Polisi ya Afrika Kusini imethibitisha kuwa kifo cha raia wa Nigeria akiwa korokoroni hakikutokana na maandamano dhidi ya wahamiaji wa kigeni nchini humo yaliyofanyika wiki iliyopita.

Maafisa hao wa usalama wamedai kuwa mwanaume huyo aliaga dunia baada ya kuzirai kwa sababu alikamatwa akiwa na dawa za kulevya ambazo inadaiwa alilenga kuiba.

Wizara ya Masuala ya Kigeni ya Nigeria Jumapili iliyopita ilidai kuwa raia huyo aliaga dunia wakati akihojiwa na polisi wa Afrika Kusini kuhusu tukio hilo.

Iliongeza kuwa mahojiano hayo yalifanyika siku mbili baada ya maandamano makubwa dhidi ya wahamiaji haramu.

Maandamano hayo ya wiki iliyopita yaliwalenga hasa raia wasiokuwa na vibali rasmi na yaliishia katika ghasia kwenye baadhi ya maeneo.

Nigeria imetishia kuchukua hatua ambayo haijawekwa wazi iwapo raia wake wataendelea kuuawa nchini Afrika Kusini.

Kampeni ya kupinga wahamiaji nchini Afrika Kusini tayari imewalazimisha maelfu ya raia wa kigeni kurejea makwao, ikiwa ni pamoja na raia wa Ghana, Malawi, Msumbiji na Nigeria.

Kambi za muda zimeongezeka katika mji wa bandari wa Durban na mji mkuu wa kifedha, Johannesburg huku maelfu ya wageni wakisubiri usafiri wa kurudi katika nchi zao, jambo ambalo limefafanya makundi ya misaada ya kibinadamu kutoa onyo kuhusu mgogoro mkubwa wa binadamu.

Matukio ya ghasia yaliyopita yaliyowalenga raia wa kigeni wasio na vibali yamekuwa mabaya sana, na watu 62 waliuawa katika ghasia za mwaka wa 2008.

Ghasia za mwaka 2019 zilishuhudia makundi ya watu waliokuwa na silaha yakishambulia biashara zinazomilikiwa na wageni karibu na Johannesburg, na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 12.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *