithi wa madaraka baada ya mwaka 2027, iwapo Ruto atashinda muhula wa pili.

Hata hivyo, ushawishi wake unazidi kupimwa na kizazi kipya cha viongozi akiwemo Sifuna na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, ambao wamepata umaarufu kupitia vuguvugu la Linda Mwananchi.

Mabadiliko hayo ya kisiasa yamezidisha maswali kuhusu iwapo Mudavadi anahifadhi ushawishi wake kwa ajili ya siasa za baadaye au anajiepusha kwa makusudi na mjadala wa sasa kuhusu mrithi wa kisiasa.

Read: ENGLISH VERSION

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia news@tuko.co.ke au WhatsApp: 0732482690.

Chanzo: TUKO.co.ke

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *