
Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran, Hujjatul Islam Gholam Hossein Mohseni Ejei, amesema kuwa chombo hicho kitaendeleza hatua za kisheria za kufuatilia uhalifu uliofanywa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu wa Iran, akisisitiza kwamba wahusika wa uhalifu wa kivita lazima waadhibiwe na walazimishwe kulipa fidia.
Ejei amesema hayo katika mkutano na wanasheria kadhaa wa kimataifa na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wabobezi wa kufuatilia uhalifu wa kivita, ambapo ametoa wito wa kuunganisha juhudi za kisheria za kimataifa ili kuwawajibisha wale wote waliohusika na jinai zinazofanywa dhidi ya watu.
Amesema: “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kuzingatia kanuni zake za kidini na kikatiba, inaendelea kuwatetea watu wanaokandamizwa, ikisisitiza kuendelea kuwaunga mkono watu wa Palestina na Lebanon katika kukabiliana na mashambulizi ya utawala ghasibu na vamizi (Israel).”
Hujjatul Islam Mohseni Ejei ameongeza: Iran inatambua mashambulizi dhidi ya watu wake yaliyofanywa na Marekani na utawala wa Kizayuni kuwa ni uhalifu wa kivita unaohitaji kufuatiliwa kisheria, akieleza kuwa vyombo vya mahakama vyenye mamlaka, hasa Ofisi ya Mashtaka ya Umma, Idara ya Kimataifa na Kituo cha Wanasheria wa Mahakama, vinafuatilia kesi hizi kwa ushirikiano na mawakili na wataalamu wa sheria kutoka nchi mbalimbali.
Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran ameeleza kwamba nchi yake inafanya jitihada za kufungua awamu mpya katika kuwashtaki wahalifu wa kivita katika ngazi zote za kisheria na kimataifa, akisisitiza kwamba ushawishi wa baadhi ya mataifa makubwa ndani ya taasisi za kimataifa hautaizuia Iran kuendeleza njia hii hadi haki itakapopatikana.
Pia ametoa wito wa kufichua uhalifu wa Marekani na Israel mbele ya maoni ya umma wa kimataifa, pamoja na kuufuatilia katika mahakama za kimataifa, akieleleza kuwa kazi ya kurekodi uhalifu huo ni jukumu la kisheria na kimaadili la kulinda na kuhifadhi haki za watu kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Hujjatul Islam Ejei amesisitiza kwamba watu wa Iran wataendelea kudai haki ya kulipiza kisasi kwa damu ya kiongozi wa taifa aliyeuawa shahidi na mashahidi wote, na kwamba Iran haitarudi nyuma au kulegeza kamba kuwafuatilia wale wote waliohusika na uhalifu huo, na itafanya kazi ili kupata haki na fidia kwa uharibifu uliosababishwa kwa watu wa Iran.