
Siku nne baada ya shambulio la waasi wa Muungano wa Uamsho wa Kizalendo (ASP), mji wa Am Dafok, katika mkoa wa Vakaga, ulitekwa tena Jumapili, Julai 5, na Vikosi vya Wanajeshi vya Jamhuri ya Afrika ya Kati (FACA) na washirika wao wa Urusi. Mji huu ulioko kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati, kwenye mpaka na Sudan, ulishambuliwa mnamo Juni 30.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Na mwandishi wetu huko Bangui, Rolf Steve Domia-Leu
ASP, kundi linaloundwa na waasi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) na mamluki wa kigeni, lilitangaza nia yake ya kuandamana dhidi ya Bangui. Shambulio la kujibu la FACA (Jeshi la Jamhuri ya Afrika ya Kati) na washirika wao lilizinduliwa yapata saa 10:00 alasiri na lilidumu kwa karibu saa mbili, kulingana na vyanzo vya kijeshi. Video zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha helikopta zikishambulia maeneo ya waasi, huku vikosi vya ardhini vikisonga mbele. Kulingana na gavana wa Vakaga, Jude Ngayoko, mji huo sasa umekombolewa: “Eneo ambalo lilikuwa likishikiliwa na adui linachukua muda ili kuweza kuliteka tena. Imekuwa siku nne kwa mikakati ya pamoja, na leo tunashikilia mji huu. Hali sasa imedhibitiwa.”
Mkuu wa Wakaga anabaini sasa ni wakati wa kuimarisha usalama katika eneo hili la mpaka. “Nitaomba serikali ifanye juhudi kwa sababu adui ameelimika. Serikali lazima ihakikishe kwamba wanajeshi wetu ni wataalamu, wamejiandaa vya kutosha, na wako kwa idadi ya kutosha kuwalinda ipasavyo wakazi wa Am Dafok.”
Katika taarifa, serikali ilitoa pongezi kwa ujasiri wa Vikosi vya Wanajeshi vya Jamhuri ya Afrika ya Kati (FACA) na washirika wao, huku ikithibitisha tena kujitolea kwake kulinda kila sehemu ya eneo la nchi.