Kufuatia mashambulizi ya mara kwa mara ya Marekani katika maji na maeneo ya kusini mwa Iran, Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kimetoa taarifa kikitangaza kujibu vikali vitendo vya uchokozi vya jeshi la Marekani.

Kulingana na taarifa ya IRGC, wakati wa awamu ya pili ya operesheni za kulipiza kisasi, kambi ya kimkakati ya anga ya Marekani huko Al-Udeid nchini Qatar, ambacho ni kitovu cha matengenezo ya ndege za kivita na kamandi ya operesheni za kikanda, ilipigwa na makombora kadhaa ya balestiki. Taarifa ya IRGC imetoa onyo la wazi kwamba “uchokozi unaoendelea wa Marekani utakabiliwa na majibu makali zaidi.”

Matukio haya yanajiri chini ya mwezi mmoja baada ya kutiwa saini hati ya makubaliano yenye vipengele 14 kati ya Tehran na Washington, makubaliano yaliyolenga kuhitimisha vita na uchokozi wa Marekani dhidi ya Iran, kurejesha usafiri salama wa meli katika Lango la Hormuz na kuliepusha eneo hilo kutumbukia tena kwenye vita kamili.

Kufuatia kurejea kwa uchokozi wa Marekani, Mohammad Bagher Ghalibaf, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ambaye pia ni mkuu wa timu ya mazungumzo ya Iran, ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba: “Enzi za makubaliano ya upande mmoja zimekwisha. Tulikwambieni: Timizeni ahadi na wajibu wenu, la sivyo mtalazimika kulipa gharama. Sasa lazima mukubali ukweli.” Kwa kunukuu sehemu ya kifungu cha tano cha makubaliano hayo, ambacho kinasisitiza kufunguliwa tena kwa Lango-Bahari la Hormuz chini ya “usimamizi wa Iran”, ametuma ujumbe wa wazi kwa Washington Kwamba: Lango Bahari la Hormuz liko chini ya mamlaka ya Iran, na kuwa hakuna nchi yoyote ya kigeni inayoweza kufanya maamuzi ya upande mmoja kuhusiana na suala hilo. Ujumbe huu unaashiria mabadiliko ya kimsingi kwamba ukiukaji wa makubaliano hayo hautafanyika tena bila gharama.

Katika muktadha huu, ripoti ya uchanganuzi ya kituo cha Marekani “MSN” ina umuhimu mkubwa, kwani inaakisi picha ya vita ambayo ni tofauti na maelezo rasmi ya Ikulu ya Marekani.

Nicholas Grossman, mhadhiri wa taaluma ya siasa katika Chuo Kikuu cha Illinois na mwandishi wa ripoti hii, anamuelezea Donald Trump kama rais aliyeanzisha mgogoro lakini akashindwa kufikia malengo yake ya kimkakati, na ambaye sasa amezama kwenye mgogoro huo huo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Marekani imeshindwa kuilazimisha Iran ikubali masharti yake kandamizi; imeshindwa kubadilisha tabia zake, muundo wa kisiasa wa Jamhuri ya Kiislamu wala haijaweza kubuni upya mifumo ya usalama ya Ghuba ya Uajemi kwa maslahi ya Washington. Suala muhimu zaidi katika ripoti hii ni lile linalohusiana na pengo kubwa lililopo kati ya simulizi ya kisiasa ya White House na hali halisi ya mambo uwanjani. Trump anaendelea kuzungumzia “ushindi,” lakini hali halisi inaonyesha vinginevyo. Lango-Bahari la Hormuz linasalia kuwa nguzo muhimu zaidi ya kijiopolitiki katika eneo, ukosefu wa usalama baharini unaendelea, soko la kimataifa la nishati linakabiliwa na hali ya kutokuwa na utulivu na Marekani inalazimika kulipa gharama zaidi ya mgogoro iliojisababishia yenyewe.

Kifungu cha 5 cha Mkataba wa Islamabad kilipanga kufungua upya njia hii ya majini kwa mujibu wa “taratibu zilizowekwa na Iran,” lakini mzozo kuhusu tafsiri ya kifungu hicho umekuwa chanzo kikuu cha mvutano. Iran inasisitiza kutumia mamlaka yake ya kitaifa, kusimamia usafiri, na kutekeleza sheria za baharini, huku Marekani ikijaribu kupuuza taratibu hizo. Matokeo yake yamekuwa kuibuliwa mzozo mpya katika eneo.

Iran inamiliki ukanda mrefu zaidi wa pwani katika Ghuba ya Uajemi, Lango-Bahari la Hormuz, na Bahari ya Oman; hivyo ina haki ya msingi ya kutetea maslahi yake huru na kuhakikisha usalama wake wa taifa ndani ya Lango-Bahari la Hormuz, hasa kufuatia uchokozi wa Marekani na kuanzishwa vita vya siku arubaini dhidi yake.  Hata hivyo, utawala wa Marekani, ukiwa ungali una fikra zile zile za kikoloni na kimabavu dhidi ya mataifa mengine, inaendelea kuishi katika zama hizo na kutaka kuzitwisha nchi nyingine matakwa yake kwa kulazimisha udhibiti wake katika njia hii muhimu ya maji kijiopolitiki.

Rais wa Marekani “ameishiwa na fikra” ambapo sasa anarudiarudia tu mikakati iliyofeli huko nyuma. Katika fikra zake za kindoto, Trump anadai kuwa ni nguvu za Marekani ndizo zimeisukuma Iran kwenye meza ya mazungumzo. Hata hivyo, hali halisi ya mambo inaonyesha kuwa mambo ni magumu sana kwa Marekani katika Ghuba ya Uajemi, huku Iran ikiwa katika nafasi imara na nzuri zaidi.

Jibu la Trump kwa ukweli huu ni kujaribu kuugeuza na kuudhihirisha vingine. Hatua ya vikosi vya jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kujibu uchokozi wa Marekani, kwa kushambulia kambi zake katika nchi tano za eneo, imeonyesha wazi kuwa Iran inalinda mamlaka yake kwa nguvu zote na kwamba hatua yoyote ya makosa ya kimahesabu itakayochukuliwa na adui itajibiwa kwa hatua kali zaidi zinazoendelea kuongezeka. Kwa kukiuka Mkataba wa Islamabad, Marekani imechagua njia ambayo imezidisha mgogoro badala ya kuutatua, ambapo sasa inakabiliwa na hali halisi ya mambo, ambayo hata baadhi ya wachambuzi wa Marekani wanasema kuwa vita vilivyoanzishwa na nchi hiyo kwa matarajio ya kupata ushindi wa haraka vimegeuka kuwa jinamizi na mtego wa kimkakati kwa Washington. Huu ni mtego ambao unafanya kila hatua mpya ya uchokozi kuongeza gharama ya kujiondoa humo na hivyo kufanya matarajio ya kupatikana amani ya kudumu kuwa magumu zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *