DODOMA: Serikali imezitaka jamii za ushirika nchini kuimarisha uwajibikaji, kutumia teknolojia za kidijitali na kuongeza ushiriki wa vijana na wanawake ili kuifanya sekta hiyo kuwa chachu ya maendeleo ya uchumi na kudumisha amani nchini.

Wito huo umetolewa leo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Profesa Peter Msoffe, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani 2026 yaliyofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre (JKCC) jijini Dodoma, yenye kaulimbiu isemayo “Ushirika kwa Dunia Yenye Amani.”

Profesa Msoffe amesema Tanzania ina historia ndefu ya mfumo wa ushirika ambao umeendelea kuwa nguzo muhimu ya kuwaunganisha wakulima, wafugaji, wavuvi na wajasiriamali, huku ukiwawezesha kupata mikopo, pembejeo za kilimo, elimu na masoko.

Amesema serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuimarisha sekta hiyo ikiwemo kuongeza matumizi ya TEHAMA na kuendelea kuimarisha mafunzo kupitia Chuo cha Ushirika Moshi.

“Nimeguswa na nilichokiona katika mabanda ya maonesho. Bidhaa na huduma za ushirika zenye thamani ya takribani Sh trilioni 4.95 zinaonesha mchango mkubwa wa sekta hii katika ukuaji wa uchumi wa taifa,” amesema.

Hata hivyo, amesema sekta hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo baadhi ya wanachama kutotambua umuhimu wa ushirika, vitendo vya ubadhirifu na rushwa, uhaba wa mitaji, ushiriki mdogo wa vijana, matumizi hafifu ya teknolojia pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amesema serikali itaendelea kuimarisha mapambano dhidi ya ubadhirifu na rushwa, kuongeza thamani ya mazao, kuwawezesha vijana na wanawake kushiriki katika shughuli za ushirika na kushirikiana na Chuo cha Ushirika Moshi pamoja na wadau wengine kutoa elimu ya usimamizi wa fedha na matumizi ya teknolojia.

Aidha, amewataka wanachama kushiriki kikamilifu katika shughuli za vyama vyao, kuchagua viongozi waadilifu, kulinda mali za ushirika na kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya ukiukwaji wa maadili.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dk Benson Ndiege, amesema mfumo wa ushirika umejengwa katika misingi ya demokrasia ambapo wanachama hushiriki kufanya maamuzi kuanzia ngazi ya vyama vya msingi hadi taifa.

Amesema utaratibu huo umeendelea kuimarisha mshikamano na amani huku ukiwawezesha wananchi, hususan wakulima, wafugaji na wavuvi, kuboresha kipato na ustawi wao kupitia shughuli za pamoja za kiuchumi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *