Morogoro. Licha ya Tanzania kuwa na hekta milioni 48.1 za misitu na kuorodheshwa miongoni mwa nchi 12 duniani zenye utajiri mkubwa wa bayoanuai, Serikali imezitaka taasisi, sekta binafsi, wadau wa maendeleo na wananchi kuongeza kasi ya juhudi za kurejesha ardhi na misitu iliyoharibika ili kufikia lengo la kitaifa la mwaka 2030.

Wito huo umetolewa leo Alhamisi, Julai 9, 2026 na Naibu Katibu Mkuu (Muungano), Ofisi ya Makamu wa Rais, Abdalah Mitawi, wakati akifungua warsha ya kujenga uwezo wa kikosi kazi cha Taifa cha urejeshaji wa ardhi na misitu Iliyoharibika iliyofanyika katika Manispaa ya Morogoro.

Mitawi amesema Tanzania hupoteza wastani wa hekta 469,000 za misitu kila mwaka, hali inayochangia uzalishaji wa zaidi ya tani milioni nne za hewa ya ukaa na kuongeza hatari ya kuenea kwa jangwa katika zaidi ya asilimia 61 ya eneo la nchi.

Amesema kupitia mpango wa AFR100, Tanzania imejiwekea lengo la kurejesha hekta milioni 5.2 za ardhi na misitu iliyoharibika ifikapo mwaka 2030.

Kwa mujibu wake, tathimini ya mwaka 2024 inaonyesha tayari hekta milioni 3.3 zimerejeshwa, hivyo bado kuna kazi kubwa ya kuhakikisha lengo lililobaki linafikiwa ndani ya muda uliopangwa.

Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais, Abdalah Mitawi kushoto akizungumza jambo katika ufunguzi wa mkutano wa wadau wa urejeshaji mandhari ya misitu uliyofanyika Manispaa ya Morogoro. Picha na Juma Mtanda.

“Tunapaswa kuongeza kasi ya utekelezaji ili kufikia na kuvuka lengo tulilojiwekea. Hili linahitaji ushiriki wa Serikali, sekta binafsi, wadau wa maendeleo na wananchi,” amesema Mitawi.

Amesema ongezeko la watu linazidi kuongeza shinikizo kwa rasilimali za mazingira, huku shughuli za kibinadamu, ikiwamo ukataji holela wa miti, kilimo kisicho endelevu, ongezeko la mifugo na uchimbaji usiozingatia mazingira, zikiendelea kuwa chanzo kikuu cha uharibifu wa misitu na vyanzo vya maji.

Akifafanua utekelezaji wa mpango huo, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais, Thomas Chali amesema bado kuna takribani hekta milioni 1.9 zinazopaswa kurejeshwa ili kufikia lengo la hekta milioni 5.2 ifikapo mwaka 2030.

Amesema mafanikio ya mpango huo yatategemea ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, sekta binafsi, wadau wa maendeleo na wananchi.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Vyanzo vya Mbegu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Dk Fortunata Senya amesema Serikali imeandaa Mkakati wa Taifa wa Urejeshaji wa Mandhari ya Misitu wa mwaka 2023–2030 ili kuongoza utekelezaji wa lengo hilo.

Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais, Abdalah Mitawi (kushoto), Kaimu meneja vyanzo vya Mbefu TFS, Dk Fortunata Senya (katikati) wakisikiliza jambo kutoka kwa Mratibu wa kitaifa wa mradi wa urejeshaji endelevu wa mazingira na hifadhi ya bayoanuai Tanzania, Dk Damas Mapunda. Picha na Juma Mtanda.

Amesema juhudi za kurejesha misitu haziwezi kufanikiwa kwa Serikali pekee, bali zinahitaji ushiriki mpana wa wadau mbalimbali, wakiwamo taasisi za utafiti, sekta binafsi, mashirika ya maendeleo na wananchi.

“Tumekusanya wadau wenye uwezo tofauti; wengine watachangia fedha, wengine utaalamu, vifaa na uzoefu. Pia tunaanzisha jukwaa la kitaifa litakaloratibu utekelezaji, kubadilishana uzoefu na kufuatilia maendeleo ya mpango huu. Tunaamini tukishirikiana tunaweza kufikia na hata kuvuka lengo la hekta milioni 5.2,” amesema Dk Senya.

Naye mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (Tafori), Joshua Maguzu amesema taasisi hiyo inaendelea kufanya tafiti za kubaini aina sahihi za miti zinazofaa kupandwa katika maeneo mbalimbali ya nchi, kulingana na hali ya udongo na tabianchi.

Amesema matokeo ya tafiti hizo yanawasaidia wataalamu na wananchi kuchagua miche inayostawi vizuri katika mazingira husika, hatua inayoongeza mafanikio ya juhudi za urejeshaji wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Tafiti zetu zinafanyika katika kanda mbalimbali za nchi ili kuhakikisha kila eneo linapata aina ya miti inayolingana na mazingira yake. Hii itaongeza ufanisi wa juhudi za kurejesha misitu na kuhifadhi bayoanuai kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo,” amesema Maguzu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *