Iran: Lango-Bahari la Hormuz limefungwa kwa safari zote kufuatia hatua ‘haramu’ za kijeshi za Marekani

Mamlaka ya Lango -Bahari la Ghuba ya Uajemi (PGSA) imeeleza katika ujumbe mfupi uliotumwa kwenye akaunti yake ya X siku ya Jumapili, kwamba njia ya kupita katika Lango -Bahari la Hormuz kwa sasa imefungwa kutokana na harakati za kijeshi za hivi karibuni za Marekani katika eneo hilo.

“Kutokana na harakati zisizo halali za hivi karibuni za askari jeshi wa Marekani katika eneo hilo, ni jambo lilisowezekana kwa sasa kupita katika Lango-Bahari la Hormuz”, imesema taraifa ya Mamlaka ya Lango-Bahari la Ghuba ya Uajemi (PGSA).

Mamlaka hiyo imefafanua kuwa: Safari za meli zitaendelea kusimamishwa hadi utulivu na hali ya kawaida itaporejea katika eneo hilo.

Mamlaka ya Lango- Bahari la Ghuba ya Uajemi (PGSA) imesema: Mara tu utulivu na hali ya kawaida vitakaporejea, maombi yote yatafanyiwa tathmini kulingana na ratiba na vibali vinavyohitajika vitatolewa.  

PGSA imesisitiza kuwa njia pekee halali ya kupata vibali vya usafiri wa meli ni katika tovuti yake rasmi ya PGSA.ir, na kwa kwamba, ili kupata taarifa ya papo kwa hapo meli zote zinapasa zifuatilie akaunti yake kwenye mtandao wa kijamii wa X.

Katika taarifa yake juzi Jumamosi, Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kilitangaza kufungwa Lango-Bahari la Hormuz “hadi taarifa zaidi itakapotolewa,” kikisema njia hiyo ya baharini itaendelea kufungwa hadi pale Marekani itakapoacha uingiliaji kati katika eneo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *