
BAADA ya Zanzibar kuwa wenyeji wa mashindano ya mchezo wa Kabaddi Afrika, shirikisho la mchezo huo kisiwani hapa limesema hiyo itakuwa fursa kushiriki mashindano ya dunia kwa upande wa wanaume baada ya awali wanawake kuipeperusha bendera kimataifa.
Mashindano hayo ya Afrika yamepangwa kufanyika kuanzia Agosti 1 hadi 14 mwaka huu ambapo wachezaji 18 wataunda timu ya taifa ya wanaume itakayoiwakilisha Zanzibar.
Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Msaidizi wa Shirikisho la Kabaddi Zanzibar, Ramadhan Mrisho, amesema timu ya wanaume haijawahi kupata nafasi hiyo, hivyo wataitumia vizuri fursa ya kuwa wenyeji kuandika historia.
“Timu ya Taifa ya wanaume ilishiriki mashindano ya Afrika 2024 na ikashika nafasi ya tatu, kwa maana hiyo haijawahi kushiriki mashindano ya dunia,” amesema.
Amesema Zanzibar imekuwa mwenyeji wa mashindano hayo kutokana na wasifu ilioutengeneza juu ya mchezo huo.
Alifafanua kuwa, kati ya nchi 10 ambazo zinashiriki, Zanzibar ipo nafasi ya tatu kitakwimu huku ya kwanza ikichukuliwa na Kenya, kisha Uganda, huku Tanzania Bara ni ya nne. Zinazofuatia ni Burundi, Rwanda, Afrika Kusini, Zambia, Malawi na Mauritius inamaliza kumi bora.
Alieleza, katika maandalizi ambayo watafanya, watahakikisha wanawapokea wageni vizuri na watashirikiana na wadau mbalimbali ili kulikamilisha jambo hilo.