Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo asubuhi vimetekeleza operesheni ya pamoja ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani nchini Jordan, Kuwait, Qatar, Oman na Bahrain, ikiwa ni hatua ya kujibu mashambulizi endelevu ya Marekani dhidi ya maeneo ya kusini mwa Iran.

Katika taarifa ya pamoja, vikosi vya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na Jeshi la Iran vimetoa onyo kali kuwa hatua yoyote ya ziada ya Marekani itakabiliwa na jibu kali zaidi.

Katika taarifa iliyotolewa mapema Jumapili, Ofisi ya Uhusiano wa Umma ya IRGC imesema kuwa Marekani imethubutu “kujaribu tena kile ambacho tayari kimekwisha jaribiwa” kwa kuilazimisha serikali ya Oman na kuchochea mvutano kupitia “harakati haramu” ya meli kadhaa kusini mwa Lango la Hormuz.

IRGC imeongeza  kuwa, Jeshi la Majini la Iran limefanikiwa kuzima jaribio hilo kwa “jibu madhubuti.”

Taarifa hiyo imebainisha zaidi kuwa Marekani ilianzisha mashambulizi ya anga dhidi ya vituo kadhaa vya mwambao na minara ya mawasiliano kando ya pwani ya kusini ya Iran kama majibu ya kushindwa huko.

Kulingana na IRGC, Kikosi cha Anga cha RGC kimelenga miundombinu muhimu ya kijeshi ya Marekani katika Kambi ya Anga ya Mwanamfalme Hassan nchini Jordan wakati wa awamu ya kwanza ya operesheni hiyo ya kulipiza kisasi.

IRGC imeongeza kuwa wakati wa awamu ya pili ya operesheni yake ya kulipiza kisasi, makombora yake ya balistiki pia yamelenga kambi ya kimkakati ya Marekani ya Al Udeid nchini Qatar, na kuharibu kituo cha matengenezo na ukarabati wa ndege za kivita pamoja na kamandi ya kambi hiyo.

Taarifa hiyo imeonya kuwa: “Adui wa Kimarekani na Kizayuni anapaswa kufahamu kuwa mwendelezo wa uchokozi wake utaleta majibu ya kusambaratisha zaidi. Sisi tuko tayari kwa lolote.”

Katika taarifa tofauti, Ofisi ya Uhusiano wa Umma ya Jeshi la Iran imetangaza kuwa imevurumisha ndege zisizo na rubani za kujitoa muhanga dhidi ya vituo vya kijeshi vya Marekani nchini Kuwait na Bahrain, ikiwa ni jibu la mashambulizi ya mara kwa mara ya Marekani katika maeneo ya kusini mwa Iran.

Jeshi limesema ndege zake zisizo na rubani zililenga mfumo wa ulinzi wa anga wa Patriot, ghala la silaha, na kituo cha rada cha kijeshi cha Marekani nchini Kuwait.

Aidha, wimbi lingine la ndege zisizo na rubani lililenga mfumo wa mawasiliano ya kijeshi ya Marekani na kituo cha rada nchini Bahrain.

Kwingineko, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi (IRGC) limetangaza kuambaratisha vituo vya usambazaji na ukarabati wa meli za kivita za Marekani nchini Oman

Katika taarifa yake, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limetangaza kuwa limefanikiwa kusambaratisha vituo vya usambazaji wa vifaa (logistics) na majukwaa ya kuongeza mafuta ya meli za kivita za Marekani katika Bandari ya Duqm nchini Oman, kupitia shambulizi zito na la kushtukiza.

“Azimio lenu dhabiti, ambalo lilidhihirika wazi katika maandamano ya kihistoria ya mamilioni ya watu yaliyoushangaza ulimwengu, sasa limejionyesha kupitia ushujaa wa wapiganaji wenu.”

Katika awamu ya tatu ya jibu la operesheni dhidi ya uchokozi wa jeshi la Marekani—jeshi ambalo limekuwa likiua watoto—wapiganaji wa Jeshi la Anga la IRGC wamevipiga na kuviharibu vibaya vituo vya usambazaji wa vifaa vya meli hizo na majukwaa ya kuongeza mafuta ya meli za kubeba ndege za Marekani katika Bandari ya Duqm, Oman, kupitia shambulizi zito na la kushtukiza.

Operesheni hizi za kulipiza kisasi zimekuja saa chache baada ya jeshi la Marekani kuanza tena vitendo vya uchokozi visivyo na sababu dhidi ya kusini mwa Iran. Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) imesema kuwa imetekeleza mashambulizi hayo kwa amri ya Rais wa Marekani Donald Trump, kwa lengo linalodaiwa la kupunguza uwezo wa Iran wa kudhibiti Lango la Hormuz.

Muda mfupi kabla ya tangazo hilo, wakazi katika miji ya bandari ya Asalouyeh na Bandar Dayyer katika Mkoa wa Bushehr waliripoti kusikia milipuko kadhaa.

Lango la Hormuz limefungwa hadi Marekani itakapokoma kuingilia mambo

Wakati huo huo, Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limetangaza kufungwa kwa Lango la Hormuz “hadi hapo taarifa nyingine itakapotolewa,” likisisitiza kuwa njia hiyo muhimu ya maji itabaki imefungwa hadi pale Marekani itakapokomesha uingiliaji wake wa kijeshi katika eneo hili.

Katika taarifa yake ya Jumamosi, Jeshi la IRGC limesema hatua hiyo imechukuliwa “kufuatia hali ya usalama iliyosababishwa na uingiliaji haramu wa madola ya kigeni.”

Jeshi la IRGC limeonya dhidi ya uchokozi wowote wa kijeshi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kwa kisingizio cha kufungwa kwa njia hiyo ya maji, jambo ambalo adui mwenyewe ndiye anayepaswa kulaumiwa kwa kusababisha hali hiyo.

Aidha IRGC imeongeza kuwa, dhima ya madhara yoyote yatakayotokea itabebwa na Marekani, utawala wa Israel, na nchi wenyeji wa kambi za kijeshi zinazotumiwa kutenda uovu dhidi ya Iran.

Awali, Jeshi la IRGC liliripoti kuwa lililazimika kufyatua risasi ya onyo dhidi ya chombo kimoja cha majini baada ya meli kadhaa kupuuza maelekezo yake kuhusu usafiri katika lango hilo.

Wakati huohuo, jeshi hilo limekumbusha jinsi lilivyokuwa limeonya mapema kwamba “uingiliaji wa kigeni na utumizi haramu wa njia za meli katika Lango la Hormuz utasababisha jibu madhubuti na kutatiza mtiririko wa usafiri wa baharini unaoongezeka katika lango hilo.”

Iran ilifunga njia hiyo ya kimkakati kwa maadui na washirika wao kuanzia Februari 28, wakati tawala za Marekani na Israel zilipoanza wimbi lao la hivi karibuni la vita haramu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Katika upande mwingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, na mwenzake wa Oman, Sayyid Badr bin Hamad Al Busaidi, wamejadili mbinu za kuhakikisha usafiri salama wa meli kupitia Lango la Hormuz, kwa mujibu wa Ibara ya 5 ya Mkataba wa Islamabad (MoU) uliotiwa saini kati ya Tehran na Washington.

Katika mazungumzo yao yaliyofanyika Muscat siku ya Jumamosi, Araghchi alikutana na Al Busaidi ambapo wamejadili uhusiano wa nchi mbili hizo na matukio ya kanda, huku kipaumbele kikielekezwa kwenye Lango la kimkakati la Hormuz.

Al Busaidi amesisitiza msimamo thabiti wa Oman kuwa diplomasia ndiyo njia mwafaka ya kuzuia hali ya mambo kuzidi kuwa mbaya katika eneo hili.

Mawaziri hao wawili pia walibadilishana mitazamo kuhusu mbinu mwafaka za kuhakikisha vyombo vya majini vinapita kwa usalama katika Lango la Hormuz, kwa mujibu wa Ibara ya 5 ya Mkataba wa Maelewano wa Islamabad.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *