DAR ES SALAAM: WANANCHI wameendelea kunufaika na huduma mbalimbali za afya zinazotolewa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), huku wakipata fursa ya kufanyiwa uchunguzi, kupatiwa ushauri wa kitaalamu na kujifunza mbinu za kujikinga dhidi ya magonjwa.

Banda la MUHAS limekuwa kivutio kwa mamia ya wananchi wanaotembelea maonesho ya Sabasaba jijiji Dar es Salaam kutokana na huduma zinazotolewa na wataalamu wa afya kutoka chuoni hapo, zikiwemo huduma za afya ya kinywa na meno, ushauri wa kitaalamu pamoja na maonesho ya bidhaa mbalimbali za dawa asili zinazofanyiwa utafiti na kutengenezwa na chuo hicho.

Katika huduma za afya ya kinywa na meno, wananchi wanapatiwa elimu kuhusu namna ya kutunza afya ya kinywa, kufanyiwa usafishaji wa meno na kupewa ushauri unaoweza kusababisha magonjwa ya fizi.

Akizungumza jana na HabariLeo, Mteknolojia wa Meno, Yugin Komba alisema watu wanaopoteza meno kutokana na ajali, magonjwa au uzee wanapatiwa elimu kuhusu huduma za meno bandia yenye ubora.

Alisema zipo hatua muhimu zenye ubora za kutumia meno bandia yaliyozingatia vipimo vya mgonjwa, namna ya kuyatunza na umuhimu wa kupata huduma hiyo kutoka kwa wataalamu wenye sifa ili kuhakikisha yanakuwa salama na imara.

“Pia kuna watu wanapenda urembo kama unataka jino liwe na rangi fulani, pia tunawapa wananchi hiyo huduma,” amesema Komba.

Kwa upande wake, Meneja Kliniki ya Kinywa na Meno, Abel Msaki alisema huduma ya uchunguzi wa kinywa na meno inatolewa bure, lengo kuhakikisha wananchi wanajitokeza kupata huduma na ushauri wa afya ya kinywa na meno.

Msaki alisema baada ya kufanya uchunguzi, wananchi wanapatiwa ushauri wa kitaalamu kulingana na changamoto waliyogundua, lakini pia njia sahihi na bora za kuendelea kulinda kinywa na meno.

“Pale mtu anapokuwa na chagamoto kubwa zaidi inayohitahi ‘resource’ zaidi tunampa rufaa,” alisema Msaki.

Aidha, MUHAS imeendelea kuonesha mafanikio yake katika tafiti za dawa asili kwa kuwatambulisha wananchi bidhaa mbalimbali zinazotokana na mimea tiba.

Wataalamu wanaeleza hatua zinazofuatwa kuanzia utafiti wa kisayansi, uchakataji wa malighafi, upimaji wa ubora na usalama hadi utengenezaji wa dawa hizo kwa kuzingatia viwango vinavyolenga kuhakikisha zinakuwa salama kwa matumizi ya binadamu.

Akizungumzia kuhusu namna walivyojiandaa kuhudumia wananchi, Mfamasia na Mtafiti, Natorias Mgaya alisema dawa hizo zimepatikana kutokana na uchunguzi kutoka kwa jamii na machapisho ya kisayansi.

“Kazi yetu kubwa ni kufanya utafiti, kisha uchakataji, kuangalia ufanisi na usalama wa dawa, pia tunaweza kujua mmea upi ni salama,” amesema Mgaya.

Amesema kupitia tafiti hizo, wamefanikiwa kupata dawa mbalimbali, ikiwemo dawa asili inayokinga mionzi ya jua. Pia dawa inayokinga fangasi na upele.

Pia dawa ambazo zinakinga changamoto ya gesi tumboni na vidonda vya tumbo.

“Pia tuna dawa kwa ajili ya pumu unatumia na unapata unafuu kwa muda mrefu, pia tuna dawa ya tezi dume inasaidia kupunguza ukubwa,” amesema Mgaya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *