Milango ya jengo jipya la kisasa la ghorofa moja la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Iringa ilipofunguliwa rasmi jana, haikuwa tu uzinduzi wa ofisi nyingine ya Serikali.

Ilikuwa hitimisho la safari ya miaka 27 ya maono, subira na uwekezaji, huku ikifungua ukurasa mpya katika mapambano dhidi ya rushwa na ulinzi wa fedha za umma.

Jengo hilo la kisasa lenye thamani ya Sh Bilioni 1.67, lililosimama kwenye eneo lililotengwa tangu mwaka 1999 katika mtaa wa Gangilonga mjini Iringa, linaashiria hatua mpya ya Serikali ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha taasisi zinazolinda uwajibikaji, kuongeza ufanisi wa utoaji huduma na kujenga mazingira salama ya kusimamia rasilimali za taifa.

Katika ulimwengu wa sasa, ambapo rushwa imeendelea kutajwa kuwa moja ya vikwazo vikubwa vya maendeleo, uwekezaji katika taasisi za uwajibikaji umeendelea kuwa kipimo cha dhamira ya serikali kujenga uchumi unaotawaliwa na uwazi na sheria.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila, alisema jengo hilo si mafanikio ya Mkoa wa Iringa pekee, bali ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuifanya TAKUKURU kujitegemea kwa miundombinu yake na kuondokana na utegemezi wa majengo ya kupanga.

“Hatujengi majengo kwa ajili ya ufahari. Tunajenga mazingira yatakayowezesha taasisi kufanya kazi kwa uhuru, kwa usalama na bila migongano ya kimaslahi inayoweza kujitokeza pale inapolazimika kupanga ofisi kwa watu binafsi,” alisema.

Chalamila alikumbusha kuwa eneo hilo lilitafutwa na kuhifadhiwa mwaka 1999 na aliyekuwa Mkuu wa kwanza wa TAKUKURU Mkoa wa Iringa, Ernest Barulo, akisema maamuzi hayo ndiyo yaliyowezesha kizazi cha sasa kushuhudia uwekezaji huo mkubwa.

“Leo tunashuhudia matunda ya viongozi waliokuwa na maono ya mbali. Kama eneo hili lisingehifadhiwa wakati huo, pengine tusingekuwa tunazungumza kuhusu jengo hili leo,” alisema.
Mbali na kujenga majengo, Chalamila alisema vita dhidi ya rushwa haviwezi kushindwa kwa kutumia sheria pekee, bali vinahitaji pia kubadili fikra za jamii.

Alisema ndiyo maana TAKUKURU imeendelea kutumia sanaa, muziki, maigizo na klabu za wapinga rushwa mashuleni kuelimisha wananchi.

Aliwataka pia wananchi wa Iringa kulitumia jengo hilo kama mahali pa kuwasilisha taarifa za vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.

“Rushwa haiwezi kushindwa bila wananchi. Kila mwananchi ana wajibu wa kulinda fedha za maendeleo kwa kutoa taarifa pale anapoona viashiria vya ubadhirifu,” alisema.

Aidha, aliitaka kila halmashauri kuhakikisha taarifa za miradi ya maendeleo zinawekwa wazi kwenye mbao za matangazo ili wananchi wajue fedha zilizotengwa, kazi zinazotekelezwa na maendeleo ya miradi hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miliki wa TAKUKURU, Mhandisi Dk Emmanuel Kyabo, alisema mradi huo ulitekelezwa kwa mfumo wa Design and Build kupitia Shirika la Magereza (Prisons Corporation Sole), huku wataalamu wa TAKUKURU na Jeshi la Magereza wakisimamia kazi zote za usanifu na ujenzi.

Alisema mradi huo umehusisha kubomoa majengo manne ya zamani na kujenga jengo jipya la ghorofa moja, nyumba ya walinzi, kituo cha kupokelea umeme wa TANESCO na jenereta, uzio wa mita 310 pamoja na mfumo wa maji wenye tanki la kuhifadhi lita 60,000.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *