
ALIYEKUWA kocha wa Simba, Dylan Kerr amefichua kuwa kocha mpya wa Yanga, Manqoba Mngqithi ana uwezo mkubwa wa kiufundi na uzoefu ambao unaweza kuisaidia timu hiyo ya wananchi kuendelea kufanya vizuri katika ligi ya ndani na kimataifa, huku wakipewa tahadhari kubwa ya kuishi naye.
Kerr ambaye alikuwa akifanya kazi Afrika Kusini katika kipindi ambacho Mngqithi alikuwa sehemu ya benchi la ufundi la Mamelodi Sundowns, amesema anafahamu vizuri uwezo wa kocha huyo kutokana na kiwango alichokionyesha akiwa ndani ya moja ya klabu kubwa zaidi barani Afrika.
Manqoba anatua nchini akiwa kocha ambaye amefanikiwa zaidi baada ya kufanya vizuri zaidi kwenye soka la Afrika kwa kipindi chake.
Kocha huyo Mwingereza alisema Mngqithi ana uzoefu mkubwa wa kusimamia timu yenye presha kubwa ya mafanikio na matarajio makubwa, jambo ambalo anaamini litakuwa faida kwake wakati akianza kazi mpya ya kuinoa Yanga ambayo pamoja na kila msimu kutaka ubingwa wa Ligi Kuu Bara bado inataka kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Wakati Kerr akizinoa klabu za Baroka FC, Black Leopards, Tshakhuma Tsha Madzivhandila na Moroka Swallows kuanzia mwaka 2020 hadi 2022, Mngqithi alikuwa akiendelea kujenga historia yake ndani ya Mamelodi Sundowns akiwa katika nafasi tofauti kuanzia kwenye jopo la makocha wasaidizi, kocha mwenza hadi kocha mkuu.
“Kiukweli ni kocha mwenye uwezo mkubwa sana, amefanya kazi katika mazingira magumu yenye ushindani mkubwa na amekuwa sehemu ya mafanikio makubwa ya Sundowns. Kama atapata ushirikiano wa kutosha, hakuna kitu kitakachomzuia kufanya vizuri Yanga ingawa wanatakiwa kumsikiliza kwa kuwa ana misimamo yake mikali kwa ajili ya kujenga,” alisema Kerr.
Mngqithi alianza kujijengea jina katika soka la Afrika Kusini akiwa kocha wa Golden Arrows kabla ya kujiunga na Mamelodi Sundowns mwaka 2014 kama msaidizi wa kocha, nafasi ambayo ilimpa nafasi ya kufanya kazi na baadhi ya makocha wakubwa.
Akiwa Sundowns, Mngqithi alikuwa sehemu ya kizazi kilichobadilisha historia ya klabu hiyo na kuifanya kuwa moja ya timu zenye nguvu zaidi Afrika, akishiriki katika mafanikio mbalimbali ya ndani na kimataifa.
Mwaka 2016 alikuwa sehemu ya benchi la ufundi lililoisaidia Sundowns kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuifunga Zamalek ya Misri katika fainali, mafanikio yaliyoipeleka timu hiyo kwenye Kombe la Dunia la Klabu.
Baada ya miaka kadhaa akiwa kocha msaidizi, Mngqithi alipandishwa kuwa kocha mwenza wa Sundowns mwaka 2020 pamoja na Mokwena ambapo wawili hao waliendelea kuiongoza klabu hiyo kutawala soka la Afrika Kusini ambalo awali lilikuwa limetekwa na Kaizer Chiefs na Orlando Pirates.
Katika kipindi chake akiwa ndani ya benchi la ufundi la Mamelodi kuanzia mwaka 2013, Mngqithi alihusika katika mafanikio makubwa ya klabu hiyo, ikiwemo kutwaa mataji matatu ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL) akiwa kwenye benchi la ufundi.
Sundowns ilitwaa ubingwa wa PSL msimu wa 2015/16, 2017/18 na 2018/19 wakati akiwa msaidizi wa kocha, kabla ya kuongeza mataji mawili zaidi ya ligi msimu wa 2020/21 na 2021/22 akiwa pamoja na Rhulani Mokwena.
Mwaka 2024 alipewa jukumu la kuwa kocha mkuu wa Mamelodi Sundowns baada ya mabadiliko ya benchi la ufundi, lakini baadaye aliachana na klabu hiyo baada ya kipindi kifupi akiwa kwenye nafasi hiyo.
Licha ya kuondoka Sundowns, rekodi ya Mngqithi bado inaonyesha uzoefu mkubwa wa kufanya kazi kwenye kiwango cha juu, hasa kutokana na muda mrefu alioutumia ndani ya klabu hiyo yenye mfumo mkubwa wa kitaalamu.
Kerr anaamini uzoefu huo unaweza kuwa silaha kubwa kwa Yanga ambayo imekuwa ikihitaji kocha mwenye uwezo wa kuiongoza kwenye mashindano ya ndani na pia kusaka mafanikio makubwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ujio wa Mngqithi unaongeza matumaini kwa mashabiki wa Yanga ambao wanataka kuona timu yao ikiendelea kutawala soka la Tanzania na kuongeza ushindani kwenye nguvu yao ya ushindani katika michuano ya kimataifa.
ALIINYIMA USINGIZI KAIZER CHIEFS
Mngqithi hajatua Yanga kutokana na kutokuwa na chaguo lingine kabla ya kuamua kuja Tanzania alikuwa akitajwa kuhusishwa na baadhi ya klabu kubwa Afrika Kusini, ikiwemo Kaizer Chiefs ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikivutiwa na uwezo wake.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 53 alithibitisha kuwa Chiefs ilikuwa na nia ya kumchukua mara kadhaa, lakini mazungumzo hayo hayakufikia hatua ya mwisho kutokana na kile alichodai kuwa kulikuwa na watu waliokuwa wakizuia mpango huo.
“Chiefs walikuwa na nia na mimi, siwezi kusema haikuwa hivyo. Lakini haikufikia hatua ya mwisho kwa sababu kuna watu ambao walizuia hilo kutokea. Kuna watu ambao wanaweza kusema vibaya kuhusu mtu na kufanya mambo yasifike mwisho,” alisema Mngqithi katika mahojiano na Radio 2000 ya Afrika Kusini.
Alisema hilo halikuwa tukio la kwanza kwa Kaizer Chiefs kuonyesha nia kwake, akieleza kuwa hata kabla ya kujiunga na Sundowns mwaka 2014, klabu hiyo ya Soweto ilikuwa imeonyesha kuvutiwa naye na aliwahi kuwasilisha mipango yake ya kiufundi kwa uongozi wa timu hiyo.
“Kabla sijajiunga na Sundowns, Chiefs walinitaka sana. Nimekuwa na mazungumzo mazuri na hata viongozi wao akiwemo Kaizer Motaung. Najua wamekuwa wakionyesha nia kwangu, lakini kwa sababu mbalimbali haikutokea,” aliongeza.
STEVE BARKER ANAMFAHAMU
Kocha huyo anatua nchini akiwa anakutana na kocha mwingine mwenye historia kubwa kwenye soka la Afrika Kusini, Steve Barker wa Simba ambaye aliwika zaidi akiwa na Stellenbosch ya nchini humo wakiwa wameshakutana mara kwa mara uwanjani.
Katika michezo 10 tofauti ambayo wamekutana, Mngqithi aidha akiwa kocha mkuu au msaidizi ameshinda mechi sita, Barker ameshinda mbili, huku mbili wakitoka sare, hata hivyo ubabe wao utaanza kuonekana kwenye mchezo wa Ngao yta Jamii watakapokutana Agosti 12, 2026 na baadaye kwenye michezo ya Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho CRDB kama wote watakuwepo.
MKALI, ANA MISIMAMO
Vyanzo mbalimbali kutoka Afrika Kusini vinasema kuwa ni kocha ambaye anapenda kukaa kwenye timu moja muda mrefu lakini ana misimamo mikali na hapendi mchezaji mmoja au kikundi cha wachezaji kujiona mastaa kwenye timu yake.
“Ni kocha mkali sana, hapendi mchezaji kujiona staa, lakini pia anahusudu sana nidhamu hata wakati akiwa Mokwena waliwezana kwa kuwa wote walikuwa na tabia sawa, hawapendi masihara, lakini pia anataka wachezaji wanaofuata kila anachotaka yeye. Kwa Yanga itabidi wabadilike kwa kuwa staili yake ya kufundisha ni pasi nyingi, soka la burudani lakini safu ya ulinzi imara lakini anapenda kuwa na mshambuliaji mmoja bora,” kilisema chanzo kutoka Afrika Kusini.
SABABU YA DILI LA FADLU KUFA
Awali kabla ya Yanga kumfuata kocha huyo ilianza mazungumzo na Fadlu Davids ambaye alikuwa kocha wa zamani wa Simba, lakini inaelezwa kuwa dili hilo lilikufa kutokana na ukubwa wa benchi alilokuwa anataka kuja nalo Fadlu Dar.
“Ni kweli kwamba tulikuwa na mazungumzo na Fadlu awali kabla ya huyu lakini dili lilikufa kwa kuwa Yanga ina uwezo wa kumudu mwalimu anayekuja watu watatu tu, sasa Fadlu alitaka kuja na watu watano kwenye benchi lake.
”Kocha wetu aliyetupa ubingwa msimu uliopita Abdihamid Moallin anabaki kwa kuwa bado tuna mkataba naye na haya ni makubaliano yetu na Mngqithi yeye atakuja na watu watatu pekee kwenye benchi lake.” kilisema chanzo hicho cha uhakika.